Watafiti walipochunguza kazi ya ajabu ya Mungu katika Harakati za Kupanda Makanisa (CPM) 1,9651 (wakati wa kuandika haya), zinazoleta zaidi ya watu milioni 114 katika Ufalme wa Mungu katika kizazi hiki,2 wamegundua jambo la kushangaza. Si tu kwamba harakati ndizo njia ambayo Ufalme wa Mungu unakua kwa kasi zaidi katika siku zetu, bali pia ndizo chanzo ambacho harakati nyingi mpya zinachipukia.
Ni asilimia 10 hadi 20 tu ya harakati zilizopo zilianzishwa na kichocheo (au vichocheo) cha nje kilichompata kichocheo (au vichocheo) cha ndani na kupanda makanisa ya kwanza. Sehemu kubwa mno ya harakati za sasa—kati ya asilimia 80 na 90 yake3—zilianzishwa na waamini kutoka harakati nyingine (za utamaduni unaokaribiana). Mfano wa “makaa ya moto” umetumika mara nyingi kuonyesha kuchukua makaa kutoka moto uliopo ili kuwasha moto mahali papya (badala ya kujaribu kuwasha moto kutoka bila kitu). Kwa mfano, harakati ya Wabhojpuri huko India Kaskazini4 imeanzisha harakati katika angalau makundi mengine manane makubwa ya lugha. Familia nyingine ya harakati katika Asia ya Kusini-Mashariki imeanzisha kazi katika UPG zaidi ya 50 na nchi 17.
Uhalisia huu wa kushangaza una athari kubwa kwa kila mtu mwenye shauku ya kuona Injili ikiyafikia mataifa yote haraka iwezekanavyo. Wale wanaotafuta kuchochea harakati mara nyingi wamelenga kutozingatia “Ninaweza kufanya nini?” bali “Ni nini kinachohitaji kufanywa?” Kauli mbiu hii inadai matumizi mapya tunapozitafakari habari zilizogunduliwa hivi karibuni kuhusu jinsi harakati nyingi zinavyoanza sasa. Ni nini “kinachohitaji kufanywa” ambacho kinaweza kutimizwa na watenda kazi wa utamaduni wa mbali?
Kwa kweli, mambo mengi sana yanahitaji kufanywa, lakini yanatofautiana kutoka harakati moja hadi nyingine, na wakati mwingine kutoka mwaka mmoja hadi mwingine ndani ya harakati yoyote ile. Watenda kazi wa utamaduni wa mbali wanaweza kuwa na nafasi muhimu sana katika kuimarisha na kuiongezea kina harakati, na/au katika kusaidia harakati kupanuka na kuchochea harakati mpya miongoni mwa UPG nyingine.
Ufunguo uko katika utayari wa kuhudumia mahitaji halisi yanayohisiwa na kuelezwa na viongozi wa harakati. Hawahitaji watu wa nje wanaojitokeza wakiwa na mipango na mawazo yao wenyewe. Wanataka watu wanyenyekevu vya kutosha na wanaonyumbulika vya kutosha kufanya chochote kinachohitaji kufanywa.
Katika baadhi ya hali, hili huenda likahusisha ujuzi maalum, lakini mara nyingi zaidi linahusisha kutumia ujuzi wa kiwango cha msingi katika eneo lenye uhitaji.
Uwezekano unajumuisha:
- Maombi na kuhamasisha maombi kutoka nje ya harakati
- Juhudi za mawasiliano
- Mafunzo ya ajira na ya kuanzisha biashara
- Msaada wa kompyuta na wa kiufundi
- Kurekodi na/au kuhariri video na/au sauti
- Kuchangisha fedha kwa njia zisizoleta utegemezi
- Msaada wa mitandao ya kijamii katika kutengeneza na/au kusambaza maudhui
- Kuandaa safari za maono kwa washirika watarajiwa kutoka nje
- Msaada wa kiutawala
- Kuwapokea na kuwasimamia wanafunzi wa mafunzo kazini kutoka nje
- Huduma na/au mafunzo na/au mitandao ya mawasiliano ya kuitikia maafa
- Huduma ya matibabu na kuandaa uwezo wa kuitikia kimatibabu ndani ya harakati
- Kusaidia katika utegemezaji, kujenga mitandao, au chochote kingine kinachoweza kuhitajika ili kusaidia kuipeleka Injili mahali ambapo haijawahi kufika
- Kusaidia katika tafsiri na usambazaji wa Biblia
- Kitu chochote na kila kitu kinachohitajika
Katika hali nyingi, harakati haziwezi kutoa maelezo mahususi ya kazi, kwa kuwa mahitaji yao yanaendelea kubadilika. Au huenda zikaanza na hitaji mahususi na maelezo ya kazi, lakini mazingira hubadilisha mahitaji. Wanataka watu walio tayari kufanya chochote kinachohitajika. Wanathamini uhusiano kwanza na kazi baadaye. Kwa maneno mengine, wanataka kuwa marafiki na watenda kazi pamoja na kaka na dada wanaoweza kuwaamini, na nafasi na kazi za huduma zitajitokeza kutokana na mahusiano hayo na mahitaji ya uwandani.
Kiongozi mmoja wa harakati, akizungumzia nafasi hii ya mtumishi wa harakati, alisema, “Wamagharibi tunaozungumza nao hawataki kwa kweli kufanya kile tunachohitaji. Kwa mfano, tungewaomba wasiende kuishi Afghanistan, bali watafute kuwafikia Waafghani walioko Ulaya na kushirikiana nasi kuinua maombi na fedha na miunganiko muhimu ya nje kwa ajili ya waamini Waafghani walioko Afghanistan. Hilo halijamvutia yeyote kati ya tuliozungumza nao. Wote wanataka kwenda kuishi nchini humo na kuwa watenda kazi wa mstari wa mbele.”
Kiongozi mwingine wa harakati alisema, “Ni vigumu kwangu kuamini kwamba Wamagharibi wangekuja na kujinyenyekeza chini ya uongozi wetu kwa muda mrefu. Katika hali chache tumejaribu kitu kama hiki. Baada ya miaka michache, wanaamua kwamba wanajua jinsi ya kufanya vizuri kuliko sisi na wanajitenga na kutumia mvuto wa fedha nyingi kupita kiasi kuwachukua baadhi ya viongozi wetu waende kuwafanyia kazi wao.”
Kwa sababu hii tunatumia neno Mtumishi wa Harakati. Kile ambacho harakati zinahitaji zaidi ni watu wenye moyo wa utumishi. Baadhi wametuhimiza tutumie “neno linalovutia zaidi” ambalo lingekuwa rahisi zaidi “kuwauzia wafadhili wao.” Kana kwamba kufuata mfano wa Yesu, aliyekuja si “kutumikiwa bali kutumika,” hakuvutii...
Mtumishi wa Harakati atasimama pamoja na viongozi wa harakati kusaidia kupanua harakati (moja au zaidi), akisaidia katika aina pana sana za shughuli za huduma, kutegemea mahitaji ya huduma na maelekezo ya viongozi wa harakati. Hili litasaidia kuongeza uwezo wa harakati kwenda mbali zaidi na kwa kasi zaidi, na kuwa na ufanisi mkubwa zaidi katika kuendeleza harakati ambazo wanashiriki.
Tunaweza kushirikisha mifano michache ya watu wanaohudumia harakati. Kwa familia moja kubwa ya harakati, baadhi ya wataalamu wa tafsiri kwa sasa wanatoa msaada kutoka nje kwa harakati zinazotafsiri Maandiko. Harakati hizi ziko katika maeneo ambayo mtu wa nje hawezi kuingia kutokana na hali halisi za kisiasa au za kidini, lakini huduma ya wataalamu wa kiufundi na wa tafsiri imekuwa ya thamani isiyo na kifani katika kuwasaidia walioko katika eneo hilo kufanya mchakato wa tafsiri unaotegemea kanisa, unaosaidiwa na kompyuta na unaosaidiwa na wataalamu. Watafsiri hawa wa kitaalamu wamelazimika kumruhusu Mungu abadilishe mtazamo wao kutoka kufanya tafsiri wao wenyewe hadi kuwasaidia walioko katika harakati kujifunza ujuzi na michakato ya kikundi itakayozaa tafsiri bora kabisa.
Katika harakati nyingine yenye waamini zaidi ya 300,000 katika eneo kubwa sana la kijiografia, baadhi ya Wamagharibi (ambao si wataalamu) wanasaidia katika kuhariri video. Wanafanya kazi na viongozi wa harakati kutengeneza video fupi za mafunzo ya uongozi zinazoweza kushirikishwa kutoka simu moja hadi nyingine.
Mfano wa tatu unatoka katika mradi wa Biashara ya Ufalme ambapo watu wa nje husaidia harakati kubaini mapengo ya utamaduni unaokaribiana yanayohitaji harakati. Watu hao wa nje husaidia katika mafunzo ya biashara, maombi na uchangishaji wa fedha (wakiongezea tu fedha zinazochangishwa ndani ya harakati) wakati familia za harakati zinapohamia maeneo mapya na kuanzisha upya biashara ili kujitegemeza kwa muda mrefu katika kulifikia kundi jipya. Hili tayari limeleta kufikiwa kwa sehemu nyingi mpya za idadi ya watu ambao hawajafikiwa. Unaweza kuona video ya wanandoa Watumishi wa Harakati wakieleza mtazamo wao katika bit.ly/MServantVideo.
Ikiwa una nia, tafadhali wasiliana nasi kupitia fomu katika bit.ly/MServant. Tayari tuna mahusiano na mitandao ya harakati—katika Afrika, Asia, na Mashariki ya Kati. Hatuwezi kuhakikisha kuunganishwa, kwa sababu hata ukiwa tayari, tutahitaji kupata harakati iliyo tayari na yenye uwezo wa kukupokea. Na yaelekea kutakuwa na hali kadhaa zenye changamoto, hata uwe tayari kiasi gani, kama vile kujifunza lugha katika baadhi ya miktadha. Lakini tunafurahi kuchunguza uwezekano!
Baadhi ya mipango ya sasa yenye mahitaji mahususi ni:
- Msimamizi anayezungumza Kiingereza na Kifaransa ili kusaidia familia ya harakati
- Wafanyakazi wa matibabu na wa usafirishaji na ugavi ili kusaidia timu za matibabu kutegemeza harakati na kuitikia hali za dharura pamoja na harakati
- Ukuzaji wa biashara ili kusaidia kuimarisha harakati katika kufanya biashara ndani ya harakati yao pamoja na kutumia biashara kufika maeneo mapya
- Kusaidia kuwaandaa watafiti wenyeji kupata mapengo katika maeneo yao
- Mratibu wa mahusiano ya kimataifa ili kusaidia familia ya harakati kuhusiana na waombaji, washirika, wafadhili, n.k.
Yesu alisema, yeyote anayetaka kuwa mkuu miongoni mwenu lazima awe mtumishi wenu (Mathayo 20:26).
Itakuwaje ikiwa njia yako bora zaidi ya kuwafikia kwa kiwango cha juu kabisa wasiofikiwa ingehusisha kazi mbalimbali, zilizochaguliwa na kugawiwa na mtu kutoka utamaduni mwingine? Je, ungekuwa tayari kutoa maisha yako na baadhi ya mapendeleo yako ili uwe na sehemu katika kuzidisha kwa kasi kwa Ufalme miongoni mwa wasiofikiwa? Harakati tayari zinasonga, na unaalikwa kuwa na sehemu katika kuongeza ukuaji wa harakati hizo.
Maelezo
- CPM ni matokeo ya kazi ya Mungu. Mungu ametumia mbinu mbalimbali kuanzisha CPM, zikiwemo DMM, T4T, Mashamba Manne, n.k. Ona http://www.missionfrontiers.org/issue/article/2414-goal kwa Kanuni za Msingi na Matokeo ya Kawaida ya mbinu ya CPM. Rudi kwenye maandishi
- Ona “Global Movement Statistics” katika https://2414now.net/resources. Rudi kwenye maandishi
- Swali hili waliulizwa viongozi wa harakati wanaowakilisha harakati zaidi ya 1,000. Wote walitoa majibu katika kiwango cha 80–90%. Rudi kwenye maandishi
- Ona “Movements Multiplying Movements: How the Bhojpuri CPM has Started Other Movements”: kurasa 185-188 katika 24:14—A Testimony to All Peoples. Rudi kwenye maandishi
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 44:6 (Nov./Des. 2022), uk. 20-22. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


