Jack1 alishika nondo za mlango wa chumba chake cha gereza na kuchungulia kwenye ujia. Moyo wake ulienda mbio huku jasho likitiririka kwenye paji la uso wake. Je, aseme au asiseme? Kama askari wa zamani, alikumbuka mateso ya kikatili yaliyotendwa katika magereza ya kijeshi. Akiwa amekamatwa kwa kuhubiri Injili, sasa alikuwa upande usiofaa wa nondo.
Je, aseme? Angewezaje kutosema? Bwana wake alikuwa amemwamuru.
Akishika nondo kwa nguvu zaidi, alizungumza kwa sauti ya chini kwa walinzi wowote waliokuwa karibu. “Msiponiachilia, damu ya watu 50,000 itakuwa juu ya vichwa vyenu!” Akarudi mbio kwenye kona ya chumba, akisubiri kupigwa. Lakini hakupigwa kamwe. Nimefanya! Nimeshuhudia mbele ya wanaonishikilia mateka.
Siku iliyofuata, akishika nondo, alizungumza kwa sauti kubwa zaidi. “Msiponiachilia, damu ya watu 50,000 itakuwa juu ya vichwa vyenu!” Lakini tena hakuna adhabu iliyokuja.
Kila siku alirudia makabiliano haya na wanaomshikilia, sauti yake ikizidi kupaa kwa kila tamko. Walinzi wa gereza walimwonya anyamaze, lakini bila mafanikio.
Mwisho wa wiki, Jack alipaza sauti ili wote wasikie, “MSIPONIACHILIA, DAMU YA WATU 50,000 ITAKUWA JUU YA VICHWA VYENU!” Hili liliendelea kwa saa nyingi hadi hatimaye askari kadhaa walimkamata Jack na kumpakia katika lori la kijeshi.
Jack alitazama huku na huko kwa hofu akitarajia mwisho kufika muda si mrefu. Baada ya saa chache, lori lilisimama. Askari walimsindikiza hadi kando ya barabara. “Hatuwezi kuvumilia kelele zako zisizokoma! Uko kwenye mpaka wa wilaya. Ondoka hapa na usihubiri tena mahali hapa kamwe!”
Lori liliporudi likiyumbayumba kwenye barabara yenye vumbi, Jack alipepesa macho kwa mshangao. Alikuwa mwaminifu kwa wito wa kuhubiri habari njema katika nchi ambayo haikuwahi kusikia habari za Yesu. Bwana alikuwa amemwita na Bwana alikuwa amemlinda. Wiki chache baadaye, akiwa amejaa hisia ya uharaka na akiwa ametiwa ujasiri na ustahimilivu wa kiroho, Jack na ndugu mwingine walijipenyeza tena katika wilaya hiyo wakifichwa na giza ili kutii amri ya Mfalme mkuu. Muda si mrefu walimwongoza mtu wa kwanza kumwamini Yesu—mtu ambaye kupitia kwake Harakati ya Kupanda Makanisa ingezaliwa.
Sifa Zisizoshikika za Vichocheo vya CPM Wenye Matunda
Sifa mbili zisizoshikika hujitokeza juu tena na tena ambazo zinaonekana kuwatofautisha vichocheo wa Harakati za Kupanda Makanisa (CPM) wenye matunda zaidi na watenda kazi wengine wengi. Kama Jack katika gereza lile la Asia, sifa hizi zinaonekana wazi katika maisha ya Kristo na katika maisha ya wanafunzi wa Matendo ya Mitume. Ni vichocheo vinavyoonekana kumsukuma mtumishi wa Kristo anayekaa ndani yake kiroho kuelekea kuzaa matunda. Ingawa ni vigumu kuzifafanua, nitaziita “uharaka” na “ustahimilivu” (grit). Kwa madhumuni haya, ninafafanua uharaka kama kuishi kwa makusudi katika utume ukiwa na ufahamu kwamba muda ni mfupi. Ustahimilivu ni azimio thabiti na uwezo wa kudumu katika utume huo, mara nyingi licha ya vikwazo visivyoshindika.
Kwa kawaida hizi si sifa za kwanza tunazozitafuta kwa wapanda makanisa na wamisionari, kwa kawaida kwa sababu ya maana hasi zinazohusishwa nazo:
- Uharaka: “Anasukumwa kupita kiasi!”
- Ustahimilivu: “Ni mkaidi kupita kiasi!”
Inazidi kuwa nadra kupata watenda kazi katika ufalme (angalau katika ulimwengu wa Magharibi) wanaokabili utume wao kwa meno yaliyokazwa na hisia ya uharaka ambayo mara nyingi huwakosesha usingizi usiku. Tunawapendelea zaidi watu wenye “nafasi ya ziada” (margin). Hata hivyo yaelekea Yesu na Paulo wasingetoshea katika fasili zetu za watu wenye nafasi ya ziada inayofaa. Leo huenda tungewashauri “wapunguze mwendo,” watumie muda zaidi katika mambo yasiyo ya kazi na kurekebisha uwiano wa kazi na maisha yao.
Hata hivyo, wanaume na wanawake ambao kupitia kwao Mungu anazaa harakati za ufalme wanaonekana kutoijali kabisa dhana ya nafasi ya ziada kama tunavyoifafanua. Badala yake, utume wa Mungu unayameza maisha yao kama ulivyofanya kwa Yesu.
Wanafunzi wake wakakumbuka kwamba imeandikwa: “Wivu wa nyumba yako utanila.” (Yohana 2:17, ESV)
Wivu (bidii) ulikuwa sifa bainifu ambayo wanafunzi waliikumbuka kuhusu Yesu. Je, John Wesley, aliyeandika mahubiri akiwa juu ya farasi aliposafiri kutoka mkutano mmoja hadi mwingine, alikuwa na nafasi ya ziada ya namna hiyo? Je, harakati ingeibuka kama angekuwa nayo? William Carey alipohangaika huko Uingereza ili aachiliwe kwenda kutimiza Agizo Kuu, je, tungeyaelezea maisha yake kuwa maisha yaliyojaa nafasi ya ziada? Je, Hudson Taylor, Mother Teresa au Martin Luther King, Jr. wangetoshea katika fasili kama hizo?
Jim Elliot, aliyekufa shahidi, alisema:
“Huwafanya wahudumu wake kuwa mwali wa moto. Je, mimi ninaweza kuwaka? Mungu niokoe na ‘mambo mengine’ ya kutisha yasiyoshika moto kama asbesto. Nijaze mafuta ya Roho ili niwe mwali. Lakini mwali ni wa kupita, mara nyingi wa muda mfupi. Je, waweza kulivumilia hili, ee nafsi yangu—ndani yangu anakaa Roho wa Yule Mkuu Aliyeishi Muda Mfupi, ambaye wivu wa nyumba ya Mungu ulimla. ‘Nifanye kuni zako, Mwali wa Mungu. Mungu, nakuomba, washa vijiti hivi vilivyokaa bure vya maisha yangu na niwake kwa ajili yako. Yateketeze maisha yangu, Mungu wangu, kwa kuwa ni yako. Sitafuti maisha marefu, bali maisha kamili, kama wewe, Bwana Yesu.’”
Kukutana na vichocheo vya CPM leo huibua maelezo yanayofanana: shauku, uthabiti, azimio, kutotulia, kusukumwa, wivu, imani, kutokubali kuacha au kukubali “hapana” kama jibu. Ni wakati wa kuziinua tena sifa zisizoshikika za uharaka na ustahimilivu hadi kiwango tunachoziona katika Agano Jipya.
Je, zinaweza kupoteza uwiano? Bila shaka. Lakini rakaa imeyumba mbali mno upande wa pili.
Uharaka
Uharaka: kuishi kwa makusudi katika utume ukiwa na ufahamu kwamba muda ni mfupi
Yesu aliishi akiwa na hisia ya uharaka akijua kwamba muda wake wa huduma (miaka mitatu) ulikuwa mfupi. Tangu mwanzo hadi mwisho wa Yohana, Yesu anataja mara nyingi “saa” yake ya kuondoka ulimwenguni (k.m. Yohana 2:4, 8:20, 12:27, 13:1). Yesu alijua rohoni mwake kwamba siku zilikuwa chache na lazima aikomboe kila moja kwa ajili ya utume ambao Baba yake alimtuma.
“Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenituma maadamu ni mchana; usiku unakuja, ambapo hakuna mtu awezaye kufanya kazi.” (Yohana 9:4, ESV)
Kwa mfano, wakati wanafunzi walikuwa tayari kupiga kambi huko Kapernaumu baada ya mafanikio ya ajabu ya siku iliyotangulia, Yesu aliamua kinyume kabisa. Akijua kwamba utume wake ulikuwa kupita Israeli yote kabla ya kuondoka kwake, aliondoka ili kuanza hatua inayofuata ya safari.
“Akawaambia, ‘Twendeni katika miji inayofuata, ili nihubiri huko nako, kwa maana ndiyo sababu nilikuja.’ Akaenda katika Galilaya yote, akihubiri katika masinagogi yao na kutoa pepo.” (Marko 1:38-39, ESV; tazama pia Luka 4:43-44)
Mwenzangu mmoja anaelezea mtazamo huu kama “uharaka wa kipindi kimoja” akirejelea urefu wa kawaida wa kipindi cha huduma ya mmisionari (miaka 3-4).
Wataalamu wa leo huenda wangemwonya Yesu kuhusu “kuchoka kupita kiasi” (burn-out). Lakini shauku ya Yesu haikuwa kuchoka kupita kiasi bali “kuwaka hadi mwisho” au “kuteketea kabisa” katika wakati ule hasa ambao Baba alimchagulia. Kuwaka hadi mwisho kunaelezea kuishi kwa uharaka na nguvu ya mwendo wa Baba (sauti yake) kuelekea utume wa Baba (lengo lake) kwa ajili ya furaha ya Baba (furaha inayotokana na kujua kwamba tunampendeza na kufanya mapenzi yake—Yohana 4:34, 5:30).
Kuchoka kupita kiasi hakuhusiani sana na kuwa na nafasi ya ziada au kuikosa bali na ukosefu wa kuridhika kwa maisha yaliyotumika vizuri. Kila mtu leo ana shughuli nyingi; si kila mtu anaishi kwa makusudi. Maisha yenye shughuli nyingi yanayoishiwa bila lengo yanayumba kuelekea kuchoka kupita kiasi. Lakini maisha yaliyokita mizizi katika uwepo wa Baba na kwa ajili ya makusudi yake yanatoa uhai. Tunamaliza kila siku tukipokea pongezi ya Mungu: “Vema, mtumishi wangu mwema na mwaminifu.” Kuwaka hadi mwisho ni kuacha maisha yetu yatumiwe kabisa na Mungu kwa mwendo wake na kwa kuitikia misukumo yake na kumwacha ayamalize maisha yetu kwa wakati wake mwema.
Yesu anawasihi wanafunzi wake kuishi kwa njia inayofanana. Uharaka ulikuwa dhamira ya kawaida katika mifano ambayo Yesu aliwafundisha. Katika mfano wa karamu ya arusi (Mathayo 22:1-14) watumishi wanapaswa kuwalazimisha watu kuja karamuni kabla haijawa kuchelewa mno. Hakuna muda wa kupoteza. Katika mfano wa watumishi walio tayari, watumishi wanapaswa kubaki “wamejifunga viuno tayari kwa kazi” ili wakeshe wakingojea kurudi kwa Bwana wao (Luka 12:35-48).
Uharaka unamaanisha kwamba hatujui tuna muda kiasi gani, hivyo maisha yetu yanapaswa kuishiwa kwa makusudi, tukizikomboa siku.
Wanafunzi walibeba hisia hii ya uharaka pamoja nao katika juhudi za utume za Matendo ya Mitume. Safari tatu za Paulo za maelfu ya maili (kwa mwendo wa miguu) na makumi ya maeneo yaliyobanwa katika kipindi cha miaka 10-12 zinaleta kizunguzungu. Paulo alikuwa na utume (kuwahubiri Mataifa wote) na muda mchache wa kuutimiza. Ndiyo sababu alitumaini kutokawia Rumi bali kusafirishwa nao kuelekea Hispania ili pasibaki mahali pa kuweka msingi wa Injili (Warumi 15:22-24).
Uharaka wa kutimiza uwakili waliopewa na Mungu daima umewasukuma watumishi wa Mungu wenye matunda zaidi:
“Hivi ndivyo mtu anavyopaswa kutuhesabu, kuwa watumishi wa Kristo na mawakili wa siri za Mungu. Tena, inatakiwa kwa mawakili waonekane kuwa waaminifu.” (1 Wakorintho 4:1-2, ESV)
Ustahimilivu
Ustahimilivu: azimio thabiti na uwezo wa kudumu katika utume, mara nyingi licha ya vikwazo visivyoshindika
Rooster Cogburn (aliyeigizwa kwa ubora na John Wayne katika True Grit), bunduki zikifyatuka, anaibua picha za mtu anayekabiliana ana kwa ana na vikwazo visivyoshindika ili kutimiza utume. Lakini katika ulimwengu wa kiroho, ustahimilivu thabiti daima umekuwa sifa ya wanaume na wanawake ambao Mungu amewaita kuzindua harakati.
Utume wa Yesu wa kipindi kimoja haukuweza kuzuiwa. Uso wake ulikazwa kama jiwe gumu kuelekea taabu zilizomngoja Yerusalemu (Luka 9:51-53). Njiani, wengi walitangaza shauku yao ya kumfuata. Lakini mmoja baada ya mwingine, aliwapa changamoto kuhusu utayari wao wa kuhesabu gharama na azimio lao la kudumu katika njia (Luka 9:57-62). Ustahimilivu.
Ustahimilivu ulikuwa sifa ya mapambano ya Bwana wetu katika majaribu ya jangwani na katika saa ya mwisho ya Gethsemane—uwezo thabiti wa kudumu wa kupita katikati ya vikwazo visivyoshindika ili kufikia lengo ambalo Baba alikuwa ameliweka.
Yesu aliwasihi wanafunzi wake kuishi kwa ustahimilivu unaofanana—kutokubali “hapana” kama jibu. Bali, kama yule mjane aliyemsihi hakimu dhalimu, “imewapasa kumwomba Mungu siku zote, wala wasikate tamaa” (Luka 18:1-8, ESV).
Hivyo, wanafunzi katika Matendo ya Mitume yote waliendelea kusukuma ufalme kuelekea nje licha ya vikwazo vya ajabu. Stefano alipopigwa mawe na waamini wenzao kuburutwa gerezani (Matendo ya Mitume 8:3), walifanya nini? Walilihubiri neno walipotawanyika! Paulo, aliyepigwa mawe huko Listra, aliinuka mara moja na kuingia tena mjini kabla ya kuendelea hadi mahali palipofuata. Paulo na Sila wakiwa wamefungwa kwa nguvu katika gereza la Filipi waliimba sifa kwa Aliye Juu wakati hali zilipokuwa chini kabisa. Ustahimilivu wa kiroho uliwadumisha katika utume.
Ni hali gani zinaweza kutokea ambazo zingekufanya uache utume wa Mungu? Kiwango chako cha ustahimilivu ni kipi?
Siri za ustahimilivu zinaweza kupatikana katika azimio la Yesu la kuukabili msalaba: “Yesu… ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba, akiidharau [kwa kweli, akiihesabu kuwa si kitu] aibu.” (Waebrania 12:2, ESV)
Furaha ya kile kilichokuwa mbele yake—kumpendeza Baba yake, kutimiza utume wake, kuleta ukombozi—ilimwongoza kuihesabu aibu ya msalaba kuwa si kitu. Faida ilizidi sana hasara.
Paulo alieleza hisia zinazofanana: “Kwa sababu hiyo nayastahimili yote kwa ajili yao waliochaguliwa, ili nao waupate wokovu ulio katika Kristo Yesu pamoja na utukufu wa milele.” (2 Timotheo 2:10, ESV)
Faida kwa Paulo—kwamba watu wateule wa Mungu katika kila mahali wapate wokovu—ilizidi sana hasara ya kustahimili dhihaka, mapigo, vifungo, kuvunjikiwa na merikebu na kupigwa mawe. Ni maono ya faida ya utume pekee yatakayotuimarisha kwa ustahimilivu tunaouhitaji ili kustahimili hasara ya magumu ili kuufikia.
Kizazi chetu kina ndani ya uwezo wake nyenzo za kuanzisha kazi miongoni mwa kila kundi la watu wasiofikiwa lililobaki na kila mahali pasipofikiwa palipobaki kwa njia za CPM zenye matunda. Tuna ndani ya uwezo wetu nyenzo za kushinda kila kikwazo cha kutimizwa kwa Agizo Kuu na kurudi kwa Bwana. Lakini kizazi kama hicho kitainuka tu kitakapoazimia kumaliza kazi kwa hisia mpya ya uharaka, kikiwa kimeimarishwa na ustahimilivu ili kupenya kila kikwazo.
Musa, mtu wa Mungu, aliomba katika Zaburi 90:12: “Basi utufundishe kuzihesabu siku zetu ili tujipatie moyo wa hekima.”
Nini kingetokea kama kanisa la ulimwenguni kote lingetambua kwamba muda ni mfupi? Itakuwaje kama tungeweka tarehe ya kukamilisha kuanzisha kazi miongoni mwa kila kundi la watu kwa mkakati madhubuti wa CPM ifikapo mwaka kama vile 2025 au 2030? Huenda tungeishi kwa mioyo yenye hekima zaidi, iliyojaa hisia ya uharaka, tukitoa mhanga wowote unaohitajika ili kutimiza lengo la utume.
Hebu tuishi kwa hisia ya uharaka na tustahimili kwa ustahimilivu hadi mwisho utakapokaribia.
Maelezo
- Jina bandia la mwanafunzi wa Kristo kutoka Asia ya Kusini-Mashariki Rudi kwenye maandishi
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 39:1 (Jan./Feb. 2017), uk. 40-43. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


