LUKA ANAANZA KITABU CHA Matendo ya Mitume kwa kutuambia kwamba kile ambacho Yesu alianza kufanya na kufundisha, sasa anaendelea kukifanya kupitia wanafunzi wake waliowezeshwa na Roho Mtakatifu.
Kisa cha Luka cha kanisa la kwanza ni kisa cha Neno lenye nguvu la Injili linalokua, kuenea, na kuongezeka, likileta wanafunzi wapya na makanisa mapya. Tunafika mwisho wa kitabu cha Matendo na bado kisa hakiishi. Paulo yuko kizuizini nyumbani akisubiri kesi yake; wakati huo huo Neno lisilozuilika linaendelea kuenea kote ulimwenguni. Maana ya Luka iko wazi: kisa kinaendelea kupitia wasomaji wake walio na Neno, Roho na agizo la kufanya wanafunzi na kupanda makanisa.
Katika historia yote ya kanisa tunaona mtindo huu ukiendelea: Neno likienea kupitia watu wa kawaida, wanafunzi na makanisa yakizaana. Wakati Dola la Kirumi lilipokuwa likiporomoka, Mungu alikuwa akimwita kijana mmoja aitwaye Patrick. Aliishi katika Uingereza ya Kirumi lakini alitekwa nyara na kuuzwa utumwani na wavamizi wa Kiayalandi. Akiwa peke yake na katika hali ya kukata tamaa alimlilia Mungu, naye akamwokoa. Baadaye aliunda harakati ya umisionari ya Kiselti iliyohusika kuinjilisha na kupanda takriban makanisa 700 kote Ayalandi kwanza na kisha sehemu kubwa ya Ulaya katika karne kadhaa zilizofuata.
Miaka mia mbili baada ya Matengenezo ya Kanisa, Waprotestanti bado hawakuwa na mpango wala mkakati wa kuipeleka Injili hadi miisho ya dunia. Hali ilikuwa hivyo hadi Mungu alipomtumia kijana mmoja wa kabaila wa Kisaksoni kubadilisha kikundi cha wakimbizi wa kidini waliokuwa wakigombana. Mwaka 1722 Count Nikolaus Zinzendorf alifungua shamba lake kubwa kwa wapinzani wa kidini walioteswa. Kupitia uongozi wake unaofanana na wa Kristo na nguvu za Roho Mtakatifu, walibadilishwa kuwa harakati ya kwanza ya umisionari ya Kiprotestanti, inayojulikana kama Wamoravia.
Leonard Dober na David Nitschmann walikuwa wamisionari wa kwanza kutumwa na Wamoravia. Wakawa waanzilishi wa harakati ya Kikristo miongoni mwa watumwa wa West Indies. Kwa miaka 50 iliyofuata Wamoravia walifanya kazi peke yao, kabla mmisionari mwingine yeyote wa Kikristo hajafika. Kufikia wakati huo Wamoravia walikuwa wamewabatiza waamini wapya 13,000 na kupanda makanisa katika visiwa vya St. Thomas, St. Croix, Jamaika, Antigua, Barbados, na St. Kitts.
Ndani ya miaka ishirini wamisionari wa Kimoravia walikuwa katika eneo la Aktiki miongoni mwa Wainuit, kusini mwa Afrika, miongoni mwa Wenyeji Asilia wa Amerika Kaskazini, na katika Suriname, Ceylon, China, India, na Uajemi. Katika miaka 150 iliyofuata, Wamoravia zaidi ya 2,000 walijitolea kuhudumu ng’ambo. Walikwenda katika maeneo ya mbali zaidi, yasiyofaa zaidi, na yaliyosahaulika zaidi. Hili lilikuwa jambo jipya katika upanuzi wa Ukristo: jumuiya nzima ya Kikristo—familia pamoja na wasio na wenzi—iliyojitoa kwa umisheni wa ulimwengu.
Vita vya Uhuru wa Marekani vilipozuka mwaka 1776, wachungaji walio wengi wa Kimethodisti wa Kiingereza walirudi nyumbani. Waliwaacha nyuma washiriki mia sita na mmisionari kijana Mwingereza aitwaye Francis Asbury aliyekuwa mwanafunzi wa John Wesley.
Asbury alikuwa ameacha shule kabla ya kutimiza miaka kumi na miwili ili kuwa mwanagenzi wa mhunzi. Ufahamu wake wa mfano, mbinu na mafundisho ya Wesley ulimwezesha kuyarekebisha ili yaendane na uwanja mpya wa umisheni huku akibaki mwaminifu kwa kanuni.
Umethodisti haukunusurika tu katika Vita vya Mapinduzi, bali ulienea kote nchini. Umethodisti chini ya Asbury uliyapita madhehebu yenye nguvu zaidi na yaliyoimarika zaidi. Mwaka 1775 Wamethodisti walikuwa asilimia 2.5 tu ya jumla ya washiriki wa makanisa nchini Amerika. Kufikia 1850 sehemu yao ilikuwa imepanda hadi asilimia 34. Hii ilikuwa wakati ambapo masharti ya Wamethodisti ya kuwa mshiriki yalikuwa makali zaidi sana kuliko ya madhehebu mengine.
Umethodisti ulikuwa harakati. Waliamini kwamba Injili ilikuwa nguvu hai iliyokuwa ulimwenguni ikileta wokovu. Waliamini kwamba Mungu alikuwepo kwa nguvu na kwa namna binafsi katika maisha ya kila mwanafunzi, wakiwemo Wamarekani Weusi na wanawake, si makasisi tu. Pia waliamini kwamba ulikuwa wajibu wao na kipaumbele chao kuwafikia watu waliopotea na kupanda makanisa kote nchini.
Umethodisti wa Marekani ulinufaika sana na kazi ya kianzilishi ya John Wesley na Wamethodisti wa Kiingereza. Akiwa huru kutoka kwa vizuizi vya jamii ya kimapokeo ya Kiingereza, Asbury aligundua kwamba harakati ya Kimethodisti ilijisikia nyumbani zaidi hata katika ulimwengu wa fursa na uhuru.
Harakati ilipoenea kupitia kazi ya wahubiri vijana wasafiri, Umethodisti ulidumisha mshikamano wake kupitia mfumo wa jumuiya uliofafanuliwa vizuri. Wamethodisti walibaki wameunganika wao kwa wao kupitia mzunguko wa mikutano ya madarasa, karamu za upendo, mikutano ya kila robo mwaka na mikutano ya kambi. Kufikia 1811 kulikuwa na mikutano ya kambi 400-500 iliyofanyika kila mwaka, ikiwa na jumla ya mahudhurio ya zaidi ya milioni moja.
Asbury alipofariki mwaka 1816 kulikuwa na Wamethodisti 200,000. Kufikia 1850 kulikuwa na Wamethodisti milioni moja wakiongozwa na wahubiri wasafiri 4,000 na wahubiri wa mahali 8,000. Shirika pekee lililokuwa limeenea zaidi lilikuwa serikali ya Marekani.
Hatimaye Umethodisti ulipoteza shauku yake na kutulia ili kufurahia mafanikio yake. Katika mchakato huo ulizaa harakati ya Utakatifu. William Seymour alikuwa mhubiri wa harakati ya utakatifu aliyekuwa na tamaa kubwa ya kuzijua nguvu za Mungu. Alikuwa mwana wa watumwa wa zamani, mlinzi-msafishaji wa jengo, na kipofu wa jicho moja. Mungu alimchagua mtu huyu asiyetarajiwa ili kuwasha harakati iliyoanza mwaka 1906 katika jengo la Kimethodisti lisilotumika tena katika Mtaa wa Azusa.
Mikutano hiyo iliyojaa hisia iliendelea mchana kutwa hadi usiku. Mikutano haikuwa na uratibu wa kati, na mara chache sana Seymour alihubiri. Aliwafundisha watu kumlilia Mungu kwa ajili ya utakaso, ujazo wa Roho Mtakatifu, na uponyaji wa kiungu.
Mara moja, wamisionari walienea kutoka Mtaa wa Azusa kwenda ulimwenguni. Ndani ya miaka miwili walikuwa wameupeleka Upentekoste katika sehemu za Asia, Amerika ya Kusini, Mashariki ya Kati, na Afrika. Walikuwa maskini, wasio na mafunzo, na wasiojiandaa. Wengi walifia uwandani. Dhabihu zao zilipata thawabu; harakati za Kipentekoste/za karismatiki na zinazohusiana nazo zikawa sura ya Ukristo wa ulimwengu inayokua kwa kasi zaidi na yenye utofauti mkubwa zaidi ulimwenguni.
Kwa kasi ya sasa ya ukuaji, kutakuwa na Wapentekoste bilioni moja ifikapo 2025, sehemu kubwa yao ikiwa Asia, Afrika, na Amerika ya Kusini. Upentekoste ndiyo harakati inayopanuka kwa kasi zaidi—ya kidini, ya kitamaduni, au ya kisiasa—kuliko zote zilizowahi kuwepo.
Yesu alianzisha harakati ya umisionari yenye agizo la kuipeleka Injili na kuzidisha wanafunzi na makanisa kila mahali. Historia imejaa mifano ya harakati kama zile za kitabu cha Matendo ya Mitume; nimetaja chache tu. Vipengele vitatu muhimu vinahitajika kwa harakati za Yesu: Neno lake lenye nguvu, nguvu za Roho Mtakatifu na wanafunzi wanaotii yale ambayo Yesu ameamuru.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 40:1 (Jan./Feb. 2018), uk. 29-31. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


