CITYTEAM INTERNATIONAL MINISTRIES imekuwa ikichochea Harakati ya Kufanya Wanafunzi (DMM) kwa ushirikiano na Lifeway Mission katika nchi nane za Afrika Mashariki kwa miaka kumi na miwili iliyopita.
Nchi nane ambamo Harakati za Kufanya Wanafunzi zinakua ni Burundi, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Tanzania, Uganda, Sudan Kusini na Sudan.
Katika eneo hili, Bwana ametuwezesha kuanzisha kazi miongoni mwa makundi ya watu 89 na makundi tisa ya watu wa mijini wenye mambo yanayofanana.
Tangu siku tulipoanza safari ya imani ya kufanya wanafunzi miaka 12 iliyopita, tunamstaajabia Mungu kwa ajili ya maelfu ya makanisa mapya ambayo Roho wake ameyazaa, na mamia ya maelfu ya watu ambao wamekuwa wafuasi wa Kristo.
Katika miaka hii 12 Mungu alipenda kutubariki kwa kupanda makanisa 7,571 yenye wanafunzi wapya 185,358. Vizazi kumi na vinne ndicho kiwango kikubwa zaidi cha kuzidisha ambacho tumewahi kuona hadi sasa katika kundi lolote moja la watu.
Ni furaha yetu kushirikisha masimulizi machache ya hivi karibuni ya kile Mungu anachofanya na jinsi alama za vidole vyake zinavyoonekana katika eneo hili— kwa sababu Yeye anastahili utukufu mwingi!
Kwa sababu za kiusalama, tumetumia majina bandia na tumejizuia kufichua maeneo.
Mlevi Anakuwa Mfanya-Wanafunzi
Jarso ni kiongozi wa mkondo ambao umepanda makanisa 63 katika miaka miwili miongoni mwa kundi la watu lisilofikiwa sana katika Afrika Mashariki. Miezi minne iliyopita Jarso alikuwa akiwabatiza wafuasi wapya wa Kristo kutoka kundi hilo la watu. Jillo, ambaye hakuwa mfuasi wa Kristo, alikuwa akitazama kwa mbali wakati Jarso akiendesha ubatizo.
Akiwa na bia mkononi, Jillo alitazama yaliyokuwa yakiendelea na akaanza kufanyia mzaha matayarisho ya ubatizo. Kabla ya kuendesha ubatizo, Jarso alisoma hadithi kuhusu ubatizo wa Yesu na akaanza kuizungumzia. Sasa akiwa katika umbali wa kusikia mahubiri, Jillo alijikuta akizama kwa kina katika kile alichosikia. Mwishoni mwa hadithi, alijua kwamba alihitaji kumfuata Yesu. Mara moja aliamua kuacha kunywa pombe na hata akaitupa chupa ya bia iliyokuwa nusu aliyokuwa ameishika.
Alirudi nyumbani mapema jioni hiyo. Mke wake alishangaa kumwona akiwa hajalewa na mikono mitupu kwa sababu kwa kawaida alileta nyumbani chupa kadhaa za kunywa. Mke wake alijitolea kumletea chupa ya bia aliyokuwa amemnunulia mapema siku hiyo. Jillo alimshtua kwa kumwambia kwamba ameacha kunywa pombe, na kwamba arudishe chupa hiyo dukani na arudishiwe pesa. Jillo, ambaye hakujua kusoma wala kuandika, kisha alimwomba mke wake alete Biblia waliyokuwa nayo nyumbani na amsomee hadithi ya Yesu ambayo Jarso alikuwa ameisoma katika sherehe ya ubatizo. Mke alikuja na Biblia na alipomaliza kusoma hadithi hiyo, Jillo alimshirikisha kile alichosikia kutoka kwa Jarso.
Jioni hiyo, Jillo na mke wake walifanya uamuzi wa kumfuata Yesu. Siku iliyofuata, Jillo aliwasiliana na Jarso ambaye alimwonyesha jinsi ya kufanya Usomaji wa Biblia kwa Kugundua (UBK) wa kifamilia. Kuanzia siku iliyofuata na kuendelea, Jillo na mke wake pamoja na watoto wao walianza kufanya UBK kila jioni.
Wiki mbili baadaye, Jillo, mke wake na baadhi ya majirani waliojiunga na Kikundi chao cha Biblia cha Kugundua walibatizwa. Jillo na mke wake wameendelea na safari hii kwa kuwezesha kuanzishwa kwa vikundi vingine vinane vya kugundua.
Mtu Aliyetilia Shaka DMM Anaanzisha Harakati Imara ya Kufanya Wanafunzi
Agali alitoa mafunzo ya Harakati za Kufanya Wanafunzi kwa kikundi cha wachungaji mwaka 2015. Kati ya wale waliopata mafunzo ya DMM, mchungaji mmoja aitwaye Roba alimjia Agali na kueleza mashaka makubwa kwamba makanisa yaliyopo yangeweza kufanya badiliko la aina hii. Agali hakubishana naye bali alimpa Roba changamoto ya kuanzisha mchakato huo katika jamii yake. Roba aliipokea changamoto hiyo na akaenda katika jamii yake kumtafuta mtu wa amani. Jamii hiyo ilikuwa kwa sehemu kubwa jamii ya Kiislamu ambapo wanaume hupenda kukusanyika katika uwanja wa wazi wakati wa alasiri kunywa chai na kujumuika.
Roba alikwenda kwenye uwanja huo alasiri moja. Aliwasalimu wanaume hao na kujitolea kuwanunulia chai akiwaambia kwamba amekuja ili kuwafahamu. Aliwaambia kwamba ingawa yeye ni Mkristo na wao ni Waislamu, wamekuwa majirani kwa muda mrefu na kama watu wanaomheshimu Mungu huenda wangepaswa kujuana zaidi. Waislamu hao walimkaribisha Roba aketi pamoja nao. Walipokuwa wakizungumza pamoja, Roba alipata fursa ya kuwasimulia hadithi kutoka katika Biblia. Aliwasimulia hadithi ya Zakayo. Wanaume hao walikuwa wakiisikiliza hadithi kwa makini na alipofikia sehemu ya hadithi ambapo Yesu alisema “Leo wokovu umeifikia nyumba hii kwa sababu mtu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu,” wasikilizaji wake walisikiliza kwa makini zaidi jina la Ibrahimu lilipotajwa. Baada ya kumaliza kunywa chai, na walipokuwa wakiagana walimkaribisha mchungaji huyo aje tena na hadithi zaidi.
Siku chache baadaye, Roba alijiunga nao tena kwa chai. Baada ya salamu za kawaida na kuzungumza kuhusu matukio ya sasa katika jamii, Roba aliwauliza kama walikumbuka hadithi aliyowasimulia katika ziara yake ya kwanza. Walimwambia kwamba wanaikumbuka. Aliwaomba wamrudie hadithi hiyo, nao wakafanya hivyo. Baada ya kuirudia hadithi hiyo, majadiliano changamfu yalifuata. Mmoja wao alimwuliza Roba kama anaamini kwamba Yesu ni Mungu. Roba aliwarudishia wanaume hao swali hilo na kuwauliza, “ikiwa Yesu katika hadithi ya Zakayo aliweza kuwapa watu wokovu, je, hili halionyeshi kwamba Yesu angeweza kuwa na sifa za kiungu zisizopatikana kwa wanadamu?” Baadhi ya wanaume hao waliitikia kwa kukubali kwa kutikisa vichwa vyao.
Mikutano hii ya chai ikawa ya mara kwa mara na ya kawaida. Katika kukua kwa kawaida kwa mahusiano hayo, Vikundi vingi vya Biblia vya Kugundua na makanisa vilianzishwa miongoni mwa Waislamu hawa, na kuzaa makanisa madogo 32.
Rahab wa Agano Jipya
Mpanda makanisa wetu, Wario, alikutana na mwanamke kijana miaka miwili iliyopita aitwaye Rahab. Mwanamke huyu alikuwa mrembo sana, na Wario alipokutana naye kwa mara ya kwanza, alikuwa, kama Rahabu wa Biblia aliyebeba jina lake, mfanyabiashara ya ngono.
Wario alianza kumsimulia hadithi ya Rahabu kutoka katika Biblia pamoja na ile inayonukuliwa kumhusu katika Waebrania 11. Alimweleza jinsi maisha ya Rahabu yalivyobadilishwa kutoka maisha ya ukahaba hadi kuwa mwanamke wa imani na jinsi alivyoingia katika ukoo wa Yesu.
Rahab hakuwahi kusoma Biblia yeye mwenyewe. Lakini alijua kwamba katika Biblia kulikuwa na mwanamke aliyeitwa Rahabu na kwamba alikuwa kahaba. Hili alilijua kutoka kwa watu mbalimbali waliosikia jina lake.
Lakini aliposikia kwa mara ya kwanza hadithi kamili ya Rahabu kutoka kwa Wario, aliguswa na akamwuliza Wario kama angeweza kuwa kama Rahabu wa Biblia. Wario alisema “ndiyo” na akajitolea kumwombea. Katika mchakato huo hatimaye aliwekwa huru kutoka katika vifungo vya mapepo. Baada ya hapo maisha yake yalibadilika kwa kiasi kikubwa.
Akawa mfuasi imara sana wa Kristo na mfanya-wanafunzi. Aliolewa na mfuasi wa Kristo na wanandoa hao wakawa wafanya-wanafunzi waliojitoa. Katika mwaka uliopita wamepanda makanisa mapya sita katika jamii yao.
Kiriba Kipya kwa Divai Mpya
Mchungaji Kamau alipoalikwa kuendesha mafunzo ya DMM miongoni mwa kikundi cha wachungaji kutoka wilaya fulani, hakutarajia mengi kutokea. Walikuwa na mashaka kwa sababu watu wa wilaya hiyo walijulikana kuwa Wakristo wa jina tu na makanisa yaliyopo yalikuwa na mapokeo mengi yenye nguvu ya kikanisa ambayo hayakuiendeleza Injili. Mchungaji Kamau aliona tumaini dogo kwamba wachungaji wa makanisa haya wangeipokea changamoto ya Harakati za Kufanya Wanafunzi na kuzitumia miongoni mwa watu wao.
Lakini kwa furaha, Mchungaji Kamau alithibitika kuwa amekosea. Miezi minne tu baada ya mafunzo ya DMM, eneo hilo lilikuwa limeona Vikundi vipya 98 vya Kugundua, vikiwa na kina cha vizazi vinne katika baadhi ya mikondo.
Mchungaji Ado alishiriki kwamba mafunzo ya DMM aliyoyapata kutoka kwa Mchungaji Kamau yalibadilisha mtazamo wake. Ado aliripoti kwamba mara tu baada ya kupata mafunzo ya DMM, aliweka Vikundi vya Kugundua mahali pa mahubiri ya Jumapili ili kuona kitakachotokea, kama kuna yeyote kati ya watu angerudi kuripoti jinsi alivyomtii Mungu.
Alieleza kwamba washiriki wake waliripoti furaha mpya katika uhusiano wao na Mungu na wao kwa wao. Baadhi ya washiriki waliripoti kuponywa magonjwa wakati wa maombi ya Kikundi cha Kugundua.
Mchungaji Ado anasema washiriki wa kanisa lake pia walipewa ukocha wa kuanzisha Vikundi vya Kugundua katika nyumba zao na katika mitaa yao na vikundi vingine 42 vilianzishwa katika miezi michache tu.
Mwanamke mmoja Mkatoliki aitwaye Christy alikuja kuwa mfuasi wa Kristo kutokana na kuhudhuria mojawapo ya Vikundi vya Kugundua na akaanzisha kikundi kingine ambacho kiliendelea kuzaana hadi kizazi cha nne. Kanisa moja la Kikatoliki lilianza kutumia Vikundi vya Kugundua kusoma Biblia na likagundua jinsi ya kulitii Neno la Mungu.
Mchungaji Ado anahitimisha ushuhuda wake kwamba ikiwa mwelekeo wa sasa utaendelea, yaelekea wilaya nzima itabadilishwa kupitia Injili.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 39:6 (Nov./Des. 2017), uk. 12-15. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


