Mara nyingi sana tunauliza swali lisilo sahihi: “Mapenzi ya Mungu kwa maisha yangu ni nini?” Swali hilo limejikita sana katika nafsi. Linahusu wewe na maisha yako.
Swali sahihi ni “Mapenzi ya Mungu ni nini?” Basi. Kisha “Maisha yangu yanawezaje kuyatumikia vizuri zaidi?” Ili kulitukuza jina la Mungu, lazima uelewe kile ambacho Mungu anafanya katika kizazi chetu—kile ambacho Yeye anashughulikia.
Ili kubaini hilo unahitaji kujua kile ambacho Mungu anafanya katika historia: simulizi lililoanza katika Mwanzo 1 na litakalomalizika katika Ufunuo 22. Kisha unaweza kupata nafasi yako katika mtiririko wa kihistoria.
Kwa mfano, Mfalme Daudi alilitumikia kusudi la Mungu katika kizazi chake kwa namna ya pekee (Matendo ya Mitume 13:36) hasa kwa sababu alikuwa mtu aliyeupendeza moyo wa Mungu (Matendo ya Mitume 13:22). Alitafuta kuchangia juhudi zake kwa simulizi la Baba. Ahadi kwa Ibrahimu (kurithi nchi na kuwa baraka kwa mataifa) ilipiga hatua kubwa mbele Mungu alipompata mtu ambaye angekuwa na moyo wake na kuyatumikia makusudi yake. Kulingana na 2 Samweli 7:1, hapakuwa na mahali palipobakia kwa Waisraeli kushinda.
Moyo wa Baba yetu ndio simulizi kuu la historia. Huharakisha mtiririko wa simulizi anapowapata wahusika wakuu walio na moyo wake.
Mungu anakiita kizazi kipya ambacho hakitakuwa tu ndani ya simulizi bali kitakachoyamaliza simulizi hilo, kuiharakisha hadithi kufikia kilele chake. Anakiita kizazi ambacho siku moja kitasema, “Hakuna mahali palipobakia kwa Ufalme wa Mungu kupanuka” (kwa mfano Warumi 15:23).
Kulijua simulizi kuu ni kuyajua mapenzi ya Mungu.
Ukishalijua simulizi kuu, unaweza kuchukua nafasi yako ndani yake, si kama mhusika wa pembeni bali kama mhusika mkuu anayesukumwa mbele kwa nguvu za Mwandishi.
Simulizi kuu lilianza katika Uumbaji (Mwanzo 1) na linamalizika katika Utimilifu (kurudi kwa Yesu — Ufunuo 22). Ni hadithi ya mbio kuu. Kila kizazi hukimbia mzunguko mmoja katika mbio hizi za kupokezana vijiti. Lakini kutakuwa na kizazi cha mwisho kitakachokimbia mzunguko wa mwisho—kizazi kitakachoshuhudia Mfalme akipokea thawabu yake kwa juhudi zake za historia nzima.
Kutakuwa na kizazi cha mzunguko wa mwisho.
Kwa nini kisiwe sisi?
Mungu anatuandaa kumaliza hadithi, tukichagua kuikubali nafasi hiyo.
Usilisahau simulizi kuu: Kumbuka!
Katika barua ya mwisho aliyoiandika, Petro aliwaita wanafunzi wasisahau sehemu yao katika simulizi kuu (2 Petro 1:13-15). Petro alikuwa ameishi kwa ajili ya siku ya kurudi kwa Bwana wake, akikimbia mzunguko wake katika mbio. Kifo chake kilipokaribia, aliliasa kanisa lisipunguze mwendo bali liharakishe simulizi—liiharakishe siku ile.
Kwa kuwa vitu hivi vyote vitayeyushwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa namna gani katika maisha ya utakatifu na utauwa, mkiitazamia na kuuharakisha ujio wa siku ya Mungu! (2 Petro 3:11-12, msisitizo umeongezwa)
Katika sura ya mwisho ya maisha yake, Petro kwa mara nyingine aliwakumbusha kuhusu kusudi kuu—simulizi kuu:
Wapendwa, hii sasa ni barua ya pili ninayowaandikia. Katika barua zote mbili ninaziamsha nia zenu safi kwa njia ya kuwakumbusha, 2ili mkumbuke maneno yaliyotabiriwa na manabii watakatifu na amri ya Bwana na Mwokozi kupitia mitume wenu. (2 Petro 3:1-2, msisitizo umeongezwa)
Mioyo yao ilikuwa safi, lakini ilikuwa rahisi kwao kusahau mtiririko wa simulizi na kupoteza nafasi yao yenye kusudi. Unyoofu wa moyo si mbadala wa kuishi kwa kusudi katika simulizi kuu la historia. Je, unachukua kwa makusudi sehemu yako katika mbio kuu?
Petro aliwakumbusha kuhusu simulizi kuu lililotolewa kwa amri ya Yesu:
Na habari njema hii ya utawala wa Mfalme itatangazwa katika ulimwengu wote kuwa ushuhuda wa kujitoa kwa kila kundi la watu [ethne], ndipo mwisho utakapokuja. (Mathayo 24:14; tafsiri ya mwandishi)
Je, unalijua simulizi kuu?
Kusudi la Historia
Simulizi hili la msingi linapita katika Biblia yote likijisuka katika kila kitabu kati ya vitabu 66. Hata hivyo ni rahisi sana kulisahau simulizi hili, na wengi hulidhihaki wazo kama hilo:
Katika siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka wakidhihaki, wakifuata tamaa zao wenyewe za dhambi. Watasema, “Iko wapi ahadi ya kuja kwake? Kwa maana tangu mababa walipolala, vitu vyote vinaendelea kama vilivyokuwa tangu mwanzo wa uumbaji.” (2 Petro 3:3-4)
Hali hii inakieleza kizazi chetu, si cha Petro tu.
Simulizi kuu la historia ni lipi?
- UUMBAJI: Katika Mwanzo 1-2, Mungu aliwaumba wanadamu kwa kusudi moja—kuwa Bibi Arusi (mwenzi) kwa ajili ya Mwanawe ili akae naye milele katika upendo na kuabudu.
- ANGUKO: Katika Mwanzo 3, kupitia dhambi, wanadamu walianguka kutoka katika mpango wa Mungu—hawakuwa tena katika uhusiano na Muumba.
- KUTAWANYIKA: Katika Mwanzo 11, lugha zilichanganywa na wanadamu walitawanywa hadi miisho ya dunia—wakiwa mbali na ukombozi wa Mungu.
- AHADI: Kuanzia Mwanzo 12, Mungu aliahidi kuyaita mataifa ya dunia yarudi kwake kupitia gharama ya damu ya Mkombozi, inayotangazwa kupitia juhudi za watu wa Mungu (wazao wa Ibrahimu) za kushiriki habari njema.
- UKOMBOZI: Katika Injili, Yesu alitoa gharama ya kulipa deni la dhambi ili kuwakomboa watu wa Mungu—watu kutoka katika kila ethne (kundi la watu).
- AGIZO: Mwishoni mwa maisha yake, Yesu aliwatuma watu wa Mungu kumaliza utume wa Mungu—simulizi kuu—na anaahidi nguvu zake ili kufanya hivyo.
- KUFANYA WANAFUNZI: Tangu Kitabu cha Matendo ya Mitume hadi leo, watu wa Mungu wamebarikiwa kwa ajili ya agizo moja kuu: kwenda ulimwenguni kote na kuutangaza ukombozi huu—wakifanya wanafunzi wa kila ethne—ili kuwa Bibi Arusi kamili wa Kristo.
- UTIMILIFU: Wakati wa Utimilifu, Yesu atarudi kumchukua Bibi Arusi wake—atakapokuwa amekamilika na yuko tayari.
Kila kitu kuanzia Mwanzo 3 hadi Ufunuo 22 kinahusu kumwita tena Bibi Arusi wa Yesu kutoka miongoni mwa mataifa. Hadi Bibi Arusi atakapokamilika, utume wa kanisa haujamalizika.
Hili ndilo simulizi kuu ambalo Petro alilizungumzia katika sura yake ya mwisho.
8 Lakini, wapendwa, msisahau jambo hili moja, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. 9 Bwana hakawii kutimiza ahadi yake kama wengine wanavyokuhesabu kukawia, bali anawavumilia ninyi, hapendi mtu yeyote apotee, bali wote wafikie toba. 10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwizi, na ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu, na miili ya mbinguni itaungua na kuyeyuka, na dunia na kazi zilizofanywa ndani yake zitafunuliwa. (2 Petro 3:8-10, msisitizo umeongezwa)
Mungu ni mvumilivu. Hatamtuma Mwanawe arudi hadi simulizi kuu litakapomalizika. Mungu hakawii, kwa maana hapendi kundi lolote la watu (ethne) lipotee. Anataka mataifa yote yaliyotawanywa ya Mwanzo 11 yawe sehemu ya bibi arusi wa Kristo kwa idadi kubwa.
Ni hizi ethne ambazo Yesu alizizungumzia katika Mathayo 24:14. Ni hizi ethne ambazo alizizungumzia katika Agizo Kuu (Mathayo 28:18-20 “wafanyeni wanafunzi wa ethne zote”). Ni hizi ethne zinazoonyeshwa katika Ufunuo 7:9.
Kilele cha simulizi kuu la historia ni Bibi Arusi kamili anayeletwa kwa Mwana pamoja na karamu kuu ya harusi ya kusherehekea.
Katika sura ya mwisho ya Petro, alizungumzia kukusanywa kwa Bibi Arusi huyu na pia anayataja maandiko ya Paulo:
Kwa hiyo, wapendwa, kwa kuwa mnayatazamia haya, fanyeni bidii ili mkutwe naye bila doa wala dosari, mkiwa na amani. Na mhesabu uvumilivu wa Bwana wetu kuwa wokovu, kama vile ndugu yetu mpendwa Paulo naye alivyowaandikia kwa kadiri ya hekima aliyopewa, kama afanyavyo katika barua zake zote.…(2 Petro 3:14-16, msisitizo umeongezwa)
Paulo alilizungumzia simulizi hilohilo akitumia maneno yaleyale:
Kristo alilipenda kanisa na akajitoa kwa ajili yake, 26 ili alitakase, akiisha kulisafisha kwa kuoshwa kwa maji katika neno, 27 ili ajiletee kanisa katika utukufu, bila doa wala kunyanzi wala kitu chochote cha namna hiyo, bali liwe takatifu na bila dosari…. Siri hii ni kubwa, nami nasema kwamba inamhusu Kristo na kanisa. (Waefeso 5:25-27, 32, msisitizo umeongezwa)
Paulo alizungumzia mpango huohuo katika Waefeso 1:
9 Sasa Mungu ametufunulia mapenzi yake ya siri kuhusu Kristo—ambayo ni kuutimiza mpango wake mwema. 10 Na huu ndio mpango: Wakati ufaao atakusanya kila kitu pamoja chini ya mamlaka ya Kristo—....kila kitu kilicho mbinguni na duniani. (Waefeso 1:9-10, NLT, msisitizo umeongezwa)
Mpango wa Mungu tangu Uumbaji hadi Utimilifu umekuwa kuwakusanya tena watu kutoka kila lugha na utamaduni ili warudi chini ya mamlaka ya Kristo kama Bibi Arusi wake milele.
Lakini kwa sasa, Bibi Arusi huyo hajakamilika. Bado anakosa mkono, jicho na mguu. Vazi lake bado lina madoa na makunyanzi. Wakati Bwana Arusi amesimama madhabahuni tayari kumkumbatia Bibi Arusi wake mikononi mwake, Bibi Arusi anaonekana kutokuwa na haraka kubwa ya kujiandaa kwa ajili ya Siku ya Harusi.
Lakini msimamo wa Bibi Arusi unabadilika. Hii ni mojawapo ya sifa kuu za pekee za kizazi chetu, na inatuelekeza kwenye upekee wa mzunguko wetu. Katika miongo miwili iliyopita kanisa la ulimwengu limeongeza kasi ya kuanzisha kazi miongoni mwa zaidi ya makundi 8000 ya watu wasiofikiwa yaliyobaki ulimwenguni—sehemu za ulimwengu ambazo bado hazijawakilishwa katika Bibi Arusi kwa idadi kubwa.
Hii ilikuwa hatua nzuri ya kwanza, lakini kuanzisha kazi hakukuwa kamwe lengo. Kwa kuwa zaidi ya watu bilioni 2 ulimwenguni bado hawana fursa ya kuifikia Injili, juhudi zetu za kuanzisha kazi miongoni mwao lazima zibadilike. Lengo letu ni kuwafikia, si tu kuanzisha kazi miongoni mwao.
Yesu alituambia tuombe Ufalme uje kikamilifu duniani kama mbinguni (Mathayo 6:9-10). Injili inapoanzisha kazi mahali pasipofikiwa, Ufalme wa Mungu lazima ufunguke kwa nguvu. Yesu daima aliona maono ya wanafunzi wakifanya wanafunzi ili wafanye wanafunzi, na makanisa yakipanda makanisa yanayoweza kupanda makanisa. Hiki ndicho kilichotokea katika Kitabu cha Matendo ya Mitume. Ilikuwa ni vinasaba vya ufuasi wa mwanzo kwamba kila mwanafunzi awe mfuasi wa Yesu na pia mvuvi wa watu. (Marko 1:17)
Yesu haridhiki na Bibi Arusi mdogo au asiyekamilika. Anataka Bibi Arusi asiyeweza kuhesabiwa na mtu yeyote kutoka katika kila moja ya ethne. Njia pekee ya kufanya hivyo ni kupitia Ufalme ukizaana katika kila moja yao. Kasi inaongezeka ili harakati za Mungu ziwe za kawaida tena. Katika miaka 20 iliyopita idadi ya harakati hizi ulimwenguni imeongezeka kutoka chini ya 10 hadi karibu 600. Mungu anaharakisha ratiba ya historia!
Hata hivyo bado kuna maelfu ya makundi ya watu na maeneo ambayo hayajafikiwa yasiyo na kanisa linalozaana miongoni mwao. Pamoja na Petro, lazima tuungane na Mungu katika kuharakisha mtiririko wa simulizi kuelekea mwisho wake.
Iharakisheni siku
11 Kwa kuwa vitu hivi vyote vitayeyushwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa namna gani katika maisha ya utakatifu na utauwa, 12 mkiitazamia na kuuharakisha ujio wa siku ya Mungu!....(2 Petro 3:11-12, msisitizo umeongezwa)
“Kutazamia” kunamaanisha kuwa katika hali ya hamu na kusubiri jambo fulani. Unasubiri nini kwa hamu? Je, unatarajia kwa shauku mwisho wa simulizi hili kuu? Mungu ametupa fursa ya ajabu ya kuungana naye katika mbio za historia ili kuharakisha mwendo wa Kanisa kuelekea mstari wa kumalizia. Mstari wa kumalizia unaonekana na kwa nguvu za Roho tunaweza kukimbia mzunguko wa mwisho.
Mojawapo ya mamaliziko makubwa zaidi—mizunguko ya mwisho—katika historia ya kuogelea ilitokea katika Michezo ya Olimpiki ya Beijing ya 2008 katika mbio za kupokezana za wanaume za mtindo huru za 4x100m. Michael Phelps na Wamarekani wengine watatu hawakupewa nafasi ya kushinda. Kufikia mzunguko wa mwisho, walikuwa nyuma ya aliyeongoza kwa karibu urefu mzima wa mwili. Robo tatu ya sehemu ile ya mwisho, Jason Lezak ambaye hakuwa akijulikana alianza kujisukuma kwa nguvu kuliko alivyowahi kufanya maishani mwake. Aliongeza kasi yake kupita matarajio yote. Katika sekunde ya mwisho alinyoosha mkono kugusa ukuta na kushinda. Umati ulipochachamaa, mtangazaji aliendelea kusema, “Siamini! Haiwezekani!” Mtu ambaye umati ulikuwa haujawahi kumsikia aliogelea mzunguko wa mwisho wa kustaajabisha zaidi katika historia ya kisasa.
Marudio ya mbio hizo yanaonyesha makundi mawili yaliyoharakisha mamaliziko hayo ya ajabu:
- Wachezaji wenzake watatu wa Lezak waliosimama kwenye mstari wa kumalizia wakimhimiza aongeze kasi yake
- Jason Lezak akiongeza juhudi zake kupita kile kilichoonekana kuwezekana
Wingu kubwa la mashahidi waliokimbia mbio kabla yetu (Waebrania 12:1) linatuhimiza kusonga mbele. Ni njia gani bora zaidi ya kuziheshimu juhudi zao kuliko kumaliza kile walichokianza?
Kutakuwa na kizazi kitakachoongeza kasi yake kupitia juhudi ya mwisho iliyojaa imani na kujitoa kwa nguvu za Roho ili kupita matarajio yote.
Na, kisha, Bwana Arusi atakapokuwa tayari, atarudi.
Fanyeni haraka!
Kabla Petro hajamaliza barua yake, alitoa wito mmoja mkuu wa mwisho kwa waamini wasichelewe kuchukua sehemu yao:
Kwa hiyo basi, marafiki wapendwa, kwa kuwa mnatazamia jambo hili, fanyeni kila jitihada [kihalisi “fanyeni haraka”] ili mkutwe bila doa, bila lawama na mkiwa na amani naye.... (2 Petro 3:14, NIV)
Je, unatamani kuona uamsho ukikujia wewe, kanisa lako au shirika lako? Jibu ni kufanya haraka kuwa aina ya watu wanaofanya sehemu yao katika simulizi kuu la historia. Unapolitumikia simulizi kuu la historia, Baba hufurahi sana kumimina Roho wake kwa ajili ya juhudi hiyo.
Mungu anatuita tuchukue sehemu yetu katika mbio hizi kuu. Kwa bahati mbaya kwa sehemu kubwa ya Kanisa hii ni kucheza tu bwawani bila kujua kabisa mbio zinazoendelea kuwazunguka.
Badala ya kucheza (kuishi kwa ajili ya simulizi lako mwenyewe) lazima uruke bwawani na kuogelea mzunguko wa mwisho kwa juhudi za kujitoa. Uwe mhusika mkuu katika hadithi—si mhusika wa pembeni.
Chagua kulenga kufikia kila kundi la watu wasiofikiwa na kila mahali pasipofikiwa, lakini fanya hivyo kupitia harakati za wanafunzi, makanisa na viongozi wanaozaana kama zile za Matendo ya Mitume. Ni hapo tu ndipo tunaweza kweli kujaza maeneo yote kwa Injili ya milele ya Mfalme wetu anayekuja.
Uliza “Mapenzi ya Mungu ni nini?” na “Maisha yangu yanawezaje kulitumikia kusudi hilo vizuri zaidi katika kizazi hiki?”
Yesu anaahidi uwepo wake wenye nguvu kwa wote wanaoungana katika juhudi hiyo....(Mathayo 28:20).
Kizazi fulani kitamaliza mzunguko wa mwisho. Kwa nini kisiwe sisi?
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 39:6 (Nov./Des. 2017), uk. 40-43. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


