HUDUMA ZA MAINGILIO NI MOJA YA nguzo za New Harvest Ministries (NHM) tangu kuanzishwa kwake, na zimekuwa na nafasi kubwa katika kudhihirisha huruma ya Mungu, katika kufanya wanafunzi, na katika kupanda makanisa katika jamii zaidi ya 4,000 katika nchi 12. Kazi hizi za huruma zimekuwa vichocheo muhimu katika mabadiliko ya mamia ya maelfu ya wanafunzi wapya, na viongozi wapya wa Kikristo zaidi ya elfu kumi.
Huruma kwa watu ni thamani muhimu ya Ufalme inayopatikana katika vinasaba vya kila Harakati ya Kufanya Wanafunzi. Tuna makumi ya aina tofauti za huduma za maingilio, na kila moja ina nafasi yake ya kipekee katika kutusaidia kuusukuma mbele Ufalme wa Mungu barani Afrika. Nyingi si za gharama kubwa, lakini kwa msaada wa Mungu, zina athari ya kipekee.
Kila huduma hufanywa kwa ubia na wenyeji. Mara nyingi wenyeji hutoa uongozi, nguvu kazi na vifaa—vitu vinavyopatikana kwa urahisi katika jamii ambavyo vinaweza kutumiwa kukidhi mahitaji.
Huruma ya Kishujaa
New Harvest inahudumia nchi nyingi lakini makao yake makuu yako Sierra Leone. Ebola ilipozuka mwaka 2014, hatukuweza kubaki mahali salama na kutolikabili janga lililokuwa kila upande wetu, hasa katika jamii za Kiislamu ambapo taratibu za mazishi zilikuwa zikisababisha mlipuko wa ugonjwa huo kulipuka katika vijiji vingi. Watu hawakuweza hata kuwagusa wazazi au watoto waliokuwa wakifa.
Katika muktadha huo kulikuwa na viongozi kadhaa wa New Harvest waliojitolea katika maeneo hatari zaidi. Baadhi walinusurika lakini kadhaa walipoteza maisha yao wakiwahudumia wengine—wengi wao wakiwa Waislamu.
Chifu wa Kiislamu wa jamii moja alikata tamaa kwa kuona watu wakijaribu kukimbia kijiji kilichowekwa karantini, na alishangaa kuona Wakristo wakija kuhudumu. Kwa siri aliomba maombi haya: “Mungu, ukiniokoa na hili, ukiiokoa familia yangu, nataka sisi sote tuwe kama watu hawa wanaotuonyesha upendo na kutuletea chakula.”
Chifu na familia yake kweli walinusurika, naye akatimiza ahadi yake. Akikariri vifungu kutoka Biblia, alianza kuvishirikisha katika msikiti ambamo alikuwa mzee. Kanisa lilizaliwa katika kijiji hicho, na chifu anaendelea kwenda kijiji hadi kijiji akishirikisha Habari Njema ya upendo wa Mungu.
Kugundua Mahitaji Yanayohisiwa, Kuukabili Upotevu
Kwa NHM, huduma za maingilio huanza kwa kutathmini mahitaji yanayohisiwa ya jamii. Tathmini ya mahitaji inapokamilika, ubia na jamii lazima ujenge kuheshimiana na kuaminiana. Kwa upande wake uhusiano huo hatimaye huleta usimulizi wa hadithi na Usomaji wa Biblia kwa Kugundua (UBK). Huduma za maingilio huufanya upendo wa Kristo uonekane na huacha alama isiyofutika mioyoni.
Njia ya Kuingilia katika Harakati za Ufalme
Maombi ndiyo msingi wa kila kitu tunachofanya. Kwa hiyo mara tathmini inapofanyika, waombaji wetu huanza kuomba kwa ajili ya:
- milango iliyo wazi na mioyo iliyo wazi
- uchaguzi wa viongozi wa miradi
- mikono iliyo wazi ya wenyeji
- kazi isiyo ya kawaida ya Mungu
- uongozi wa Roho
- riziki ya Mungu ya rasilimali zinazohitajika
Vituo vyetu vyote vya maombi vinazijua jamii zinazohudumiwa, na vinafunga na kuomba kwa ajili ya kila moja yao. Na Mungu daima hufungua mlango sahihi, kwa wakati sahihi, pamoja na riziki sahihi.
Maombi ndiyo huduma ya maingilio yenye nguvu zaidi na ufanisi zaidi, na yamesababisha athari ya mtiririko katika harakati nzima. Bila shaka yoyote, tunasadiki kwamba kufunga na kuomba kwa kimkakati huleta kila mara kuvunjwa kwa nguvu za giza. Wakati mwingine kuwaombea wagonjwa ni kiharakisho kizuri cha maingilio yenyewe.
Kupitia maombi ya kudumu tumeona jamii zenye uadui mkubwa zikifunguka, Watu wa Amani wasiotarajiwa wakitambuliwa, na familia nzima zikiokolewa. Utukufu wote ni kwa Baba anayesikia na kujibu maombi. Maombezi ndiyo mkondo wa chini unaotegemeza yote tunayofanya. Mimi huwaambia watu kwamba vipengele vitatu muhimu zaidi vya huduma za maingilio ni: kwanza—maombi, cha pili ni maombi, na cha tatu pia ni maombi.
Kila Mradi Humfanya Mfalme Wetu Ajulikane Sana
Tunafanya chochote kinachohitajika ili kuifikisha Injili kwa watu ili Kristo atukuzwe. Kazi yetu kamwe haituhusu sisi. Inamhusu Yeye. Tunamfanya ajulikane kwa mkazo wa kimkakati juu ya makundi ya watu ambao hawajafikiwa.
Timu ya Elimu
Elimu inapokuwa hitaji lililo dhahiri, basi waombaji hulipeleka hitaji hili kwa Mungu katika maombi.
Tunapokuwa tukiomba, tunashirikiana na jamii kugundua ni rasilimali gani zinazopatikana, na ni nini walicho tayari kutoa ili kukidhi hitaji lao wenyewe. Mara nyingi jamii itatoa ardhi, jengo la jamii, au vifaa vya ujenzi kwa ajili ya kujenga jengo la muda.
Kwa kawaida jamii inatiwa moyo kulipa sehemu ya mshahara wa mwalimu. Mwalimu ana sifa kamili za kitaaluma na pia ni mfanya-wanafunzi/mpanda makanisa mzoefu. Shule huanza na mabenchi machache, penseli au kalamu, sanduku la chaki, na ubao. Shule inaweza kuanzia chini ya mti, katika kituo cha jamii, au katika nyumba ya zamani. Tunaanza polepole na kuikuza shule kitaaluma na kiroho.
Mtu wa Amani anapofungua nyumba yake, inakuwa mahali pa kuanzishia mikutano ya UBK na baadaye kanisa. Tumeanzisha zaidi ya shule 100 za msingi, nyingi zikiwa sasa zinamilikiwa na jamii.
Kutokana na programu hii rahisi Mungu pia ameinua shule kumi na mbili za sekondari, shule mbili za ufundi, na Every Nation College ambacho kina Shule ya Biashara na Shule ya Theolojia zilizoidhinishwa. Kinyume na kile ambacho kingeweza kutarajiwa, Harakati za Kufanya Wanafunzi pia zinahitaji seminari imara.
Matibabu, Meno, Usafi
Tunapotambua hitaji la kiafya, tunatuma timu za wahudumu wa afya wenye sifa nzuri wakiwa na dawa, vifaa na mahitaji mengine. Washiriki wote wa timu zetu ni wafanya-wanafunzi imara na wana ujuzi wa kuwezesha mchakato wa UBK. Wengi pia ni wapanda makanisa wenye ujuzi.
Wakati wagonjwa wakitibiwa, timu inashughulika kumtafuta Mtu wa Amani. Ikiwa hapatikani katika ziara ya kwanza, basi ziara ya pili inafanyika. Mara anapogunduliwa, atatumika kama daraja na mwenyeji wa baadaye wa UBK. Ikiwa mtu huyu hapatikani, basi timu itaitafuta jamii nyingine, huku ikiendelea kuomba kwa ajili ya mlango wazi katika jamii ile ya kwanza.
Meno
Wapanda makanisa kumi wamefunzwa vizuri, wameandaliwa, na kuidhinishwa na mamlaka za afya kufanya ung’oaji na uzibaji wa meno kwa njia ya kutembea. Mwingine, ambaye pia ni mtaalamu wa macho, hupima uwezo wa kuona na kutoa miwani inayofaa (kwa bei ya gharama—ili kuufanya mchakato uendelee na kuepuka utegemezi).
Washiriki wengine wa timu ya afya hutoa mafunzo kuhusu usafi, unyonyeshaji, lishe, chanjo za watoto, na huduma kabla ya kujifungua kwa wanawake wajawazito.
Huduma ya Maingilio Isiyo ya Kawaida Kabisa
Haya yote yanapofanywa kwa namna inayofanana na Kristo, ikitafuta kuufanya Ufalme wa Mungu uonekane, Mungu hutenda na kuufanya uwepo Wake udhihirike. Kwa kawaida hili huanza na familia moja au kiongozi wa jamii asiyetarajiwa. Kwa njia hii tunaona kila mara kuzidisha kunakoendelea kwa wanafunzi, Vikundi vya Usomaji wa Biblia kwa Kugundua, na makanisa.
Kulikuwa na jamii kubwa katika sehemu ya Kusini ya Sierra Leone ambayo ilikuwa ngumu sana kwetu kuipenya. Walikuwa na uadui mkubwa sana dhidi ya Wakristo. Ilikuwa vigumu hata kwa watu waliojitambulisha kama Wakristo kuingia mahali hapo. Kwa hiyo tuliuombea mji huo. Lakini muda ulipita na hakuna mkakati wetu wowote uliofanikiwa.
Kisha ghafla jambo fulani likatokea! Habari za kitaifa zilianza kuripoti kwamba kulikuwa na tatizo la kiafya katika mji huo na vijana wa kiume walikuwa wakiugua na kufa. Ikabainika kwamba walikuwa wamegundua kwamba maambukizi hayo yalihusiana na ukweli kwamba kijiji hicho hakikuwahi kuwatahiri wavulana wao. Nilipokuwa nikiomba kuhusu tatizo hilo nilihisi msukumo wa Bwana kwamba hatimaye hii ilikuwa fursa yetu ya kuuhudumia mji huu.
Tulikusanya timu ya matibabu ya kujitolea na kwenda kwa jamii hiyo tukiwa na vifaa na dawa zinazofaa, na tukauliza kama wangeturuhusu tuwasaidie. Ilikuwa ajabu viongozi wa mji walipokubali. Katika siku ya kwanza waliwatahiri vijana wa kiume zaidi ya 300.
Katika siku zilizofuata wanaume hao walikuwa wakipona tu, na hiyo ilikuwa fursa yetu ya kuanza Vikundi vya Usomaji wa Biblia kwa Kugundua wakati wa siku za kupona. Mwitikio ulikuwa wa ajabu na punde kuzidisha kwa Ufalme kulianza kutokea huku makanisa yakipandwa.
Mahali ambapo Wakristo hawakuweza kuingia palibadilishwa katika miaka michache tu kuwa mahali ambapo Utukufu wa Mungu ulidhihirishwa. Huruma ya watu wa Mungu, nguvu ya maombi mengi, na Neno la Mungu linalobadilisha vilibadilisha kila kitu.
Timu ya Kilimo
Huduma yetu ya kwanza ya maingilio ilikuwa kilimo. Katika nchi ambazo kilimo ni muhimu sana, kilimo huwa lango zuri la kuwahudumia watu. Kilimo kingi ni cha kujikimu na kimsingi kwa matumizi ya familia. Kwa kawaida, hakuna mbegu inayowekwa akiba kwa ajili ya upandaji unaofuata.
Hali hizi zilitufanya tuanzishe benki za mbegu kwa ajili ya wakulima. Kama ilivyo kwa timu zetu nyingine, tuna wataalamu wa kilimo waliofunzwa ambao pia ni wapanda makanisa waliofunzwa. Wataalamu hawa wa kilimo/wafanya-wanafunzi huwaelimisha wakulima. Mafunzo na ulezi wao huleta mahusiano yanayozaa vikundi vya UBK, ubatizo na hatimaye makanisa. Leo wakulima wengi ni wafuasi wa Kristo.
Timu ya Michezo
Huduma ya michezo ni njia nyingine ya maingilio ya ajabu, hasa katika jamii zenye idadi kubwa ya vijana. Tathmini zinapofanywa, na tukagundua idadi fulani ya vijana na shauku, tuseme, ya mpira wa miguu, mara moja tunachukua hatua kwa kutoa changamoto kwa timu yetu yenye nguvu kucheza mechi ya “kirafiki.”
Ikiwa mji hauna timu nzuri, tunawatia moyo kupata wachezaji kutoka karibu ili waweze kuunda timu nzuri. Hili likishafanyika, mara nyingi tunatoa jezi na mipira ya miguu ili kusaidia mazoezi yao.
Siku ya mchezo inapofika kijiji kizima kiko katika hali ya sherehe kikiimba sifa za timu yao. Wana uhakika kabisa kwamba watashinda. Timu yetu inaingia katika mchezo ikijua kitakachotokea.
Wanacheza kwa ushindani lakini mwishowe watashindwa, kwa makusudi.
Wanaposhinda, unaweza kuwazia msisimko wa mji. Hili huwa jambo la kujivunia. Habari haiishii hapa. Kwa kawaida tunaomba mechi ya marudiano. Kwa uhakika mkubwa, jamii hujibu, “Njooni wakati wowote. Tutawashinda tena!”
Mechi ya marudiano kwa kawaida huchezwa katika tarehe ya mapema iwezekanavyo. Katika mchezo wa pili, timu yetu itacheza kwa ustadi mkubwa ikihakikisha inaicharaza timu mwenyeji bila huruma. Baada ya kushindwa kwao vibaya, hali huwa ya msisimko zaidi kwa kuwa timu ya jamii mara moja itaomba mechi nyingine.
Sababu ya kushindwa katika mchezo wa kwanza ni kujenga uhusiano imara na jamii. Tunasadiki kwamba ufuasi hatimaye unahusu jambo moja—uhusiano. Kila uhusiano una pande kuu mbili, uhusiano na Mungu na uhusiano na mwanadamu.
Lengo la mchezo ni kujenga mazingira yatakayoleta vikundi vya UBK na hatimaye makanisa. Makanisa mengi yamepandwa, wanafunzi na viongozi wameinuliwa ambao wanazaana kwa kasi ndani ya makabila yao au jamii zao. Leo, tunasherehekea makocha na wachezaji wengi ambao wamekuwa wanafunzi waliojitoa, wafanya-wanafunzi na wapanda makanisa wenye shauku.
Kupanda Makanisa
Takriban asilimia 90 ya huduma za maingilio tulizojaribu zimeleta kanisa. Na mara nyingi sana makanisa kadhaa hupandwa kutokana na kazi moja. Tunapozitembelea jamii tena tunasikia shuhuda nyingi za mabadiliko ya watu binafsi, ya familia na ya jamii. Huruma kwa watu, ikimfanya Mungu ajulikane sana!
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 39:6 (Nov./Des. 2017), uk. 32-35. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


