Mambo mawili muhimu sana ya Kibiblia husukuma upanuzi wa Harakati za Kupanda Makanisa (CPM). La kwanza huwezesha kupenya katika maeneo mapya. La pili huwezesha upanuzi ndani ya eneo hilo. Kila harakati ni usawazishaji endelevu wa mambo haya mawili.
Kanuni zote mbili zilifundishwa na Yesu kwa wanafunzi wake (Mathayo 10, Luka 10) kuhusu jinsi ya kufikia mahali papya. Kanuni hiyo ya kwanza inahusisha kuwatafuta Watu wa Amani au, kama wengine walivyowaita, Watu wa Udongo wa Nne, wanaozaa matunda mara 30, 60 au 100. Kuwatafuta Watu wa Amani kumekuwa mkakati wa kawaida wa wanamikakati wa CPM walio wengi. Watu wa Amani ni milango iliyoandaliwa na Mungu kuingia katika jamii mpya. Mioyo yao imeandaliwa kwa ajili ya 1) mmisionari, 2) ujumbe, na 3) utume wa kuifikia nyumba yao au mzunguko wao wa ushawishi (Kig. oikos: mtandao wa familia na marafiki wa karibu.)
Kwa bahati mbaya, tunaweza kusisitiza sehemu ya kielelezo cha Mtu wa Amani na kuiathiri kanuni ya pili iliyofungamana nayo sana katika Mathayo 10 na Luka 10. Ikiwa Watu wa Amani (POP) ndio malango, basi kanuni ya pili ni kwamba harakati hupanuka kadiri POP hao na wainjilisti wanaowafikia wanavyozipelekea nyumba zao Injili. Kibiblia, nyumba hizi zinaweza kujumuisha watu kutoka ulimwengu wao wa kibaiolojia, wa kijiografia, wa kikazi na wa hiari. Neno ambalo Agano Jipya linatumia kwa jambo hili ni oikos.
Makala hii si jaribio la kutetea uhalali wa uinjilisti wa oikos. Badala yake ni kutetea umuhimu wa waamini kuwa na imani katika maono kwamba Mungu anataka nyumba yao yote iokolewe.
Tatizo: Uvunaji wa Oikos Usiokamilika
Hivi karibuni, nimegundua kwamba baadhi ya wanamikakati wa CPM hawasisitizi vya kutosha kanuni ya pili: kuivuna oikos. Jambo la ajabu zaidi linaloweza kutokea ni pale nyumba nzima inapoamini kwa wakati mmoja. Lakini kama haitokei, kutoamini kunaweza kuingia kwa urahisi: “Mungu hataiokoa oikos yangu, kwa hiyo ninahitaji kuhubiri Injili mahali pengine.” Nyumba isipokuja kwenye imani mara moja, kuvunjika moyo au kukatishwa tamaa kunaweza kuingia na mtindo usiofaa hujitokeza: mwinjilisti humchukua POP pamoja naye ili kuanza kutafuta POP wapya. Mtu mpya anaokolewa lakini huenda oikos mpya nayo inabaki bila kuvunwa. Mtindo huu wa kushindwa kuivuna oikos ukiendelea kwa muda wa kutosha, watu wa malango (POP) huacha kuwa malango, na tunavuna tu waamini wapya mmoja au wawili katika maeneo mbalimbali. Hakuna makanisa yanayoundwa kuwazunguka Watu hawa wa Amani na upanuzi wa harakati unabaki dhaifu.
Iwe katika jamii zinazoishi kijumuiya au za kibinafsi, makusudi ya Mungu tangu mwanzo yalikuwa kwamba nyumba nzima ifikiwe kwa Injili—iwe kwa wakati mmoja au baada ya muda. Bila maono na imani kwamba nyumba itaokolewa, POP hawatakuwa malango ambayo kupitia kwayo harakati hupanuka. Nyundo ya Oikos iliyo hapa chini ni chombo kinachoweza kurejesha maono na imani hii kwa kila mwamini.
Mtindo na Ahadi: Nyundo ya Oikos
Kuanzia Uumbaji hadi Utimilifu wa mambo yote, ahadi na mtindo wa Mungu ni huu: utaokolewa, wewe na nyumba yako yote. Ahadi ya Mungu kwa watumishi wake waaminifu ni kwamba atawaleta walio wengi au wote walio wao. Nyundo ya Oikos inafuata tu mtindo huo katika kurasa zote za Maandiko. Inaitwa nyundo kwa sababu inaendelea kugonga fikra zako unaposoma wingi wa vifungu vinavyoeleza na kuahidi jambo hili.
Ninakuhimiza uipitie Nyundo ya Oikos wewe mwenyewe, kisha ujifunze kuwashirikisha maono haya waamini unaowafanya wanafunzi. Yanayofuata kwa lazima ni rahisi na rahisi kushiriki. Yanaweza kushirikiwa kwa dakika 10 hadi 15. Nguvu iko katika kurudiwa kwa Mungu akifanya mambo yanayofanana tena na tena katika Agano la Kale na Agano Jipya.
1. Nuhu (Mwanzo 6:8-10, 18; 7:1)
Kwa sababu ya haki na uaminifu wa Nuhu, Mungu aliahidi kumwokoa si yeye tu, bali pia nyumba yake. Wokovu wa nyumba ulitegemea haki ya mtu ambaye Mungu alimwona. Mungu anapotuwezesha kuwapata watu walioandaliwa, tunapaswa kutarajia kwamba atawaokoa si wao tu, bali pia wale walio wao. Nyanja ya oikos: kibaiolojia (familia)
2. Ibrahimu (Mwanzo 18:17-19)
Tunalifahamu agano la Ibrahimu kwamba kupitia yeye Masihi angekuja na mataifa yote yangebarikiwa. Ni wazi kabisa katika Mwanzo 18:17-19 kwamba njia na mtindo ambao kupitia kwao Mungu angeleta baraka juu ya mataifa ulikuwa ni Ibrahimu kushughulikia wokovu katika malezi ya nyumba yake. Baraka ilikuja Mungu alipoleta wokovu kwa nyumba ya Ibrahimu. Ibrahimu alizingatia mambo sahihi (oikos yake), na Mungu alitimiza ahadi pana zaidi kwa sababu ya uaminifu wake. Nyanja ya oikos: kibaiolojia na kikazi (watumishi wake walioajiriwa)
3. Lutu (Mwanzo 19:12-15)
Ingawa Lutu aliishi katika mji mwovu, kusudi la Mungu lilikuwa kumwokoa kila mtu aliyekuwa wake: kihalisi “kila mtu uliye naye katika mji.” Lutu alijaribu kuwaokoa wakwe zake ambao walidhani anafanya mzaha tu. Hata hivyo, Mungu, kwa wema wake, bado aliwaokoa Lutu na binti zake. Kifungu hiki kinaonyesha kwamba oikos ni zaidi sana ya mahusiano ya damu tu; inaonekana kumaanisha kila mtu aliye wetu. Nyanja ya oikos: mahusiano ya kibaiolojia, ya hiari na ya kijiografia.
4. Yusufu (Mwanzo 45:5-11; 50:20)
Wokovu wa nyumba ya Yusufu ulichukua miaka mingi. Mungu haahidi kila mara wokovu wa nyumba zetu mara moja, lakini ahadi bado ipo. Ni ahadi inayotuita kudumu katika ushuhuda wetu kwa wale walio wetu. Mapema katika maisha ya Yusufu, Mungu alimpa ndoto zilizoona mbele wokovu wa nyumba yake. Yusufu hakuwahi kukata tamaa, nasi hatupaswi kukata tamaa. Kupitia taabu nyingi Mungu aliandaa wokovu wa wengi. Nyanja ya oikos: kibaiolojia (familia pana)
5. Rahabu (Yoshua 2:18)
Kupitia tendo la haki la Rahabu la kuwaficha wapelelezi wa Israeli, Mungu aliahidi kumwokoa yeye na wote waliokuwa wake. Wokovu wa nyumba ulikuja kupitia binti, lakini Mungu aliahidi wokovu kwa wazazi, kaka zake na kila mtu aliyekuwa wa nyumba ya baba yake. Hatujui kamwe njia ambayo oikos itaokolewa kupitia kwayo, iwe kupitia kichwa cha familia au mtoto. Nyanja ya oikos: kibaiolojia
6. Mwanamke Mshunami (2 Wafalme 8:1)
Mwanamke mwenye haki aliyemwandalia nabii Elisha chumba cha juu alivuna ahadi ya oikos. Mungu aliandaa mimba ya kimiujiza ya mwana na kisha kufufuliwa kwake kimiujiza alipokufa. Elisha alimjulisha yeye peke yake kati ya Waisraeli wote kwamba njaa ilikuwa inakuja katika nchi. Mungu alileta wokovu kwake na kwa nyumba yake—katika hali hii kupitia mke. Nyanja ya oikos: kibaiolojia
7. Mtu wa Gerasi Aliyepagawa na Pepo (Marko 5:1-20; 7:31, Mathayo 15:29-31)
Mtu aliyepagawa na pepo ni mfano mzuri ajabu wa Mungu kuahidi wokovu si kwa mtu mmoja tu, bali kwa kundi kubwa la watu. Badala ya kumruhusu mtu huyo aliyepagawa na pepo aandamane naye, Yesu alimpa utume ulio wazi—oikos yake pana ya marafiki katika miji kumi. Sifa yake ilikuwa kubwa kiasi kwamba alienda katika eneo lote la miji kumi (Dekapoli) na kuleta matokeo makubwa. Nyanja ya oikos: ya hiari, kijiografia
8. Mwanamke Msamaria (Yohana 4:7-42)
Mungu alimwandaa mwanamke mwenye historia ya kusikitisha sana apokee wokovu na kupitia yeye alete wokovu kwa mji mzima. Si kwamba tu Mungu alitaka kuleta wokovu kwa mwanamume aliyekuwa akiishi naye, bali alitaka kuleta wokovu kwa jamii nzima ya Sikari. Nyanja ya oikos: kibaiolojia, kijiografia
9. Afisa wa Kana (Yohana 4:46-54)
Katika mji wa Kana, mwana wa afisa mmoja alikuwa mgonjwa sana na karibu kufa. Yesu alimtumia mtu huyu ujumbe kwamba angemponya mwana. Jambo hili lilipotokea, baba na nyumba yake yote walimwamini Yesu. Nyanja ya oikos: kibaiolojia
10. Dorkasi (Matendo 9:36-42)
Huko Yafa, mwanafunzi Dorkasi alijaa matendo ya huruma na ulimwengu wake ulijaa wajane wengi waliompenda sana. Mungu alipomfufua Dorkasi kutoka kwa wafu wajane hawa walishangaa na wengi katika eneo lote walimwamini Bwana. Nyanja ya oikos: ya hiari (wajane), kijiografia
11. Kornelio (Matendo 10:1-48; 11:14)
Malaika aliposema na Kornelio kabla hajamwamini Yesu, alimpa Kornelio maono yaliyo wazi: kwamba si tu yeye angeokolewa, bali ahadi ilikuwa kwa nyumba yake yote (Matendo 11:14). Katika hali hii kundi kubwa ambalo Kornelio alilikusanya kama nyumba yake lilikuwa familia na marafiki (Matendo 10:24). Nyanja ya oikos: kibaiolojia, ya hiari, huenda pia kikazi (askari wengine)
12. Lidia (Matendo 16:13-15, 40)
Lidia, mwanamke aliyekuwa akimtafuta Mungu, alipokea wokovu na mara moja Mungu aliiokoa nyumba yake. Inaonekana nyumba yake kisha ikawa mahali pa kukutania kwa kanisa la Filipi. Nyanja ya oikos: kibaiolojia, ya hiari (wanawake wengine)
13. Mlinzi wa Gereza wa Filipi (Matendo 16:23-34)
Mtu aliyekuwa amewapinga Paulo na Sila saa chache tu kabla alifunguka baada ya tetemeko la ardhi. Mara moja Mungu alimwokoa. Alikuwa na shauku kubwa sana ya familia yake kuamini kiasi kwamba aliwaamsha kutoka usingizini na familia nzima ilibatizwa kabla ya mapambazuko. Nyanja ya oikos: kibaiolojia
14. Krispo na Stefana (Matendo 18:8; 1 Wakorintho 16:15)
Hatujui mengi kuhusu watu hawa isipokuwa kwamba wokovu wao ulikuwa muhimu sana katika kuanzishwa kwa kanisa la Korintho. Kwanza, nyumba ya Stefana ilikuwa waamini wa kwanza katika jimbo zima la Akaya. Pili, Krispo, mkuu wa sinagogi lililokuwa likimpinga Paulo, aliupokea wokovu na nyumba yake yote iliamini. Hilo lazima liliwapiga watesaji pigo kubwa kiasi gani! Nyumba ndizo njia ambazo Mungu hutumia kufungua maeneo mapya kwa ajili ya ufalme. Nyanja ya oikos: kibaiolojia
15. Yesu (Matendo 1:14)
Kati ya maelfu mengi ya watu ambao Yesu aliwahudumia katika Israeli wakati wa miaka yake mitatu ya huduma, hakuwahi kupuuza kuifikia nyumba yake mwenyewe. Ingawa alidhihakiwa na ndugu zake ambao hawakumwamini (Yohana 7:5), Yesu hakuwakatia tamaa. Wanafunzi wa kwanza walipokusanyika katika chumba cha juu kuomba, ni nani walikuwepo isipokuwa Mariamu, mama yake Yesu, na ndugu zake? Mungu alitenda wokovu kamili katika nyumba hiyo. Mmoja wa ndugu hao (Yakobo) baadaye angeongoza kanisa la Yerusalemu na kuandika kitabu cha Yakobo. Ndugu mwingine aliandika kitabu kifupi cha Yuda. Nyanja ya oikos: kibaiolojia.
Wape wengine maono na imani hii
Vifungu hivi kumi na vitano vinaonyesha kusudi la Mungu katika historia yote la kumwokoa mtu na kupitia yeye nyumba nzima: familia, marafiki, majirani na wafanyakazi/wanafunzi wenzake. Jambo hili halipaswi kutushangaza kwa sababu Petro alitangaza ahadi hiyo hiyo Siku ya Pentekoste watu 3,000 walipookolewa. Hakuwaita tu kwenye wokovu (Matendo 2:38) bali aliwapa maono ya nyumba zao (vizazi vitatu):
“Kwa maana ahadi ni kwa ajili yenu na kwa ajili ya watoto wenu na kwa ajili ya wote walio mbali, kila mtu ambaye Bwana Mungu wetu anamwita kwake.” (Matendo 2:39, ESV)
Nyundo ya Oikos inapaswa kutufunulia mtindo wa Mungu wa tangu zamani wa upanuzi wa ufalme:
- Wokovu wa nyumba: Lazima tusilenge tena watu mmoja mmoja tu kuja kwenye imani. Iwe makundi yanaamini wote kwa wakati mmoja, au kwa kipindi cha muda, ahadi na kusudi la Mungu ni kwamba Watu wa Amani wazifikie nyumba zao zote. Mtazamo wetu tangu mwanzo hadi mwisho lazima uwe kwenye nyumba huku Watu wa Amani wakiwa malango ya kuingia ndani yake.
- Fasili pana ya oikos: Inaonekana oikos hujumuisha wote walio wako: kibaiolojia (familia), kijiografia (majirani), kikazi (wafanyakazi wenzako/wanafunzi wenzako) na ya hiari (wale mnaoshiriki mambo mnayoyapenda).
- Wape imani ya wokovu wa nyumba: Lazima tusawazishe kati ya kuwafikia Watu wa Amani wapya na kuwasaidia kuifikia oikos yao. Kamwe si suala la ama hiki au kile, bali lazima tuwasaidie Watu wa Amani kukua katika imani na uwezo wa kuipata nyumba yao yote.
- Mavuno ya oikos ya makusudi: Ili kuwasaidia kuzifikia nyumba zao, huenda tukataka kufanya mavuno ya oikos (au “msukumo”) pamoja nao—yaani, kuandaa matukio au fursa fulani za kuikusanya oikos pamoja ili isikie Injili kutoka kwa wengine (kama Petro alivyokwenda kwa Kornelio), kujifunza Biblia pamoja, n.k. Ikiwa oikos inachelewa kuja kwenye wokovu, panga matukio ya kuivuna pamoja na Mtu wa Amani.
- Kasi ikipungua, tafuta Watu wa Amani wapya: Oikos inapokuwa imefikiwa kikamilifu au hakuna maendeleo yanayopatikana, huenda tukahitaji kutumia muda zaidi kutafuta Watu wa Amani wapya na kumsaidia Mtu wa Amani wa kwanza kujifunza kufanya vivyo hivyo pamoja nasi.
Nyundo hii ikusaidie katika kuwapa waamini wote maono na imani kwamba watakuwa mifereji ya wokovu kwa wengi. Maono yetu lazima yasiwe Watu wa Amani tu, bali nyumba nzima za imani.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 40:5 (Sep./Okt. 2018), uk. 44-47. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


