Mara Tano
Walipokuwa wakitembelea makanisa katika sehemu ya pembezoni ya nchi nyingine, silika ya ukarimu ya Mike na Rebecca iliamka. “Lazima tutafute njia ya kuyasaidia makanisa haya,” walitangaza. Kabla ya kurudi Marekani, waliamua kutoa dola 100 kwa kila moja ya makanisa matatu katika eneo hilo ili yatumie kwa hitaji lao la dharura zaidi. Mike na Rebecca walitafsiri shukrani ya bashasha ya wapokeaji kama ishara kwamba fedha hizo zilikuwa msaada mkubwa. Walihakikisha makanisa yanajua kwamba walikuwa na hamu kubwa ya kushirikiana nayo.
Walipokuwa nyumbani, Mike na Rebecca walikusanya vifaa vya zamani vya shule ya Jumapili ya watoto kutoka makanisa mbalimbali katika jiji lao na kuvituma kwa makanisa matatu ambayo walikuwa wameanzisha ushirikiano nayo.
Miezi sita baadaye, Mike na Rebecca walipanga safari nyingine ya kuyatembelea makanisa yaliyokuwa yameiteka mioyo yao kiasi hicho. Wakati huu timu ndogo ya wafanyakazi wa ujenzi iliungana na Mike na Rebecca. Walitumia muda wao huko kukarabati majengo ya kanisa yaliyokuwa yamechakaa.
Matarajio ya hamu ya makanisa yaliongezeka kila mara waliposikia kwamba Mike na Rebecca walikuwa wanakuja kwa ziara nyingine. Swali lisilotamkwa mara nyingi lilipepea akilini mwa waamini wa mahali hapo: Wakati huu watatusaidia na nini?
Wiki mbili kabla ya ziara iliyofuata ya Mike na Rebecca, mojawapo ya makanisa liliwatumia barua pepe kwa moyo wa kutarajia. Barua pepe hiyo ilikuwa na ombi lifuatalo: “Je, mngekuwa tayari kutuletea gitaa, kama lile analopiga Mike anapokuwa hapa? Pia, tumekuwa tukifikiri kwamba tunahitaji kujenga mahali pa mchungaji kuishi kwenye eneo la kanisa. Hili lingefanya kazi yetu ya kichungaji iwe na ufanisi zaidi kwa ajili ya Yesu na ninyi mngeweza kukaa hapo mnapokuja.” Mike na Rebecca walisaidia kutimiza ombi hili lililoonekana kuwa la busara.
Katika ziara iliyofuata ya Mike na Rebecca, mwanamume mmoja aliyehudhuria mojawapo ya makanisa ya mahali hapo alimwomba Mike fedha za kuwapeleka watoto wake shuleni. Mtu huyo alionekana wazi kukatishwa tamaa Mike alipomwambia kwamba alihitaji kulifikiria. Hii ilikuwa mara ya kwanza Mike kujiuliza kama huenda walikuwa wameanzisha jambo ambalo hawakulikusudia kupitia utoaji wao wenye nia njema. Shukrani waliyoipata mwanzoni ilionekana kugeuka kuwa hisia ya kustahili. Kwa wakati huo, Mike aliliweka kando wazo hilo lililokuwa likimsumbua.

Kadiri Mike na Rebecca walivyowasaidia watu wa huko, ndivyo mahusiano yalivyozidi kuwa magumu. Baada ya miaka miwili ya kuyasaidia makanisa haya matatu, Mike na Rebecca walitambua kwamba huenda walikuwa wamejenga utegemezi.
Hadithi hii ya kubuni lakini halisi sana inaonyesha kwamba hakuhitajiki zaidi ya mara tano za ruzuku ya kigeni ya upande mmoja ili kujenga utegemezi usiofaa.1
Siku Tisini
Hii ni habari mbaya ikiwa mazoea hayo si mazuri na habari njema ikiwa mazoea hayo ni mazuri. Kwa mfano, ukigharamia mara kwa mara juhudi za huduma za siku 90 kwa niaba ya kanisa katika nchi nyingine, itakuwa mazoea ya kudumu ya mtindo wa maisha kwa kanisa hilo kutazama nje ya kusanyiko lao kwa ajili ya rasilimali za kuendesha huduma walizopewa na Mungu. Kwa upande mwingine, ukilihimiza kanisa hilo hilo kuhamasisha rasilimali za mahali hapo kwa huduma zao wenyewe za siku 90, itakuwa mazoea ya kudumu ya mtindo wa maisha kwa kanisa hilo kuhamasisha rasilimali zao wenyewe kwa ajili ya juhudi zao wenyewe za huduma. Ni juu yetu kuifanya kanuni ya 21/90 ifanye kazi kwa manufaa ya kujenga utamaduni wa heshima, uendelevu, kuzidisha, na harakati, badala ya kufanya kazi dhidi yake.
Kizazi Kimoja
Saranya Kapur aliandika makala ya mtandaoni katika Business Insider iitwayo “Parents on Welfare Are Bequeathing a Culture of Welfare unto Their Children.”2 Katika makala hii, Kapur anaandika kuhusu utafiti uliotolewa na National Bureau of Economic Research (NBER) yenye makao yake Marekani. Utafiti wa NBER unaonyesha kwamba wazazi wanaotegemea misaada ya ustawi wa jamii hujenga utamaduni wa kutegemea misaada kwa watoto wao. Kapur anaendelea kueleza kwamba kuna sababu kuu tatu kwa nini hili hutokea:
- Wazazi wanaotegemea misaada huwapa watoto wao wanaokua habari daima kuhusu programu zote za misaada zinazopatikana.
- Wazazi hupunguza unyanyapaa wa kushiriki katika programu hizi za ruzuku.
- Wazazi hawawekezi katika kujiendeleza kwa familia yao wenyewe.
Hatimaye, utafiti unaonyesha kwamba mara nyingi zaidi wazazi kutegemea misaada ndicho chanzo kikuu cha watoto wao kutegemea misaada, badala ya sababu nyingine halali inayohusiana.
Vivyo hivyo, kizazi cha kwanza cha makanisa kutegemea msaada wa nje ndicho chanzo kikuu cha kizazi kinachofuata cha makanisa kutegemea msaada wa nje, badala ya sababu nyingine halali inayohusiana. Kwa maneno mengine, makanisa yanayokuzwa katika utamaduni wa kikanisa wa kutegemea misaada yanarithisha utamaduni wa kikanisa wa kutegemea misaada kwa kizazi kinachofuata cha makanisa:

Inahitaji mara tano za utoaji wa upande mmoja ili kujenga utegemezi. Inahitaji siku 90 ili kukuza mazoea ya kudumu ya mtindo wa maisha yanayoambatana na kuwategemea wengine. Inahitaji kizazi kimoja tu cha familia na makanisa yaliyozama katika utamaduni wa kikanisa wa kutegemea misaada ili kuurithisha kwa kizazi kinachofuata cha familia na makanisa.
Hiyo ni habari ya kuvunja moyo. Huu hapa ndio uzuri badala ya majivu. Yoyote kati ya kanuni hizi inaweza kufanya kazi kwa faida yetu kwa matokeo chanya.
Ni nini kingetokea kama ungewawezesha kikundi cha wanafunzi kutoa na kushiriki rasilimali za mahali hapo kwa ajili ya jambo lililo karibu na mioyo yao mara tano, au kwa siku 90, au kwa kizazi cha kwanza cha wanafunzi? Ungejenga kutegemeana kwa wenyeji wenyewe kwa wenyewe, kuunda mazoea ya kudumu ya mtindo wa maisha na kukirithisha kizazi kinachofuata cha wanafunzi shauku na uwezo wa kutoa na kushiriki rasilimali zao.

Kinachovutia kuhusu hili ni kwamba lazima tuanze na sisi wenyewe. Tukichagua kuifanya kuwa lengo na mazoea yetu kutumia rasilimali za mahali hapo kuunda kile tunachohitaji kwa siku 90, hili litakuwa mazoea yetu ya kudumu ya kiutume. Zaidi ya kukuza mazoea ya kiutume yenye afya kwa ajili yetu, tunajikuta tukiwavuvia na kuwaonyesha mfano wa uwezo wa kuzaa tena na kuzidisha kwa hiari wengine walio katika eneo letu la ushawishi. Kwa maneno mengine, uwezo wa kuzaa tena utakuwa thamani yetu na mazoea yetu na wengine wataiga.
Inahitaji mara tano tu za utoaji usio wa busara na huduma za bure ili kujenga utegemezi. Hutujia kwa kunyemelea haraka sana. Lakini, tukiamua kutumia kanuni ya 21/90 kwa maana chanya, tunaweza kurithisha heshima, kujitegemea, imani, ubunifu, azimio, na mengi zaidi kwa vizazi vya wanafunzi na makanisa yanayozaana. Na iwe hivyo!
Maelezo
- Robert Lupton, Toxic Charity (New York, NY: Harper One 2011), 130. Rudi kwenye maandishi
- Saranya Kapur, “Parents on Welfare Are Bequeathing a Culture of Welfare unto Their Children,” Business Insider. http://www.businessinsider.com/children-of-parents-on-welfare-are-more-likely-to-be-on-welfare-2013–11. Rudi kwenye maandishi
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 43:3 (Mei/Juni 2021), uk. 13-15. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


