KABLA SIJAHAMIA NCHI YENYE WAISLAMU WALIO WENGI (zaidi ya miongo miwili iliyopita), nilikuwa katika wafanyakazi wa kichungaji wa kanisa moja katika eneo la vijijini la kaskazini mwa jimbo la New York. Nilizifahamu familia chache zilizofanya kile walichokiita “kanisa la nyumbani”. Familia hizi zilikuwa zimehudhuria kanisa letu kwa muda, kisha zikaondoka. Pia zilikuwa zimeyaacha yaliyo mengi au yote ya makanisa mengine yanayohubiri Injili yaliyo ndani ya mwendo wa takriban dakika 30 kwa gari. Hakuna kanisa lililokuwepo lililokuwa sahihi kimafundisho vya kutosha au lililojaa Roho vya kutosha au jambo jingine vya kutosha kwa ladha yao. Kwa hiyo waliabudu wenyewe nyumbani na kuliita kanisa la nyumbani. Kwa ufahamu wangu, “makanisa hayo ya nyumbani” yaliwaleta wengine wachache, kama wapo kabisa, kwenye imani inayookoa (isipokuwa baadhi ya watoto wao wa kuzaa) na hayakuwahi kuleta athari kubwa katika jamii. Maono yao hayakufika mbali zaidi ya kuwa “wa kibiblia zaidi” kuliko makanisa waliyokuwa wameyaacha hivi karibuni. Walionekana kuwa kielelezo cha roho ya kujitegemea ya kishamba ya eneo hilo. Sikuvutiwa nao.
Katika mwaka uliopita nimehariri makumi ya mifano ya Harakati za Kupanda Makanisa miongoni mwa makundi ya watu wasiofikiwa. Sehemu kubwa kabisa ya harakati hizi zinakua kupitia kuzaana kwa kasi kwa aina fulani ya makanisa ya nyumbani, yaani ushirika mdogo kiasi unaoongozwa na waamini wasiowekwa wakfu rasmi, unaotimiza yaliyo mengi au yote ya mambo yaliyoelezwa katika makala kama “Generational Mapping: Tracking Elements of Church Formation Within CPMs”. Baada ya kuuliza na kupokea majibu ya maswali yangu kuhusu uthabiti wa mafundisho, ukomavu wa kiroho na uendelevu, nimefikia kuyaona makanisa ya nyumbani kama haya kwa mtazamo mzuri zaidi sana kuliko mikusanyiko ya kifamilia ya watu waliozoea kuacha makanisa niliowafahamu hapo awali nchini Marekani. Makanisa haya ya nyumbani yana uhai na yanazaana daima kadiri yanavyowafikia wasioamini wanaoyazunguka. Makanisa rahisi yanayounda Harakati za Kupanda Makanisa zilizo nyingi huwezesha kuenea kwa kasi kwa Ufalme kunakozitambulisha harakati hizi, mwenendo unaofanana na kile tunachokiona katika Agano Jipya.
Hata hivyo, miongoni mwa mambo mengine, nimegundua dhamira moja inayojitokeza mara nyingi kwa kushangaza katika nyingi ya harakati hizi. Walipoulizwa kuhusu changamoto zinazoikabili harakati yao, wengi wamesema, “Changamoto yetu kubwa zaidi inatoka kwa Wakristo wengine”. Hivi karibuni nilihariri mfano mmoja kutoka Asia uliosema: “Ingawa nchi hii kwa ujumla ina uadui dhidi ya Injili, tuligundua kwamba shida kubwa zaidi, kwa mbali kabisa, ilitoka kwa viongozi wa Kikristo wa kimapokeo. Walisababisha mkanganyiko mwingi katika makanisa mapya kwa kuwa mara kwa mara walipinga mawazo kwamba mwanafunzi yeyote anaweza kumfanya mwanafunzi mwingine, anaweza kumbatiza mwanafunzi mwingine na/au anaweza kuhudumia Meza ya Bwana. Tangu mwanzo wa kazi hii hadi sasa, Wakristo wa kimapokeo wamekuwa, kwa mbali kabisa, tatizo kubwa zaidi ambalo harakati imekabiliana nalo”. Ni jambo la kusikitisha na la kushangaza kiasi gani kwamba wakati mamilioni ya watu waliopotea wanakuja kwenye imani inayookoa na ushirika na Mungu Aliye Hai, kizuizi kikubwa zaidi kinatoka kwa Wakristo wengine!
Ninaweka kando shaka ya nia za ubinafsi kama vile kuiba kondoo ili kutoa taarifa kubwa zaidi za ukuaji wa kanisa au kuleta michango zaidi. Ninaweka kando shaka ya kujisifu kidini: kutamani huduma kubwa zaidi ili kuonekana na kujisikia wa kuvutia zaidi. Natumaini sote tunakubaliana kwamba nia kama hizo (ziwe zimefichika au ziko wazi) zinapingana na Injili na mapenzi ya Kristo ambaye jina lake tunalidai. Kujenga huduma kwa viambato hivyo ni sawa na mti, nyasi na majani yaliyokusudiwa kuharibiwa na moto mtakatifu wa Mungu (1 Wakorintho 3:10-15).
Ninathamini hangaiko la waamini wapya kuingia katika ushirika wenye mafundisho thabiti ya kibiblia na uchungaji wa kutosha. Hata hivyo Ufalme wa Kristo unaposonga mbele kwa nguvu miongoni mwa wale ambao hawajawahi kumjua hapo awali, inaonekana ni kinyume na lengo kuvuruga mchakato huo kwa msingi wa masuala ya pili kwa umuhimu, kama vile mambo ya utaratibu wa kanisa na masuala ya kuwekwa wakfu. Mfano wa karibu zaidi wa kibiblia unaonijia akilini ni mwitikio wa Mafarisayo kwa Yesu kumponya mtu siku ya Sabato (k.m. Luka 6:6-11; 13:10-17). Huko tunaona tofauti kubwa kati ya madhihirisho yenye nguvu ya Ufalme na ukosoaji unaotokana na dini. Injili zote nne zinaonyesha wazi msimamo thabiti wa Yesu kuhusu mambo hayo.
Usomaji wangu mwenyewe wa Agano Jipya haupati kifungu chochote kinachotaka kwamba ubatizo na/au Meza ya Bwana vihudumiwe tu na mchungaji aliyewekwa wakfu. Ninaielewa mifuatano ya hoja yenye busara na yenye msingi wa Biblia inayoeleza umuhimu wa usimamizi wa kichungaji kwa ajili ya sakramenti hizi. Hata hivyo maelezo haya daima yanaonekana kuwa angalau hatua moja mbali na amri au mifano halisi ya kibiblia. Swali moja muhimu sana lingekuwa matumizi ambayo Bwana alikusudia ya Agizo Kuu (“wafanyeni mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza na kuwafundisha kutii…” Mathayo 28:19-20). Je, hilo lilikuwa kwa ajili ya mitume wa kwanza tu? Nadhani Wakristo wa kiinjili walio wengi wangesema sivyo. Je, basi, ni kwa ajili ya wachungaji waliowekwa wakfu tu? Sikumbuki kuwahi kusikia mtu yeyote akitoa dai hilo. Je, linawahusu wafuasi wote wa Yesu? Ikiwa ndivyo, ukuhani wa waamini wote (1 Petro 2:5-9) ungeonekana kuenea hadi kwenye kuwabatiza wanafunzi wapya.
Kwa namna hiyo hiyo, wengine wanapinga Neno la Mungu kufundishwa na kutumiwa na mtu mwingine yeyote asiye mchungaji aliyewekwa wakfu hadharani. Hili linaonekana zaidi kuwa mwendelezo wa ukasisi wa Kanisa Katoliki la Roma kuliko jambo lolote linalopendekezwa katika Agano Jipya. Kuweka mipaka ya kuhubiri kwa makasisi waliosomea theolojia kunabana sana uwezekano wa kuzidisha makanisa na kuwafikia wasiofikiwa. Cha kushangaza, hoja ambayo mara nyingi huwasilishwa kwa nguvu zaidi kuhusu ulazima wa makasisi waliosomea theolojia (ili kuzuia mafundisho ya uongo) inageuka kuwa isiyo na msingi. Kuenea kwa theolojia huria na kuangamizwa kwa makanisa makuu ya kihistoria katika ulimwengu wa Magharibi kulikuja kwa kiasi kikubwa kupitia elimu ya juu ya theolojia, badala ya kuzuiwa nayo.
Katika dhehebu nililokulia, mara nyingi nilisikia maoni ya kusikitisha kuhusu vijana waliokwenda seminari wakiwa na shauku kuhusu Yesu na Biblia, na kuhitimu wakiwa hawaamini sana yoyote kati ya hivyo viwili. Nadhani elimu ya theolojia ina thamani kubwa, lakini siikubali hoja kwamba inazuia theolojia mbaya au inahakikisha mafundisho thabiti na yenye kujenga. Uzushi mkubwa unaonekana kutokea mara nyingi zaidi sana kutoka kwa mhubiri/mwalimu mwenye kipaji na mvuto ambaye wafuasi wake hushikilia kila neno lake, kuliko kutoka kwa vikundi vidogo vya waamini wanaojifunza Biblia kwa njia ya kiuchunguzi na kuishi matumizi wanayohisi Roho anawapa kwa ajili ya maisha yao. Fikiria si Umormoni na Watchtower Society tu, bali pia uzushi uliopewa majina ya waanzilishi wake, kama vile Usabelio, Uariani, na Uapolinari. Mafunzo ya Biblia ya vikundi vidogo yenye matumizi ya maisha yanayowajibishwa yanaweza kukosa baadhi ya undani wa kanuni za ufasiri, lakini kwa ujumla yana hatari ndogo zaidi ya kitheolojia kuliko mawasiliano ya upande mmoja yaliyong’arishwa kwa umati mkubwa unaostaajabia.
Katika karne ya kumi na nane, wahubiri walei wa John Wesley waliikwaza taasisi ya kidini na pia kuleta wokovu kwa idadi kubwa sana ya watu ambao vinginevyo wasingesikia kamwe. Uwajibikaji usiotetereka wa “mikutano ya madarasa” ya vikundi vyake vidogo uliimarisha matunda ya wahubiri hao kuwa ushirika wa wanafunzi wanaokua. Hata hivyo zaidi ya karne mbili za juhudi za bidii za wahubiri “walei” pamoja na wahubiri waliowekwa wakfu bado zimetuacha mbali sana na lengo la “kuyafanya mataifa yote kuwa wanafunzi”. Itakuwaje tukigundua (kama inavyoonekana kuwa hivyo) kwamba vikundi vidogo vinavyojifunza Biblia kwa njia ya kiuchunguzi vinaweza kuuelewa ujumbe wa Mungu vya kutosha ili kuwa na mizizi na kuimarishwa katika Kristo? Itakuwaje ikiwa uwajibikaji wao wa pamoja unaongoza kwenye mitindo ya maisha ya utii na uinjilisti wenye ufanisi kwa wasiofikiwa? Itakuwaje ikiwa Roho wa Mungu anaweza kuwaongoza watu wake katika kweli yote ya msingi na kuinua vizazi vya viongozi kupitia ufuasi wa maisha kwa maisha na mafunzo kazini yanayotolewa na waamini waliokomaa zaidi katika imani? Ninapendekeza tufanye lolote tuwezalo ili kuhimiza harakati kama hizo za imani ya kibiblia inayosonga mbele. Hili lingejumuisha kutojaribu kuvuta ushirika wa nyumbani unaozaana kuelekea muundo wa dhehebu letu wenyewe au ladha yetu ya huduma.
Nilipojaribu kuelewa mahangaiko ya wapinzani kuhusu uhalali wa makanisa rahisi/ya nyumbani, masuala hayo kwa kawaida yanaonekana kujumlika kuwa moja au zaidi ya yafuatayo:
- Watu hawabatizwi na mtu aliyewekwa wakfu.
- Meza ya Bwana haihudumiwi wala kusimamiwa na mtu aliyewekwa wakfu.
- Ushirika unaongozwa na mtu asiye na elimu rasmi ya theolojia.
- Kikundi hakijasajiliwa wala kutambuliwa na serikali ya kitaifa.
- Kikundi hakihusiani na dhehebu lolote la Kikristo linalotambulika.
- Kikundi hakina tamko rasmi la imani lililoandikwa.
Sioni Agano Jipya likiwasilisha lolote kati ya haya kama kipengele cha lazima cha kanisa linalompendeza Mungu. Kwa mtazamo wa Agano Jipya, yanaonekana kuwa bora kuyatazama kama “adiaphora”- matendo ambayo hayaamriwi wala hayakatazwi. (Kwa maelezo zaidi, tazama makala yangu “What is Church? From Surveying Scripture to Applying in Culture” katika EMQ Oktoba 2011.) Silikosoi kanisa lililo na au linalotekeleza lolote kati ya mambo haya. Lakini ninaamini Yesu anasimama kwa nguvu dhidi ya wale ambao “mafundisho yao ni kanuni za wanadamu tu” (Mathayo 15:9), na wanaotumia kanuni kama hizo kuwapinga waamini wengine, hivyo kuzuia kuenea kwa Ufalme wake. Je, tunaweza kukubaliana kwamba Mungu anakusudia tutumie mafundisho ya Agano Jipya kama kiwango cha kanisa lake? Je, tunaweza kuacha kushambuliana, kukosoana au kuibiana kondoo kwa msingi wa mitindo ya ziada ambayo kikundi chetu wenyewe kinaamini itakuwa nyongeza yenye msaada? Huenda hilo ni wazo kali. Lakini kanisa rahisi linapoweza kutimiza makusudi ya Mungu kwa ufanisi, kwa nini isiwe rahisi?
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 40:2 (Mac./Apr. 2018). Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


