MUDA MFUPI KABLA YESU HAJAPAA kwenda mbinguni, aliwapa wanafunzi wake kazi tunayoiita Agizo Kuu: “kwenda ulimwenguni kote,” wakifanya wanafunzi wa kila kundi la watu. Tangu wakati huo, Wakristo wameota siku ambayo kazi hii itakamilika. Wengi wetu tunaihusisha na Mathayo 24:14, ahadi ya Yesu kwamba Injili “itahubiriwa katika ulimwengu wote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote, na ndipo mwisho utakapokuja.” (NIV) Ingawa tunaweza kujadiliana kuhusu maana halisi za kifungu hiki, tuna mwelekeo wa kufikiri kwamba kazi hiyo “itakamilika,” na kwamba kukamilika huko kwa namna fulani kunahusiana na “mwisho.”
Ingawa tunasubiri kwa hamu kurudi kwa Kristo, lazima tukabiliane na ukweli: ikiwa mwisho wa kazi na kurudi kwa Yesu kwa namna fulani vinahusiana, yaelekea kurudi kwake bado kuko mbali. Kwa vipimo vingi, “mwisho wa kazi” unazidi kwenda mbali nasi!
Tunapimaje hasa “mwisho wa kazi?" Njia mbili zinazowezekana zinahusiana na maandiko haya: kipimo cha kutangaza Injili na kipimo cha ufuasi.
Kama kipimo cha ufuasi, tunaweza kufikiria ni sehemu kiasi gani ya ulimwengu inayodai kuwa ya Kikristo, na ni sehemu kiasi gani ya ulimwengu inayoweza kuhesabiwa kuwa “wanafunzi hai.”
Center for the Study of Global Christianity (CSGC) huhesabu Wakristo wa aina zote. Wanatuambia kwamba mwaka 1900, 33% ya ulimwengu ilikuwa ya Kikristo; mwaka 2000, 33% ya ulimwengu ilikuwa ya Kikristo. Na kufikia 2050, mambo yasipobadilika kwa kiasi kikubwa, ulimwengu bado utakuwa 33% wa Kikristo! Kanisa linalokua tu kwa kiwango sawa na idadi ya watu halipeleki Injili kwa ulimwengu wote kuwa ushuhuda kwa makundi yote ya watu.
Vipi kuhusu “wanafunzi hai?” Kipimo hiki ni kigumu zaidi sana, kwa kuwa hatuwezi kweli kujua “hali ya moyo.” Lakini katika The Future of the Global Church, Patrick Johnstone alikadiria “Wakristo wa kiinjili” (evangelicals) kuwa takriban 6.9% ya idadi ya watu ulimwenguni mwaka 2010. IMB inakadiria Wakristo wa kiinjili kuwa 3% leo. Kwa makadirio yoyote, idadi ya Wakristo wa kiinjili inakua kwa kasi zaidi kuliko sehemu nyingine zilizo nyingi za Ukristo, lakini inaendelea kuwa asilimia ndogo ya ulimwengu.
Hata hivyo, idadi ya waamini si kipimo pekee cha kukamilisha kazi. “Kutangaza Injili,” kama ilivyoelezwa hapo juu, ni kipimo kingine. Baadhi ya watu wataisikia Injili na wasiipokee. Vipimo vitatu vya kutangaza Injili vinatumika sana: wasiohubiriwa Injili, wasiofikiwa na ambao hakuna kazi iliyoanzishwa miongoni mwao. (Mission Frontiers liliangalia vipimo hivi vitatu kwa kina katika toleo la Januari-Februari 2007).
Wasiohubiriwa Injili ni jaribio la kupima ni nani wasio na fursa ya kuifikia Injili: ni nani ambao, kwa uhalisia, hawatapata nafasi ya kuisikia Habari Njema na kuiitikia katika maisha yao. CSGC inakadiria kwamba 54% ya ulimwengu hawakuwa wamehubiriwa Injili mwaka 1900 na 28% hawajahubiriwa Injili leo. Hii ni habari njema: asilimia ya ulimwengu wasio na fursa ya kuifikia Injili imeshuka kwa kiasi kikubwa. Hata hivyo, habari mbaya: mwaka 1900, jumla ya watu wasiohubiriwa Injili ilikuwa milioni 880. Leo, kwa sababu ya ongezeko la idadi ya watu, idadi hiyo imepanda hadi bilioni 2.1.
Ingawa asilimia ya watu wasiohubiriwa Injili ilipunguzwa karibu nusu, jumla ya idadi ya watu wasio na fursa imeongezeka zaidi ya maradufu. Kazi iliyobaki imekua kwa ukubwa.
Wasiofikiwa ni tofauti kidogo: kinapima ni makundi gani yasiyohubiriwa Injili ambayo hayana kanisa la wenyeji, la asili, linaloweza kupeleka Injili kwa kundi zima bila msaada wa wamisionari wa tamaduni tofauti. Joshua Project inaorodhesha takriban makundi 7,000 yasiyofikiwa yenye jumla ya watu bilioni 3.15, ambayo ni 42% ya ulimwengu.
Hatimaye, makundi ambayo hakuna kazi iliyoanzishwa miongoni mwao ni yale ambayo hayana kazi yoyote iliyoanzishwa na timu ya upandaji makanisa. Leo, kuna makundi 1,510 kama hayo: idadi hiyo imekuwa ikipungua tangu ilipoanzishwa mwaka 1999 na IMB. Kupungua huku ni ishara nzuri, lakini kunamaanisha kwamba kwa makundi “ambayo kazi imeanzishwa hivi karibuni,” kazi haijakamilika, imeanza tu hivi karibuni! Ni rahisi zaidi sana kuanzisha kazi miongoni mwa kundi kwa timu ya upandaji makanisa kuliko kuona matokeo yanayodumu.
“Ukweli mchungu” ni kwamba, kwa kipimo chochote kati ya hivi, hakuna juhudi zetu zilizopo zitakazowafikia watu wote katika makundi yote hivi karibuni. Tunaona sababu kadhaa muhimu za hili.
Licha ya shauku yetu ya dhati ya kutimiza Agizo Kuu, tusipobadilisha jinsi tunavyo“kimbia mbio,” yaelekea hatutauona mstari wa kumalizia hivi karibuni. Kwa kusonga hatua ndogo ndogo, kamwe hatuwezi kuziba pengo la watu waliopotea. Tunahitaji kukabiliana na ukweli mchungu kwamba umisheni na upandaji makanisa kwa namna ya kawaida havitafikia lengo.
Tunahitaji harakati ambapo idadi ya waamini wapya inazidi kiwango cha ukuaji wa kila mwaka wa idadi ya watu. Tunahitaji makanisa yanayozaa makanisa na harakati zinazozaa harakati miongoni mwa wasiofikiwa. Hii si ndoto wala nadharia tu. Mungu anafanya hivi katika baadhi ya maeneo. Kuna zaidi ya Harakati 600 za Kupanda Makanisa (CPM) (angalau mikondo minne tofauti ya makanisa ya vizazi 4+ kwa uthabiti) zilizoenea katika kila bara. Kuna harakati nyingine 250+ zinazoibuka zinazoona kuzidishwa kwa makanisa kwa kizazi cha 2 na cha 3.

Lazima tuzingatie kile Mungu anachofanya na kubadilisha mikakati yenye matunda kidogo kwa mikakati yenye matunda mengi.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 40:1 (Jan./Feb. 2018), uk. 14-16. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


