Kila mtu anastahili kuwa na Neno la Mungu katika lugha ya moyo wake. Leo, tuko karibu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kuona Biblia ikitafsiriwa katika kila lugha, lakini vizuizi vikubwa bado vimesalia. Zaidi ya asilimia 20 ya watu wa ulimwengu bado wanaisubiri Biblia katika lugha yao wenyewe (lugha 6,600+).
“Hatua ya mwisho” hutumika kueleza sehemu fupi ya mwisho ya kuwafikishia wateja huduma au bidhaa. Mipango ya usafirishaji ya hatua ya mwisho kwa kawaida ndiyo sehemu tata zaidi na ya gharama kubwa zaidi katika kukamilisha huduma au usafirishaji. Mwenendo huu huu hutokea katika kukamilisha kazi ya kutafsiri Biblia katika kila lugha.
Kuna sababu za kukosekana kwa Biblia katika lugha zilizobaki za “hatua ya mwisho” zisizo na Biblia. Nyingi ya hizi bado hazina Biblia katika lugha yao wenyewe kwa sababu wazungumzaji wake wanaishi katika maeneo yenye uadui dhidi ya Injili. Tofauti na tafsiri za kimapokeo za zamani na za sasa ambapo timu za tafsiri hukaa mahali fulani na kufanya kazi pamoja kwa miaka mingi, mara nyingi watafsiri wa nje wanaotafuta kufanya tafsiri katika maeneo yenye vizuizi vya kisiasa na/au yenye uadui hawawezi kupata kibali cha kuingia katika maeneo hayo. Watafsiri walio na uwezo wa kuingia mara nyingi hulazimika kufanya kazi kwa siri, wakihama kutoka mahali pamoja kwenda pengine na kuficha kazi yao kwa marafiki, familia na jamii. Mara nyingi kwa sababu ya vitisho vya kuuawa na mateso, watafsiri husubiri hadi kazi ikamilike, kisha kwa siri wanapeleka kazi iliyokamilika kwa washirika ili ichapishwe na kushirikiwa na wengine. Katika miaka ya hivi karibuni, kumekuwa na matukio mengi ya watafsiri katika maeneo ya aina hii kutekwa nyara na/au kuuawa.
Changamoto moja inayokabiliwa katika mazingira haya ni kuhakikisha kwamba watafsiri wanapata ulezi, msaada na ufadhili unaofaa wanaouhitaji. Hata hivyo, mifumo ya kimapokeo ya kusaidia tafsiri na kuipima haiwezekani. Sisi tunaosaidia tukiwa nje lazima tujirekebishe kulingana na hali halisi mpya na kutambua kwamba wanaume na wanawake hawa wanaohatarisha maisha yao wanastahili juhudi zetu bora na msaada wetu wenye moyo wa kitumishi, badala ya kuwataka waendane na mifumo na mitazamo yetu ya awali ya tafsiri.
Hata hivyo, hakuna yeyote anayehusika anayetaka tafsiri ya Neno la Mungu iliyofanywa ovyo na yenye ubora duni. Basi tunawezaje kuhakikisha ubora na uwajibikaji kwa wafadhili wa nje huku tusihatarishe maisha ya wale walio katika hatua ya mwisho wakitafsiri katika maeneo haya yenye vizuizi?
Muungano wa Harakati za Kupanda Makanisa (CPM) wa Antioch Family of Churches umeanzisha mchakato wa hatua saba ambao umezalisha tafsiri bora huku pia ukitoa vipimo na matokeo yanayokidhi mahitaji ya wafadhili wa nje. Viongozi wa 24:14 wameuidhinisha mchakato huu na wanachunguza jinsi ya kusaidia CPM nyingine kufuata mfumo huu. CPM ina vizazi vinne au zaidi vya makanisa yanayopanda makanisa (makanisa wazazi yanayopanda makanisa watoto, wajukuu na vitukuu, yenye matawi mengi ya mti wa familia)—kwa kawaida hii inamaanisha angalau makanisa 100+ na wanafunzi waliobatizwa 1500+. Muungano mpana wa 24:14 wa Harakati za Kupanda Makanisa unawakilisha CPM 1053 zenye wanafunzi zaidi ya milioni 74, hasa katika maeneo yenye uadui ambayo hapo awali hayakuwa yamefikiwa na Injili.
Mchakato wa Hatua Saba wa Kuhakikisha Ubora wa Tafsiri na Athari ya Maandiko kwa maeneo yenye uadui ni:
Ubora wa Tafsiri
1) Uchaguzi wa Lugha: Uongozi wa CPM isiyo na Biblia unatambua kupitia maombi na ushauri pamoja na washiriki wengine wa 24:14 kwamba tafsiri ya Biblia katika lugha fulani (au lugha kadhaa) inahitajika. Baada ya maombi na majadiliano ya kina, lugha (au lugha hizo) huchaguliwa kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:
- kujitoa kwa viongozi kukamilisha mchakato wa tafsiri na kufanya matumizi bora kabisa ya kusambaza na kutumia Maandiko yaliyotafsiriwa;
- uwezo uliopo wa CPM na wa washirika wa nje wanaoweza kusaidia mchakato huo;
- usalama wa watafsiri pia ni jambo la kuzingatia, ambao unawezekana zaidi pale kuna kundi kubwa zaidi la waamini kama tunavyoona katika CPM;
- harakati nyingine zinazohusiana na lugha hiyo katika nchi tofauti;
- mafunzo yaliyopo, zana za tafsiri na maandiko ya marejeo;
- hitaji na uwezekano wa kutafsiri katika lugha mbili au zaidi zinazohusiana kwa karibu au lahaja kuu za lugha kubwa sana.
2) Kuwapata Wanaofaa na Kuwaandikisha Wanatimu wa Tafsiri: Katika kila lugha, kundi la mwanzo la wazungumzaji 25‐30 wa muda wote wa lugha mama, wanaojua lugha mbili na wanaojua kusoma na kuandika, huthibitishwa mapema kuwa wanafaa na viongozi wa makanisa yao ya mahali.
3) Mafunzo/Maandalizi ya Timu ya Tafsiri: Mlezi wa Tafsiri wa 24:14 (au walezi kadhaa) huanza kuifunza timu ya tafsiri. Zana za kujifunzia binafsi na nyenzo nyingine za msaada pia hutolewa ili kuzisaidia timu kushughulikia mapengo na kupata fursa za kujifunza zaidi.
4) Uandishi wa Rasimu za Mwanzo za Tafsiri Huanza: Baada ya kuthibitishwa kuwa wanafaa na viongozi wa makanisa yao ya mahali na Walezi wa Tafsiri wa 24:14, timu hizi hufanya kazi kwa muda wote kwa ushirikiano ili kufafanua maneno muhimu na kuzalisha rasimu bora za Maandiko. Kila rasimu ya mwanzo hupitiwa na Mlezi wa Tafsiri kwa mujibu wa Miongozo ya Tafsiri ya 24:14.
5) Kukagua/Kuhariri Maandiko: Sehemu za Maandiko hukaguliwa na wenzao, hukaguliwa na kanisa la mahali na kisha hutumwa kwa Walezi wa Tafsiri ili zipitiwe. Baada ya kuidhinishwa kama rasimu ya mwanzo, maandiko hujaribiwa katika jamii kupitia seti ya maswali iliyoidhinishwa ili kusaidia kubaini uwazi, ulaini wa lugha, usahihi na kukubalika kwake. Marekebisho hufanywa na kujaribiwa tena. Kwa jumla katika kila lugha, wastani wa watu 500 wanatarajiwa kuhusika katika mchakato huu.
6) Ukocha Unaoendelea kutoka kwa Mshauri wa Ubora wa Tafsiri: Mfululizo wa zana za mtandaoni na zisizo za mtandaoni hutumika kusaidia kuhakikisha usahihi, uwazi, ulaini wa lugha na kukubalika kwa Maandiko. Katika mchakato wote wa ukaguzi kila mratibu wa lugha anayeongoza timu ya tafsiri anaweza mara kwa mara kuwafikia Walezi wa Tafsiri wa muda wote ambao, kwa upande wao, wanaweza kuwafikia kwa mbali washauri wa ubora wa tafsiri.
7) Tathmini ya Uongozi wa Makanisa ya Harakati: Baada ya maandiko kupimwa, kutathminiwa, kuhaririwa na kukaguliwa na mtandao wa makanisa ya mahali na jamii, na kuidhinishwa na Walezi wa Tafsiri, rasimu hupelekwa kwa ajili ya tathmini ya mwisho na uongozi mpana zaidi wa makanisa katika CPM.
Athari ya Maandiko
A) Kujitoa kwa kukamilisha, kusambaza na kutumia Maandiko ni muhimu sana.
B) Uwezo: Kipaumbele hupewa CPM kwa sababu zina ukomavu na uwezo mkubwa zaidi wa kukamilisha tafsiri na kuitumia kwa ufanisi.
C) Kuunganisha: Ni wazi kwamba kuzalisha tafsiri inayoweza kuwa daraja la kusaidia tafsiri katika lugha nyingine zinazohusiana au lahaja kuu kutaongeza uwezekano wa Athari ya Maandiko.
D) Ufuasi wa Timu ya Tafsiri: Athari ya mwanzo ya Maandiko huanza kutokea kwa wale walio katika timu ya tafsiri wanapojifunza na kulitumia Neno la Mungu kwa kina zaidi katika maisha yao.
E) Ufuasi: Njia ya pili ya athari ya Maandiko ni katika maisha ya waamini wanaosaidia katika hatua hii, ambao ufahamu wao na utendaji wao wa Maandiko huzidi kuwa wa kina kwa kujaribu na kutumia mafungu ya Biblia katika michakato ya ufuasi.
F) Uinjilisti: Njia ya tatu ya athari ya Maandiko huja kwa kuwaomba wasioamini wa mahali hapo kusaidia kukagua kama mafungu haya yaliyotafsiriwa yanaeleweka. Hii ni njia yenye ufanisi ya kushiriki Injili na familia na marafiki. Mara nyingi ni wakati huu wa kuwaomba wasioamini kushiriki (kwa tahadhari) ndipo moyo wa asiyeamini hulainishwa na kugeuzwa kuelekea Injili. Baadhi humwamini Kristo kwa kusoma tu Neno la Mungu.
G) Usambazaji: Awamu inayofuata ni kusambaza Neno la Mungu kwa ajili ya ufuasi na uinjilisti unaoendelea. Kutegemea hali ya makanisa ya mahali, usambazaji unaweza kufanyika kupitia uchapishaji kwa mahitaji na/au kidijitali kupitia kadi za microSD, vifaa vya sauti, Bluetooth, vifaa vya Wifi vya mahali visivyounganishwa na intaneti kama vile Lightstream, n.k.
H) Kupima Matunda: Tunajua kwamba Neno la Mungu halitarudi bure, kwa hiyo kupima athari katika maisha ni kipengele muhimu sana na kinachopuuzwa mara nyingi katika tafsiri na matumizi ya Maandiko. Kupima ongezeko la idadi (idadi ya makanisa mapya na wanafunzi) na la ubora (vipimo vya ufuasi vya maisha na jamii zilizobadilishwa) ndicho kipande cha mwisho kinachohitajika katika kupima Athari ya Maandiko.
I) Umiliki: Kwa kuhusisha angalau watu mia kadhaa katika kutafsiri na kukagua tafsiri, jamii inakuwa na hisia kubwa ya umiliki ambayo itaongeza tu heshima yao kwa Biblia na matumizi yao ya Biblia.
Kwa kuhitimisha, nyingi ya lugha zilizojumuishwa katika “Hatua ya Mwisho” ya tafsiri ya Biblia zinahusisha baadhi ya magumu na hatari ambazo hatuwezi kuzishinda kwa michakato ya kimapokeo ya tafsiri ambayo Mungu ameitumia kwa ufanisi mkubwa hapo zamani na anaendelea kuitumia leo. Kutoweza kwa watafsiri wa nje kupata kibali cha kuingia pamoja na mateso na hatari zinazotoka kwa wapinzani wa Injili kunamaanisha kwamba Biblia haitatafsiriwa katika lugha hizi isipokuwa tupate njia mpya.
Ni maeneo haya hasa yenye mateso makali ndiyo yanayohitaji zaidi kuliko yote Biblia katika lugha yao wenyewe. Historia ya kanisa inatuambia kwamba Biblia katika lugha ya moyo si lazima kwa uinjilisti na ufuasi wa mwanzo. Hata hivyo, Biblia katika lugha ya moyo ni kigezo kimoja muhimu sana cha kunusurika na kustahimili mateso. Mfano mmoja ni kudumu kwa muda mrefu kwa kanisa nchini Misri na Ethiopia ukilinganisha na kuangamia kwa haraka kwa Kanisa katika Afrika Kaskazini baada ya mashambulizi ya Uislamu. Sababu moja kuu ya hili ni kwamba Misri na Ethiopia zilikuwa na Biblia katika lugha za wenyeji, ilhali kanisa la Afrika Kaskazini lilikuwa na Biblia katika Kilatini iliyozungumzwa na watu wa tabaka la juu pekee.
Mungu hashangazwi na changamoto hizi. Mungu kwa hekima yake ametumia tafsiri zilizopo za Biblia katika lugha za biashara ili kuanza kuzidisha wanafunzi na makanisa katika nyingi ya lugha hizi za “hatua ya mwisho” zisizo na Biblia. Wanafunzi hawa wako ndani ya jamii hizi za lugha na wako tayari kukabiliana na hatari za kutishia maisha katika tafsiri kwa sababu wanatamani kwa kina kuwapatia waamini na waliopotea Biblia katika lugha ya moyo wao wenyewe. Zaidi ya hayo, Mungu ametuwezesha kuishi katika siku ambayo tunaweza kuwaimarisha na kuwasaidia wale wanaohatarisha mengi kwa kuwafunza na kutumia maendeleo ya hivi karibuni ya kiteknolojia kwa ajili ya tafsiri.
Kama ilivyoonekana, mchakato huu wa tafsiri wa hatua saba si tu unahakikisha tafsiri bora bali pia unahakikisha athari ya Maandiko wakati wa mchakato wa tafsiri na baada yake. Tunapoona jinsi ambavyo Roho Mtakatifu tayari ameutumia mchakato huu, tunaweza kuamini na kufanya kazi na kuomba ili kuona tafsiri nyingi zaidi zikifanyika hadi katika kizazi chetu kusiwe tena na lugha zisizo na Biblia. Mungu anatupa fursa ya kuona ulimwengu ukijaa utukufu wa Mungu, lakini ni siku inayotupa changamoto ya kumwamini na kumtegemea yeye kuliko wakati mwingine wowote!
Ilichapishwa katika Mission Frontiers 43:5 (Sep./Okt. 2021), uk. 40-43. Frontier Ventures. Imechapishwa tena kwa ruhusa kutoka toleo la Julai 2020 la Accel, Juzuu 1, Na. 6, kurasa 3-5. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


