NIMEWASIKIA WATU WAKISEMA KWAMBA wamepata mafunzo ya Harakati ya Kufanya Wanafunzi (DMM) na kuyatekeleza, lakini hawaoni matokeo yaliyotarajiwa. Wengine hata husema kwamba hayafanyi kazi kwao mahali pao pa huduma.
Mwaka 2005, nilipopata mafunzo hayo mimi mwenyewe kwa mara ya kwanza, nilisema jambo lilelile: “Hili halitafanya kazi mahali nilipo.” Lakini, nilipoamua kuyatekeleza, niliona, na ninaendelea kuona, matokeo popote kanuni za DMM zinapotekelezwa.
Nimetumia muda na watu ambao kwao “haifanyi kazi.” Katika kila hali, hawatekelezi mfumo mzima. Wanachagua kanuni moja au mbili na kuzitekeleza. Wanaona kuongezeka kwa kiasi fulani kwa wafuasi wapya wa Kristo, lakini si kuzidisha na kasi ya harakati waliyoitarajia.
Kuna mambo mawili ambayo karibu kila mara watu huchagua kuyatekeleza: kanuni za Mtu wa Amani na Usomaji wa Biblia kwa Kugundua (UBK). Hata hivyo, mara nyingi hawazitekelezi kanuni hizi kikamilifu wala kwa makusudi.
Makala hii inahusu kutekeleza kanuni ya “Mtu wa Amani” kwa namna inayoongoza kwenye kuzidisha na harakati. Kanuni hii ni kipengele muhimu katika mchakato wa Harakati za Kufanya Wanafunzi. Lakini, ili kuiona ikizaa matokeo yake kamili, lazima itekelezwe kwa njia sahihi.
I. Dhana
Tunaipata dhana ya “Mtu wa Amani” katika maelekezo ambayo Yesu aliwapa wanafunzi wake alipowatuma katika Mathayo 10, Luka 9, na Luka 10. Kimsingi, Yesu aliwaambia wanafunzi wake kwamba wanapoingia katika jamii, kipaumbele chao kitakuwa kumtafuta na kumpata mtu wa amani. Wakimpata, yafaa wakae; wasipompata, yafaa waondoke (Luka 10: 5-11).
Mtu wa Amani ni muhimu sana katika mchakato wa Harakati za Kufanya Wanafunzi. Kila DMM ni kazi ya Mungu, si ya mwanadamu. Ikiwa Mungu bado hajawainua watu wa amani, hakutakuwa na harakati. Kumbuka, Yesu aliwatuma wanafunzi wake mbele yake katika maeneo ambayo yeye mwenyewe alikuwa karibu kwenda kisha akasema “… Mavuno kweli [ni] mengi, lakini watenda kazi [ni] wachache; kwa hiyo, mwombeni Bwana wa mavuno atume watenda kazi katika mavuno yake.” (NKJV: Luka 10: 1-2).
Kuwepo kwa Mtu wa Amani katika jamii ni uthibitisho kwamba Mungu anatenda kazi katika jamii hiyo. Si hilo tu, mtu huyo ndiye mlango wa kuingia katika jamii na katika mavuno ya Ufalme katika jamii hiyo. Kwa kawaida yeye pia ni mvunaji ambaye atahitaji kupewa ukocha na kulelewa ili atimize nafasi hiyo.
Kuna mifano kadhaa ya Watu wa Amani katika Agano Jipya, kama vile Akida (Luka 7:1–10), Mwanamke Msamaria (Yohana 4:1–30), Towashi Mwethiopia (Matendo ya Mitume 8:26–40), Kornelio (Matendo ya Mitume 10:9–11:1), Lidia (Matendo ya Mitume 16:13–15), na Mlinzi wa Gereza wa Filipi (Matendo ya Mitume 16:22–38).
II. Yeye ni nani?
Aly alikuwa akitembelea jamii moja akitafuta mtu wa amani. Alipokutana na Kone alimtambua kama mtu wa amani. Kone alikuwa mchangamfu sana, mkaribishaji na mkarimu. Baada ya ziara tatu, Aly alitambua kwamba Kone hakuwa mtu wa amani. Walikuwa na mazungumzo mazuri ambapo Aly alijaribu kuleta mada za kiroho, lakini Kone hakuwa na jambo lolote la kiroho alilotaka kujadili. Hamu yake ilikuwa urafiki na Aly tu.
Watu wengi hukutana na mtu wa aina hii na kufikiri wamempata mtu wa amani. Watatumia muda mwingi na watu hawa na hawataona chochote kikitokea kinachoongoza kwenye kufanya wanafunzi. Wanachanganyikiwa na kuhitimisha kwamba DMM haifanyi kazi.
Mtu wa amani anaweza kuwa na sifa njema, lakini si kila mara. Mara nyingi wao ni wakarimu, wasaidizi, au wachangamfu. Lakini sifa muhimu zaidi inayomwelezea mtu wa amani ni kwamba yeye ana mahangaiko au maswali binafsi ya kiroho. Bila kujali asili yao ya kidini, kwa kawaida wana kutoridhika fulani kiroho au maswali. Kutoridhika huku kunasababishwa na ukweli kwamba Mungu anatenda kazi katika maisha yao, na Baba anawaandaa kuipokea Injili na kuwa kichocheo cha kuivusha Injili kuingia katika jamii. Kuwepo kwao katika jamii kwa kawaida kunamaanisha kwamba Mungu anatenda kazi katika jamii hiyo.
Kwa muhtasari, mtu wa amani:
- Si Mkristo – Yesu aliwatuma wanafunzi wake katika mavuno miongoni mwa watu wasiookolewa.
- Ana maswali ya kiroho na ni mtafutaji.
- Anadhihirisha kwamba Mungu anatenda kazi kupitia yeye.
- Anaonyesha kwamba Mungu amemwandaa kuipokea Injili.
- Kuwepo kwao katika jamii kunamaanisha kwamba Yesu anaitembelea jamii hiyo; Mungu anatenda kazi huko.
III. Jinsi ya kumpata mtu wa amani
Wafanya-wanafunzi huwapata watu wa amani kupitia mchakato wa maombi mengi, kutoa huduma au wema fulani katika jamii, na kuishi maisha ya kiroho yenye neema (Kumbukumbu la Torati 6: 4-9). Makala hii ni fupi mno kulipanua jambo hili hapa.
IV. Baada ya kumpata mtu wa amani, nini kinafuata?
Jua kwamba Mungu anatenda kazi katika jamii hiyo na ujiunge naye. Kuna mavuno ya kuvunwa. Mtu wa amani ni mbegu… mavuno yako zaidi yake. Mtu wa amani ana mtandao wa kijamii wa familia, marafiki, na wafanyakazi wenzake. Na kila mmoja wa hao ana mtandao wake wa kijamii. Na mitandao hii ya kijamii inaingiliana. Mtu wa amani ndiye mlango wa kuingia katika mitandao hii yote ya kijamii.
Lazare alitumia miaka bila kuzaa matunda akijaribu kupanda makanisa miongoni mwa watu wa Malinke katika nchi moja ya Afrika Magharibi. Kisha akapata mafunzo ya DMM. Alianza kuwapata watu wa amani katika jamii tofauti. Lakini kila mara alipompata mmoja, katika msisimko wake, alimwongoza tu kwa Kristo kisha akaenda kutafuta watu wengine wa amani. Alikosa kabisa kiini cha kazi ya kimkakati ya Mungu. Alikuwa akiwapata watu wengi wa amani, lakini hakuwa akipanda kanisa lolote.
Jambo bora la kufanya mtu anapompata mtu wa amani ni:
- Jikite katika mtandao wao wa kijamii katika jamii.
- Usiharakishe kuwaongoza kwa Kristo wakiwa peke yao.
- Wafanye wawaalike watu wa mitandao yao ya kijamii.
- Fanyeni Usomaji wa Biblia kwa Kugundua pamoja na kikundi ambacho mtu wa amani anakikusanya.
V. Kikundi cha Usomaji wa Biblia kwa Kugundua
Usomaji wa Biblia kwa Kugundua ndicho chombo cha kutumia kusaidia kikundi kumgundua Kristo na hitaji lao la kumhitaji kwa ajili ya wokovu. Mchakato wa ufuasi huanza na UBK kama chombo cha jambo hilo. Huku ni kukifanya kikundi kuwa wanafunzi kuelekea kuongoka.
Kikundi cha Kugundua pia ni chombo cha kutumia kujenga vinasaba vya kuzaana ndani ya kikundi. Kufikia wakati kikundi kinapofanya uamuzi wa kumfuata Kristo, wamejifunza thamani ya kumtii Mungu, kushirikisha kila kitu walichojifunza, na kuzaa tena kile walichokipitia.
VI. Kanisa jipya linaanza na kuzaa tena
Kikundi cha Usomaji wa Biblia kwa Kugundua kinahama kutoka kuwa kikundi cha kugundua hadi kuwa kanisa jipya waamini hawa wapya wanapobatizwa na kuanza kufanya kazi kama kanisa. Kanisa jipya litahitaji ukocha na ulezi zaidi ili kuwa na viongozi wake wenyewe na kuanzisha mchakato uleule mahali pengine.
Mtu wa amani ni muhimu katika mchakato wa Harakati ya Kufanya Wanafunzi. Lakini, ili wao watimize nafasi yao waliyopewa na Mungu katika DMM, lazima kwa makusudi wapewe ukocha na kulelewa ili kutimiza nafasi hiyo kama ilivyoelezwa hapo juu.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 39:6 (Nov./Des. 2017), uk. 26-28. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


