Umeamua moyoni mwako kwamba unataka kuona Mungu akizaa Harakati ya Kupanda Makanisa (CPM) katika jamii yako au kundi lako la watu. Swali ni: “Nianzeje?” Tuseme tumeketi katika mgahawa wa kahawa na ninakupa kitambaa cha mezani cha karatasi, nikisema, “Chora kwa haraka njia ya kuelekea CPM.” Je, ungejua pa kuanzia? Lazima uingie katika njia ambayo huenda ikaongoza kwenye “harakati,” badala ya ile ambayo haitaongoza huko. Lazima uelewe njia hiyo inaonekanaje.
Changamoto ya njia ya CPM ni neno harakati. Mungu ndiye anayeanzisha Harakati za Kupanda Makanisa, si watumishi wake. Hata hivyo huwatumia watumishi wake kuwa mawakala wanaoanzisha CPM pale wanapozielewa njia zake na kuzitiisha kikamilifu juhudi zao za huduma chini ya njia hizo.
Kuweka Matanga ya Huduma Yako ili Kunasa Upepo wa Roho
Fikiria hivi. Nikiwa baharia, ninaweza kushughulikia mambo yote yaliyo ndani ya uwezo wangu: kuhakikisha matanga yangu yamepandishwa, usukani uko katika mkao sahihi, matanga yamerekebishwa ipasavyo. Lakini hadi upepo uvume, mashua yangu ya tanga imesimama tu majini. Upepo ndio kitu kilicho nje ya uwezo wangu. Au ikiwa upepo unavuma, lakini mimi kama baharia nikashindwa kupandisha matanga au kuyarekebisha ili kunasa upepo, siendi popote. Katika hali hii, upepo unavuma lakini sijui jinsi ya kwenda pamoja na upepo.
Yesu alitoa tamko hili: “Upepo huvuma upendako, nawe unasikia sauti yake, lakini hujui unakotoka wala unakokwenda. Ndivyo ilivyo kwa kila mtu aliyezaliwa kwa Roho.” (Yohana 3:8 ESV).
Roho huvuma kwa njia ambazo hatuwezi kuzitabiri, lakini hakika huvuma. Swali ni: “Je, huduma yangu imewekwa katika mkao wa kwenda jinsi anavyovuma ili iweze kuwa harakati ya Mungu?” Ikiwa huduma zetu hazishirikiani na njia za Roho, tunajaribiwa kusema: “Mungu hatendi tena leo kama alivyotenda siku za zamani!” Hakika ushuhuda wa CPM nyingi kwa makumi ulimwenguni kote na katika kila bara ni kwamba “Yesu Kristo ni yeye yule jana na leo na hata milele.” (Waebrania 13:8 ESV).
Moyo na Mashamba Manne: Mambo Muhimu ya CPM kwenye Kitambaa cha Mezani
Ni vipengele gani muhimu (mambo yaliyo ndani ya uwezo wetu) vinavyotuwezesha kuweka matanga yetu katika mkao wa kwenda pamoja na Roho wa Mungu? Ingawa yameelezwa kwa njia nyingi na watendaji wa CPM, kinachofuata ni muhtasari rahisi wa mpango wa msingi wa CPM. Mara nyingi mimi huchora mchoro huu rahisi kwenye kitambaa cha mezani katika mgahawa wa kahawa kwa ajili ya rafiki. Mimi huutumia kumweleza jinsi tunavyoweza kushirikiana na Mungu kwa ajili ya harakati. Ikiwa huwezi kuchora mpango wa msingi wa CPM kwenye kitambaa cha mezani, yaelekea ni tata mno kuuishi wewe binafsi na tata mno kwa wengine kuuzaa tena.
MOYO
Pata MOYO wa Mungu kwa ajili ya watu wako na umtafute kwa imani ili maono yake yatimie. MAONO yapo ndani yako na timu yako ya kufanya lolote linalohitajika chini ya Mungu ili kuona kwamba watu wote wanapata nafasi ya kuuitikia Ufalme. Unayatafuta maono ya Mungu, si yako mwenyewe (Mathayo 6:9-10; 28:18-20). Maono ya ukubwa huu yanapaswa kuleta umati wa waamini na maelfu ya makanisa.
Kwa kuwa maono haya ni makubwa sana, lazima uyagawe katika SEHEMU za msingi za kimahusiano ili ujue jinsi ya kuanza. Lengo lako ni rahisi: panda vikundi vya mbegu ya haradali vinavyozaa tena (Mathayo 13:31-33) vyenye uwezo wa kuifikia sehemu hiyo na zaidi.
Unajua kwamba harakati imeota mizizi katika kila sehemu pale unapoweza kufuatilia angalau vizazi vinne vya waamini na makanisa—G4—mahali hapo (2 Timotheo 2:2). CPM zinafafanuliwa kwa makanisa ya angalau kizazi cha 4 yanayojitokeza kwa uthabiti ndani ya kipindi kifupi kiasi (miezi na miaka, si miongo).
Ili kutimiza maono, lazima uanzie kwenye msingi kwa KUKAA NDANI YA KRISTO (Yohana 15:5). Wale wanaozaa matunda ni wale wanaokaa ndani yake. Hupati CPM kwa kukaa ndani ya Kristo, lakini hupati CPM usipokaa ndani yake. Tunapojinyenyekeza, lazima tumlilie Mungu kwa bidii katika MAOMBI ili kuona maono yake yakitimia (Luka 10:2). Kila Harakati ya Kupanda Makanisa huanza kwanza kama harakati ya maombi.
MASHAMBA MANNE
Ili kutimiza maono, unafanya sehemu yako katika ushirikiano kati ya Mungu na mwanadamu—shughuli tano zenye thamani kubwa. Kila moja lazima ifanywe kwa namna inayoweza kuzalishwa tena na waamini wapya.
JUKWAA LA KATIKATI: VIONGOZI WANAOZAA TENA
(Tito 1:5-9; Matendo ya Mitume 14:23). Baadhi ya waamini watajithibitisha kuwa VIONGOZI wanaozaa tena wanaofaa kwa hatua hiyo ya kazi. CPM ni harakati za kuzidisha uongozi kama vile zilivyo Harakati za Kupanda Makanisa.
MISHALE NA KIFO
Waamini wengi wataendelea KURUDIA sehemu mbalimbali za mashamba manne. Kichocheo cha kiroho ni KIFO (Yohana 12:24)—utayari wa waamini kustahimili kwa ujasiri, hata kufa, ili kuona maono ya Mungu yakitimia. Hadi waamini watakapokuwa tayari kuhesabu gharama kwa furaha, haya yote yanabaki kuwa nadharia tu.
Je, unaweza kuuzaa tena mchoro huu kwenye kitambaa cha mezani pamoja na rafiki?
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 35:4 (Jul./Ago. 2013). Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


