Yesu anatuambia katika Mathayo 24 kwamba kabla hajarudi, majanga mengi yatakuja, yakiwemo kila aina ya maafa ya asili na ya kibinadamu. Waamini watatolewa kwa mateso, watachukiwa na ethnē zote kwa sababu ya Yesu na hata kuuawa. Wengi watageuka na kuiacha imani katika Yesu na kusalitiana na kuchukiana. Kwa sababu ya kuongezeka huku kwa uovu, upendo wa waamini walio wengi utapoa. Si picha nzuri, sivyo?
Kisha anasema na (Mathayo 24:14a) katikati ya vurugu hizo zote (badala ya kusema lakini au licha ya), mambo mawili yanayohusiana yatatokea. 1) Wale watakaosimama imara hadi mwisho wataokolewa, na 2) habari hii njema ya ufalme itashirikishwa hadharani katika ulimwengu wote kama ushuhuda wa kujitoa mhanga kwa ethnē zote – na ndipo mwisho utakapokuja! Kwa maneno mengine, makundi yote ya watu yatapewa “chaguo la Yesu” kabla mwisho haujaja. Na hilo litatokea katikati ya machafuko yote, si licha ya machafuko hayo.
Mawimbi ya mateso yametokea katika historia yote na si jambo jipya. Kumekuwa na miitikio mikuu miwili: 1) waamini hukasirika na kushangaa mateso yanapotokea na kushauriana kujificha ili huenda wasilengwe; na 2) baadhi ya waamini huwa na ujasiri wenye hekima, lakini wenye msukumo safi. Kundi hili la pili limefanya wanafunzi wengi katika vipindi hivi, mara nyingi kwa gharama kubwa.
Katikati ya miaka ya 1980, karibu nusu ya wamisionari kutoka mashirika yote nchini Indonesia walilazimishwa kuondoka nchini. Wengi waliobaki au waliokuwa wamewasili tu walitambua uharaka mpya na kuchukua hatua mpya za ujasiri ili kufanya wanafunzi licha ya hatari zozote walizokabiliana nazo. Leo, katika nchi kadhaa kubwa, watenda kazi wako chini ya uangalizi mkali wa serikali au wanafukuzwa. Mwitikio wetu utakuwa upi? Je, tutasalimu amri kwa dhana potofu za kimisiolojia au tutafuata mifumo ya kibiblia? Ona unavyofikiri kuhusu yafuatayo.
Mfumo wa Kibiblia—Tutateseka tukiwa katikati ya mapenzi ya Mungu. Yesu aliishi kikamilifu katikati ya mapenzi ya Mungu – na aliuawa. Kwa kweli, alijua kwamba angeuawa na aliyahatarisha maisha yake kwa hiari.
Katika 2 Wakorintho 1:8-11, Paulo anaelezea jinsi yeye na timu yake walivyopitia shinikizo kupita kile walichohisi wangeweza kustahimili. Walikata tamaa hadi kufikia hatua ya kuhisi kana kwamba hukumu yao ya kifo ilikuwa imeshatolewa. Hata hivyo katika hali hiyo mbaya mno walijifunza kumtegemea Mungu na wakaendelea kuwagusa watu.
Katika 2 Wakorintho 11:23-28, Paulo anaorodhesha mateso yake mengi: kupigwa mijeledi mara nyingi, kuvunjikiwa na merikebu, kupigwa mawe, vifungo, wanyang’anyi, njaa, kiu, uchi, hatari katika maeneo mengi na kutoka kwa aina nyingi za watu. Tuwe wakweli. Kumtangaza Yesu miongoni mwa wasiofikiwa kunaweza kusababisha maumivu halisi, huzuni, kukata tamaa, dhuluma, misiba, n.k. Tuwe wakweli zaidi. Yote yatastahili tutakapoona wanafunzi wanaozaana wenye maisha yaliyobadilishwa katika Kristo.
Mfumo wa Kibiblia—Tunapaswa kuwa mashahidi wenye ujasiri hata tunapotazamwa na mamlaka. Watu tayari wanajua sisi ni akina nani na wanatutazama. Kwa hiyo ni afadhali tuwe wazi kwa hekima. Tunataka kuwa na hekima (na tusiteswe kwa kutenda kipumbavu), lakini lazima tusiziruhusu nguvu za ulimwengu huu kutusukuma kuchukua sura ya kidunia. Hakuna mtu mwenye tahadhari kupita kiasi aliyewahi kujulikana kuchochea harakati ya kufanya wanafunzi.
Yesu alisema: “Watakapowapeleka [si wakiwapeleka] mbele ya … wenye mamlaka, msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au mtakalosema, kwa maana Roho Mtakatifu atawafundisha saa ile ile yawapasayo kusema.” (Luka 12:11-12, NIV)
Anatuita tuendelee kushirikisha, hata chini ya tishio la kifo. Anatualika pia kufurahi tunapopata aibu kwa ajili ya Yesu. ‘Furahini na kushangilia, kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni.’ (Mathayo 5:12a, NIV) Mitume walionyesha kwa mfano ujasiri huu na furaha hii.
Mitume waliletwa na kusimamishwa mbele ya Baraza (Sanhedrin) ili kuhojiwa na kuhani mkuu. “Tuliwapa amri kali msifundishe kwa jina hili,” alisema. “Hata hivyo mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu na mmeazimia kutufanya tuwe na hatia ya damu ya mtu huyu.” Petro na mitume wengine walijibu: “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu!” (Matendo ya Mitume 5:27-29, NIV)
Wenye mamlaka walikasirika sana na kuamua kuwaua. Gamalieli aliwashawishi wasiwaue, kwa hiyo waliwapiga mijeledi tu (!) na tena wakawaamuru wasizungumze kuhusu Yesu.
Je, waliacha? Hata kidogo. Hawakuacha kamwe kufundisha. Walifundisha siku kwa siku. Walifanya hivyo hadharani katika viwanja vya hekalu na nyumba kwa nyumba. Na walifurahi kwamba walihesabiwa kuwa wanastahili kupata aibu kwa ajili ya lile Jina! (Matendo ya Mitume 5: 40-42)
Mfumo wa Kibiblia—Lazima tuonyeshe kwa mfano utayari wa kuteseka kwa ajili ya Yesu. Tunahisi wasiwasi, na ni haki, pale vikundi tunavyosaidia kuanzisha visipozaana. Sababu ambayo mara nyingi hutolewa ni kwamba kila mtu katika utamaduni huo huwashuku wengine na hivyo husita kufanya wanafunzi. Je, inaweza pia kuwa kwamba sisi hatujaonyesha kwa mfano utayari wa kuhatarisha kukamatwa na kuteseka kwa ajili ya Injili?
Tuwe tayari na wenye ujasiri wa kuhatarisha kwa unyenyekevu wa kweli. Mtume Paulo alitupa mfano na changamoto katika hili, “Igeni mfano wangu, kama mimi ninavyoiga mfano wa Kristo.” (1 Wakorintho 11:1). Mfano wa Yesu hatimaye ulimwongoza kwenye dhabihu yake kuu – na mwitikio mkubwa sana uliofuata.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 41:5 (Sep./Okt. 2019), uk. 42-43. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


