Tumejifunza kanuni zetu za huduma kwa sehemu kubwa kupitia majaribio ya uwandani. Tulipopata matunda kidogo (watu binafsi waliomjia Kristo, vikundi vya waamini au viashiria vingine vya ukuaji wa kiroho), tulijaribu kuchunguza: Kwa nini hivyo? Ni nini kilichotusaidia kupiga hatua? Tunawezaje kuongeza yale mazoea yaliyozaa matunda zaidi? Tunawezaje kupunguza yale mazoea ambayo hayakuwa yakionyesha kuzaa matunda?
Kwa ufupi, tunaunda mazingira ya majaribio, na kufanya tathmini kila robo mwaka ili kukuza kwa bidii mazoea yenye matunda na kuzima mazoea yasiyo na matunda. Bila shaka, hatuzimi mazoea ya kibiblia, iwe yanachangia moja kwa moja kuzaa matunda au la, kama vile kuwasaidia maskini. Tunafanya hilo pia, ingawa huenda likazaa au lisizae vikundi zaidi vya waamini, kwa sababu ya amri za Mungu za kuwasaidia maskini. Huo ni mjadala tofauti; ninazungumzia tu yale mazoea ambayo tunaweza kuyarekebisha bila kuvunja au kupuuza kanuni za kibiblia.
Vinasaba vyetu vya majaribio vimewavutia sana watu wanaotaka kujifunza kutoka kwetu. Wanapokuja, hawawezi kuamini, kwa sababu vichocheo vya harakati wa mahali hapo wanatueleza, kila robo mwaka: a) majaribio mapya wanayoyafanya, b) wamepiga hatua kiasi gani katika miezi mitatu waliyokuwa wakifanya jaribio, na c) watarekebisha nini wanaposonga mbele katika miezi mitatu ijayo ya jaribio. Ubunifu wetu unasonga mbele kwa hatua ndogo kila robo mwaka. Unaweza kufikiria watu wabunifu tuliowavutia na jinsi ubunifu wao ulivyokua. Ni jambo ambalo nimelifurahia sana: kubuni na kuwapata watenda kazi wabunifu wa mahali hapo.
Si kwamba watu wote wenye matunda ninaowasimamia ni wabunifu. Lakini ninafanya kazi hasa na wale 40% hadi 50% kati yao ambao ni wabunifu, kwa sababu wao ndio wanaogundua njia mpya. Asili ya huduma miongoni mwa UPG ni kwamba hakujakuwa na mafanikio kwa miongo kadhaa. Tukiendelea kufanya mambo ambayo Wakristo wengine walikuwa wakiyafanya, tunaweza kuwa na uhakika kabisa kwamba bado hatutapata mafanikio katika miongo ijayo. Ndiyo sababu ubunifu ni muhimu katika kuwafikia UPG, hasa katika maeneo ambapo hakujakuwa na ongezeko kubwa la matunda hapo awali.
Huu hapa ni mfano mmoja wa kujifunza kwa majaribio kupitia uchunguzi linganishi wa kifani. Ningewaajiri wainjilisti wazuri wa mahali hapo, kisha kuwatazama wakifanya kazi na kulinganisha hadithi zao. Kulinganisha mazoea tofauti ya watu tofauti na kulinganisha matunda yao, ni sehemu ya kujifunza kwangu na kwao.
Kiongozi wetu wa kwanza wa timu alianzisha vikundi vitatu. Alionekana kutoa mfano kwa wainjilisti wengine kuufuata. Lakini hakuwahi kuvuka vikundi vitatu. Wakati huo huo, wale wengine walikuwa kama kobe katika mbio dhidi ya sungura. Walikuwa nyuma sana lakini waliendelea kufanya kazi na hatimaye wakaanzisha kikundi kimoja. Kiongozi alikuwa tayari na vikundi vitatu, kisha wale walioanza polepole zaidi wakakuza vikundi viwili kila mmoja, kisha vikundi vitatu kila mmoja. Ghafla wapandaji walioanza polepole zaidi waliripoti vikundi vinne na vitano, kwa sababu baadhi ya vikundi vyao vilikuwa vimeanzisha vingine. Lakini kiongozi alikuwa bado anaongoza vikundi vitatu yeye mwenyewe. Kisha vikundi vile vitatu vikapungua hadi vikundi viwili. Kulikuwa kunatokea nini?
Ulinganisho huu wa matunda ya wapandaji tofauti uliibua swali. “Wote ni wahitimu wa Chuo kimoja cha Biblia na walipata ukocha ule ule, na wote walikuwa wakifanya kazi katika eneo moja ambapo 99.6% ya watu ni wa dini ya walio wengi. Ni nini kinachotokea kwa njia tofauti?” Wale waliokuwa wakifikia vikundi vingi zaidi hawakuwa wazi kushirikisha mambo katika mikutano kwa kuogopa kumwaibisha kiongozi aliyekuwa akizidi kuchanganyikiwa. Hawakuwa wakitoa uchambuzi wa wazi. Nilipochunguza zaidi, niligundua kwamba kiongozi aliogopa kwamba kama angezungumza na vikundi badala ya watu mmoja mmoja, angeongeza hatari kwake na kwa familia yake. Kwa hiyo, alikuwa akizungumza na watu mmoja mmoja tu. Njia hiyo ilikuwa ikileta kiasi fulani cha matunda, lakini haikuwa ikizalishwa tena na watu wa mahali hapo. Wakati huo huo, wale wapandaji wengine walioanza polepole zaidi, wote walikuwa wakizungumza na makundi ya asili ya watu na mara chache tu na watu mmoja mmoja.
Katika nchi yetu, karibu kamwe humkuti mtu akiwa peke yake. Kuna msongamano mkubwa, kila mtu yuko pamoja na wengine kila wakati. Hata ukienda dukani, au ukienda kukimbia, popote uendapo unaona watu wakiwa katika makundi. Wako pamoja na kaka yao na mjomba wao na rafiki yao: labda watu wanne au watano au sita. Simaanishi vikundi rasmi, bali makundi ya kawaida ya watu. Kwa hiyo wale wainjilisti walioanza polepole zaidi walianza kuzungumza na makundi ya watu wa mahali hapo. Walirekebisha mtindo wao wa mazungumzo ili utoshee katika makundi. Mwanzoni, kushirikisha Injili katika makundi kulienda polepole zaidi kuliko kushirikisha watu mmoja mmoja. Lakini watu katika makundi walipoanza kuzungumza kuhusu Injili wao kwa wao, na kuanza kumwamini Yesu huku wakisaidiana, yale makundi ya kwanza ya waamini wa mahali hapo hayakuwa tasa. Yalizaana kwa kuiga mfumo huo. Watu binafsi waliovutwa kwa Bwana wakiwa peke yao walikuwa tasa. Hawakuweza kuzaa watoto; hawakuweza kunakili mchakato ule ule, kwa sababu katika nchi yetu, hakuna anayezungumza na mtu mmoja akiwa peke yake. Kama mtu angezungumza na mtu mwingine ana kwa ana faraghani, ilionekana kuashiria kwamba kuna jambo lisilo halali kuhusu mada inayojadiliwa. Kama kitu fulani kilihitaji kufichwa, yaelekea kilikuwa cha aibu. “Kwa nini unahitaji kuzungumza na mtu mmoja akiwa peke yake? Je, una kitu cha kuficha?” Lakini unapozungumza katika makundi ya watu ambao tayari wanafahamiana, ni ishara kwamba hili ni jambo zuri kuzungumza nalo na wengine.
Watu waliomjia Bwana katika makundi ya asili, wana uzoefu kama wa watu katika kikundi cha Alcoholics Anonymous: wanatoa na kupokea msaada huku wakishirikisha kile wanachojifunza. Hawa ni watu katika Makundi ya Watu Wasiofikiwa ambao wanafanya jambo tofauti na watu wengine wote. Wanahitajiana kwa ajili ya kusaidiana ili kumtafuta Bwana pamoja kupitia Biblia. Wanahalalishana: “Ni sawa kufungua Biblia na kuijadili.” Wanalindana dhidi ya kushambuliwa na majirani na marafiki. Wanaweza kumjia Bwana pamoja na hili ni jambo wanaloweza kulirudia, kwa sababu mpangilio na mienendo ya kijamii inaunga mkono mwingiliano unaoendelea. Ni kama mchezo wa pingpong unaofurahiwa na kikundi cha marafiki: mpira unapigwa huku na huko huku wakicheka pamoja. Wanazungumza huku na huko kuhusu Maandiko na jinsi ya kuyatumia, na mwingiliano huo ni sehemu ya furaha. Ni watu wanaopenda furaha; wanapenda kufanya hivyo pamoja. Kwa hiyo sasa wanatumia mienendo ya kijamii ambayo tayari ipo katika utamaduni, na vikundi vinaanza kuzaana.
Nilishiriki hadithi iliyotangulia kama mfano wa jinsi tulivyojifunza mojawapo ya kanuni zetu kuu. Tuna mazoea yenye matunda 15 au 20. Zoea lenye matunda tulilojifunza kutokana na kisa hiki lilikuwa “Vikundi, si Watu Mmoja Mmoja.” Walitengeneza kauli mbiu kutokana na kila moja ya mazoea yenye matunda, na hii ni mojawapo: “Vikundi, si Watu Mmoja Mmoja.” Zoea hili lenye matunda ni mojawapo ya kanuni zetu zinazotuongoza. Tuliligundua kupitia majaribio, kwa kulinganisha kile kilichokuwa kikifanya kazi na kile ambacho hakikuwa kikifanya kazi vizuri hivyo.
Tulipokuwa tumeendelea kwa miaka 10 na kuwa na vikundi 110, nilishiriki katika kongamano ambapo niliombwa kushirikisha uchunguzi wetu wa kifani. Nilikuwa ndani ya ndege nikifikiri “Hawataamini nitakapowaambia kwamba kuna vikundi 110 vya watu kutoka dini ya walio wengi, ambao wamemjia Kristo na wanaijadili Biblia na kuitumia. Watadhani ninadanganya!” Lakini masomo mengine yote ya kifani yaliyowasilishwa yalitoka Afrika na India, na yote yalikuwa na matunda mengi zaidi sana kuliko hayo!
Lilikuwa mshtuko mzuri sana kwangu, kutambua kwamba kile kilichokuwa kikikua katika nchi yetu kilikuwa tone dogo tu ndani ya ndoo, ukilinganisha na kile ambacho wengine walikuwa nacho. Kilikuwa kitia-moyo kikubwa kwa imani yangu kutafakari: “Hakuna mipaka kwa mfumo unaoweza kupanuka. Hili linaweza kuendelea.” Na wakati wa kongamano hilo, nilipokea mafunzo ya CPM kwa mara ya kwanza, yaliyotolewa na David Watson: mfumo wa DMM.
Washiriki wengi wa kongamano hawakuyapenda mafunzo ya CPM kwa sababu yalitikisa jinsi walivyokuwa wakifanya mambo katika miaka mingi ya huduma. Walitoa pingamizi ambazo hazikuhitaji kutolewa. Niliendelea kufikiri: “Ninapaswa kusimama na kuwaambia: ‘Kwa nini msitoke chumbani na kuniacha nimsikilize mzungumzaji huyu?’ Haya ndiyo tumekuwa tukijifunza katika nchi yetu. Kanuni hizi ni mambo yale yale ambayo Mungu amekuwa akitufundisha. Yeye aligunduaje hili, katika nchi tofauti?” Huo ndio ulikuwa uzoefu wangu katika kongamano hilo. Walio wengi kati yetu hatutaki kuacha kufanya kile tumekuwa tukikifanya na kujaribu mfumo mpya. Hata hivyo, kile tulichojifunza kupitia majaribio uwandani kwa miaka mingi, wengine pia walikuwa wamekigundua, katika miktadha mingine miongoni mwa aina nyingine za makundi ya watu wasiofikiwa.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 44:2 (Mac./Apr. 2022), uk. 18-20. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


