WAEFESO 4:11-13 ILINITESA MOYONI!
Ingawa yaelekea Waefeso ilikuwa waraka niliopenda zaidi kuuhubiri na kuufundisha, sehemu hii ilinithibitishia kwamba mafunzo yangu hayakuwa ya kutosha na hata yalikuwa yamepotoshwa. Unawezaje kufanya kitu kwa namna tofauti wakati hicho ndicho pekee ulichowahi kukiona?
Paulo anaandika:
Yeye [Yesu] aliwatoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii, na wengine kuwa wainjilisti, na wengine kuwa wachungaji na walimu, kwa ajili ya kuwaandaa watakatifu kwa kazi ya huduma, hata kuujenga mwili wa Kristo; hadi sote tufikie umoja wa imani, na wa kumjua Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufikia kipimo cha kimo kinachohusika na utimilifu wa Kristo.
(NASB, mpangilio ni wangu, JKK.)
Je, Unawaandaa Watu wa Kawaida?
Mitume ni “waliotumwa” ambao wamepewa agizo la kuleta utamaduni wa Ufalme duniani kama ulivyo mbinguni, hasa katika maeneo ambapo Injili haijawahi kusikika. Hawa ni watenda kazi wa Ufalme walio ncha ya mkuki, wale wanaokwenda kwa mataifa yasiyotoa viza za umisionari.
Manabii huwasilisha maono ya mbinguni hapa duniani. Huwasaidia watu kuwazia “Jamii yetu itaonekanaje mapenzi ya Mungu yatakapofanyika hapa?” Biashara, elimu na burudani vyote vitabadilishwa maono ya Mungu yanapokuwa lengo letu!
Wainjilisti hushirikisha Habari Njema kwa shauku ya Yesu popote wanapoishi, wanapofanya kazi na wanapostarehe. Wakiwa wamejaliwa shauku inayofurika ya kuona kila mtu akimjua na kumpenda Yesu, wale waliojazwa karama hii ya neema hawawezi kujizuia kuzungumza kuhusu upendo wa Mungu kwa kila mtu. Wachungaji/walimu hujenga jumuiya ya kimungu kwa kuwafundisha watu ujuzi wa mahusiano. Hapa “familia” inakuwa picha ya uponyaji kwa maeneo mengi yaliyovunjika katika maisha yetu na mitaa yetu. Ushahidi wa kazi yao utaonekana katika upatanisho na vipaumbele vilivyobadilika.
Lakini Paulo hazingatii hasa “karama hizi za neema” (ziwe ni nne au tano)! Jambo lake kuu ni kwamba karama hizi zote zitumike “kwa ajili ya kuwaandaa watakatifu” zikiwawezesha kufanya kazi ya huduma.
Kusudi la karama hizi za kuandaa ni kuujenga mwili ili wote waakisi tabia ya Yesu na tuonekane, tutende na tusikike kama Baba yetu wa mbinguni!
Tunakuwa wanaume na wanawake wa ukweli na uadilifu. Tunatumia maneno yetu kuwajenga watu badala ya kuwabomoa. Tunafanya kazi badala ya kutafuta njia za mkato na kuwaibia wengine. Tunasamehe kwa uhuru kama tulivyoonja msamaha wa Mungu. Sote tunakuwa watumishi wanaohudumu kwa huruma na kutangaza Ufalme, kama Yesu alivyofanya (Waefeso 4:14-32).
Mitazamo ya Harakati
Ingawa watu wanaofanya kazi kwa mamlaka ya kitume ni wa lazima kabisa ili kufungua njia mpya za umisheni, huduma za kinabii, za kiinjilisti na za kichungaji lazima zifuate haraka ikiwa utamaduni wa Ufalme wa mbinguni utabadilisha kijiji, mji au eneo la jiji. Ili kuona harakati miongoni mwa kundi la watu, karama hizi zote za neema lazima zitumike kuzaa tabia ya Kristo ndani ya kila mwanafunzi, kila familia ya wanafunzi na kila kikundi cha marafiki wanafunzi.
Hata hivyo, mfumo wa Mhubiri/Mwalimu Mahiri ambao umejikita kwa kina sana katika kanisa la Amerika Kaskazini haujinakili kwa urahisi. Unahitaji muda mrefu, elimu ya gharama kubwa na uzoefu unaopatikana polepole, ambavyo huwa kidhibiti mwendo kinachopunguza kasi ya ukuaji hadi kutambaa. Lakini hayo ndiyo yaliyokuwa maisha yangu!
Harakati za Kufanya Wanafunzi (DMM) huzingatia hasa huduma ya kitume. Vinasaba vya msingi vinahusu kuuleta utawala wa Kristo katika uhalisia—hasa mahali ambapo jina lake bado halijasikika. Kuongeza zaidi ya kile ambacho kanisa la Magharibi limekuwa likifanya hakutatuleta kwenye utii unaodaiwa katika Agizo Kuu. Kusema kweli, kuyafanya mataifa yote kuwa wanafunzi halikuwa jambo nililolifikiria. Nilikuwa nimekubali nafasi ndogo mno katika Ufalme—kuwakomaza baadhi ya wale waliokuja kumfuata Yesu, lakini tunawezaje kumfuata ikiwa hatufanyi wanafunzi?
Mtazamo wa Kujinakili
Badiliko la kwanza la mtazamo kwangu lilikuwa kukubali kanuni ya vinasaba kwamba: “Chochote unachofanya lazima kiweze kuzaliwa tena na watu unaowafundisha.” “Je, wanaweza kulinakili hili?” ni swali linalotikisa dunia kujilazimisha kulijibu. Shahada yangu ya Biblia ya miaka minne na shahada zangu mbili za Uzamili zilisisitiza kwamba lazima uwe na Kamusi ya Biblia na Konkodansi (Concordance) angalau, ikiwa utaenda kujifunza Biblia kwa kweli.
Unawezaje kuwaandaa watu kwa huduma ikiwa huwezi kuwafundisha kujilisha wenyewe kiroho? Ingawa ningeweza kudai kwamba wote wangeweza kununua Konkodansi na Kamusi ya Biblia, hapa Marekani, vipi kuhusu watu katika makanisa ambapo kulikuwa na nakala moja tu ya Biblia kwa kanisa zima? Mungu alilipasua sanduku langu wazi kwa kunipeleka Afrika Magharibi miezi michache kabla ya mafunzo ya kwanza ya DMM kufanyika.
Mtazamo wa Kugundua
Kugundua kukawa jibu. Tunawezaje kuwafanya watu wapunguze kasi na kusikiliza kwa kweli kile ambacho Neno linasema? Tunawezaje kuwafanya wajibu maswali ya msingi yanayokwenda mbali kidogo zaidi ya kuelewa usomaji wa jumla, lakini si mbali sana? Majaribio yangu mengi ya mwanzo yalikuwa magumu mno na yalidai teknolojia nyingi mno, lakini lile swali lisilonipa raha liliendelea kurudi akilini mwangu: “Je, wanaweza kulinakili hili?” Kati ya watu sitini niliojaribu kuwafundisha mchakato rahisi wa usomaji wa Biblia wa kiuchunguzi, watano hawakujua kusoma na kuandika. Unawezaje kulifanya Neno na Kugundua kufikika pia kwa wanaojifunza kwa njia simulizi?
Harakati za Kufanya Wanafunzi kwa kweli zinadai vichocheo wanaojifunza kumsikia Mungu na kutumia kile wanachogundua katika maisha yao kwa vitendo halisi—utii unaofaa. Kushika sheria ni kutumia orodha ya kanuni ambazo mtu mwingine anatupa. Utii ni kuitikia maelekezo ya Mungu. Kuuandaa mwili kunatuhitaji kuwa makocha zaidi kuliko wachezaji mahiri. Ukocha mzuri huonyesha kwa mfano imani kubwa ajabu katika Roho Mtakatifu. Unakiri kwamba Mungu huleta matokeo bora kuliko kocha anavyoweza. Unaamini kwamba rasilimali ziko katika mavuno. Nguvu ya kuuendeleza Ufalme itainuka kutoka katika shamba la mavuno la Mungu, ikiwa tutaufanya mwili kuwa wanafunzi ili ufanye wanafunzi kwa mtindo wa Yesu.
Mtazamo wa Ukocha
Mafunzo yanahusisha kujifunza ujuzi. Unampaje ukocha Mtu wa Amani ili awezeshe Kikundi cha Kugundua kinachojumuisha marafiki zake miongoni mwa wazazi wa timu ya soka inayosafiri? Ni maswali gani utakayotumia naye kwa uthabiti hadi awe na ujasiri katika kuwezesha? Ni lini yuko tayari kuwezesha kikundi akiendelea kupewa ukocha? Ni lini anahitaji uwepo wako kwa kiasi kidogo zaidi? Ukocha na mafunzo mazuri hufanya kazi vizuri pamoja, lakini katika ulimwengu wa DMM sehemu kubwa ya mafunzo yetu hufanywa kwa makusudi ili kuwapata wale wachache walio tayari kupewa ukocha. Walio wengi katika Kanisa la Magharibi hawako tayari kupewa ukocha. Hata wale wanaokuwa tayari mara nyingi huhitaji kukutana mara nyingi na kanuni muhimu na uzoefu wa kujaribu michakato ya Kugundua.
Kumpata Mtu wa Amani kunakuwa ndoano kubwa zaidi ya “kutuvuta” sisi ambao “tumenaswa” na fikra za Harakati. “Onjeni mwone...” huenda ukawa mwaliko wa kwanza. Kuona mabadiliko yenye furaha katika maisha ya Mtu wa Amani anayefuata njia ya Kugundua kunalewesha.
Kuwasaidia watu wa kawaida kupata mafanikio ya kuvunja vizuizi katika kufanya wanafunzi hunipa furaha kubwa! Kunazidi sana kuridhika kwa kuwa na Mkristo anayesema wiki baada ya wiki: “Mahubiri mazuri! Sijawahi kuyasikia yakielezwa hivyo hapo awali!”
Kuzidisha Huenda Mahali Ambapo Sisi Hatuwezi
Juhudi zangu za kwanza za kuwafanya wanafunzi wafanya-wanafunzi zilifanyika katika Gereza la Kaunti ya Rutherford lililo maili chache tu kutoka nyumbani kwangu huko Murfreesboro. Ingawa ningeweza kumtembelea mfungwa yeyote mmoja kwa vipindi viwili tu vya dakika 45 kwa wiki, yeye alikuwa akitumia saa 24 kila siku za wiki pamoja na wanaume zaidi ya 50 katika chumba chao cha mahabusu na mara mbili kwa siku, siku saba kwa wiki aliweza kukutana na wanaume kutoka chumba jirani katika chumba cha mazoezi. Kumfundisha kuwezesha usomaji wa kugundua kulitoa uwezo mkubwa zaidi sana wa kuipeleka Injili gerezani. Miaka mitatu baada ya kuachiliwa kwake, nilikuwa nikifanya kazi na mwezeshaji tofauti wa 17 wa usomaji wa kikundi uliokuwa ukiendelea bila kukatika. Marafiki katika Afrika waliposikia kuhusu kikundi hiki, waliweza kupata fursa zaidi hata ya kuingia magerezani na mahabusu. Wengi zaidi walifanywa wanafunzi hadi kufikia imani na kuendelea hadi ukomavu.
Unajua kwamba unatumia mikakati bora zaidi unapogundua kwamba msichana Mchina katika chuo kikuu nchini Marekani anawezesha mchakato wa Kugundua na mama yake huko Mongolia ya Ndani kupitia Skype. Ingawa binti huyo hakuwa mwamini wakati huo, alithamini kile kilichokuwa kikitokea moyoni mwake kiasi cha kukinakili kwa mtu aliyempenda. Hivi karibuni msichana huyo alimwamini Kristo—tunaomba kwamba mama yake naye amwamini. Siwezi kujizuia kujiuliza kama huenda kuna wengine huko China walio karibu na Ufalme pia.
Floyd McClung amesema, “Watu wa kitume hulipeleka kanisa ulimwenguni; hawasubiri ulimwengu uje kanisani.” Tunahitaji watu wa kitume ili kuifikia asilimia kubwa ya Wamarekani ambao hawatakuja makanisani mwetu. Pia tunahitaji watenda kazi wa kinabii, wa kiinjilisti na wa kichungaji wanaoshikana mikono na wa kitume ili kuuandaa mwili ukue hadi kufikia utimilifu wa Kristo!
Je, watu unaowafanya wanafunzi wanaweza kuwafanya wengine kuwa wanafunzi ili wawe wafanya-wanafunzi. Harakati za kufanya wanafunzi ni za vizazi vingi, la sivyo kwa kweli si harakati!
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 39:6 (Nov./Des. 2017), uk. 29-31. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


