Mungu anatenda kazi kwa njia za ajabu miongoni mwa wazungumzaji wa Kibabu wa India Kaskazini, kupitia Harakati ya Kupanda Makanisa (CPM) yenye wanafunzi wa Yesu waliobatizwa zaidi ya milioni 10. Utukufu wa Mungu katika harakati hii unang’aa zaidi hata ukilinganishwa na historia ya eneo hili. Eneo la Wababu nchini India lina rutuba kwa njia nyingi, si katika udongo wake tu.
Hata hivyo eneo la Wababu limeelezwa kuwa mahali pa giza—si na Wakristo tu, bali pia na wasio Wakristo. Mshindi wa Tuzo ya Nobel V.S. Naipaul, baada ya kusafiri katika mashariki mwa Uttar Pradesh, aliandika kitabu kiitwacho An Area of Darkness, kinachoeleza vizuri huzuni na upotovu wa eneo hilo.
Zamani, eneo hili lilikuwa na uadui mkubwa sana dhidi ya Injili, iliyoonekana kuwa ya kigeni. Lilijulikana kama “makaburi ya umisheni wa kisasa.” Ugeni ulipoondolewa, watu walianza kuzipokea Habari Njema.
Lakini Mungu hataki kuwafikia wazungumzaji wa Kibabu peke yao. Mungu alipoanza kututumia kuwafikia watu zaidi ya kundi la Wababu, baadhi ya watu waliuliza, “Kwa nini msiendelee tu kuwafikia Wababu? Kuna mamilioni mengi sana yao! Kwa nini msibaki tu huko hadi kazi hiyo ikamilike?”
Jibu langu la kwanza ni asili ya uanzilishi ya kazi ya Injili. Kufanya kazi ya kitume/ya uanzilishi kunahusisha kutafuta daima maeneo ambapo Habari Njema hazijaota mizizi: kutafuta fursa za kumtangaza Kristo mahali ambapo bado hajulikani. Hiyo ni sababu moja ya sisi kupanua kazi yetu hadi makundi mengine ya lugha.
Pili, lugha hizi mbalimbali zinaingiliana katika matumizi yake, moja na nyingine. Hakuna mstari ulio wazi ambapo matumizi ya lugha moja yanaishia na mengine yanaanza. Pia, mara nyingi waamini huhama kwa sababu ya mahusiano, kama vile kuoa au kuolewa au kupata nafasi ya kazi mahali pengine. Watu walio katika harakati waliposafiri au kuhama, Habari Njema zimeenda pamoja nao.
Baadhi ya watu walirudi na kusema, “Tunamwona Mungu akitenda kazi mahali hapa pengine. Tungependa kuanzisha kazi katika eneo hilo.” Tuliwaambia, “Endeleeni!”
Kwa hiyo walirudi mwaka mmoja baadaye na kusema, “Tumepanda makanisa 15 huko.” Tulishangaa na kubarikiwa, kwa sababu ilitokea kwa njia ya asili. Hakukuwa na ajenda, hakuna maandalizi, wala hakuna fedha. Walipouliza nini kinafuata, tulianza kufanya kazi nao kuwasaidia waamini kujikita katika neno la Mungu na kukomaa haraka.
Tatu, tulianzisha vituo vya mafunzo vilivyopanua kazi, kwa makusudi na bila makusudi (zaidi ni mpango wa Mungu kuliko wetu). Wakati mwingine watu kutoka kundi la lugha la jirani wangekuja kwenye mafunzo kisha kurudi nyumbani na kufanya kazi miongoni mwa watu wao wenyewe.
Sababu ya nne ya upanuzi: wakati mwingine watu wamekuja kwetu na kusema, “Tunahitaji msaada. Mnaweza kuja kutusaidia?” Tunawasaidia na kuwatia moyo kadiri tunavyoweza. Haya ndiyo yamekuwa mambo muhimu katika kuingia maeneo jirani nje ya Wababu.
Kazi ilianza miongoni mwa Wababu mwaka 1994, kisha ikaenea katika lugha na maeneo mengine kumi na mbili hivi. Tunamsifu Mungu kwamba harakati imeenea kwa njia mbalimbali hadi makundi tofauti ya lugha, maeneo tofauti ya kijiografia, makundi mengi ya tabaka (ndani ya maeneo hayo ya lugha na ya kijiografia), na dini tofauti. Nguvu ya Habari Njema inaendelea kuvunja mipaka ya kila aina.
Kazi miongoni mwa watu wa Makarios ni mfano mzuri sana wa ushirikiano. Ushirikiano wetu na kiongozi mmoja muhimu ulikuwa jaribio katika kupanua harakati. Badala ya sisi kufungua ofisi yetu wenyewe yenye wafanyakazi wetu wenyewe, tulitimiza lengo hilohilo kwa njia inayoweza kuzaa tena zaidi.
Ingawa harakati hizi zinaongozwa na wenyeji, tunaendelea kushirikiana pamoja. Hivi karibuni tulianza kuwafundisha viongozi 15+ wa Adelphos katika jimbo la jirani katika huduma kamilifu (jumuishi). Tunapanga kusaidia kuanzisha vituo vya huduma kamilifu katika maeneo matatu tofauti ya Adelphos katika mwaka ujao na kuinua viongozi wengi zaidi wenyeji wa Adelphos. Mshirika wetu muhimu anayefanya kazi miongoni mwa Makarios pia anapanua kazi hadi eneo la Adelphos.
Ilichapishwa tena katika Mission Frontiers 45:1 (Jan./Feb. 2023), uk. 24. Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers, Januari/Februari 2018. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


