INJILI YA UFALME ikihubiriwa katika dunia nzima ndiyo tumaini na ombi la kila mwamini na kilele cha Mathayo 24. Kwa kweli, Mathayo 24 inajibu mojawapo ya maswali muhimu sana ambayo watu wa Mungu wamekuwa wakiuliza tangu kuwekwa misingi ya dunia: Inagharimu nini kuona jina la Mungu likifanywa “kuwa kuu katika mataifa, tangu maawio ya jua hata machweo yake?” (linganisha Malaki 1:11). Kizazi kitakachotimiza Mathayo 24:14 kitalazimika kustahimili nini katika kizazi hicho cha mwisho?
Kwa kweli, tumepewa fursa ya pekee ya kuwa kizazi kinachoweza kusema kwamba kihalisi hakuna ukanda wa saa ambao Yesu haabudiwi ndani yake. Hata hivyo, ndani ya kila ukanda wa saa, kuna maeneo ya giza ambapo Yesu hajulikani wala haabudiwi. Hili halipaswi kuwa hivyo.
Ingawa tunaipenda Mathayo 24:14, huwa tunaepuka sehemu iliyobaki ya sura hiyo. Hii ni kwa sababu Yesu anaweka wazi kwamba kutakuwa na majanga mengi duniani kabla ya wakati ambapo hatimaye Mungu atatukuzwa miongoni mwa mataifa yote ya dunia.
Kwa mfano:
- Vita vya kiwango cha dunia nzima (mst. 6-7)
- Njaa na matetemeko ya ardhi (mst. 8)
- Mateso na kuuawa (mst. 9)
- Kuchukiwa na mataifa yote (mst. 9)
- Wengi wataikana imani yao (mst. 10)
- Manabii wa uongo (mst. 11, 22-6)
- Kuongezeka kwa uovu (mst. 12)
- Upendo wa walio wengi kupoa (mst. 12)
- Uasi unaozidishwa (mst. 12)
Yesu anaweka wazi kwamba kuja huku kwa Ufalme si kwa utaratibu, si rahisi, wala si kwa unadhifu. Hata hivyo, katika kifungu hichohicho, anatupa angalau njia tano ambazo waamini wanapaswa kuwa na “ushupavu wa kweli” ili tuweze kusimama imara hadi mwisho (mst. 13).
Yesu anatuambia tuwe tayari kuhama na wepesi wa kubadilika. Anaonyesha kwamba lazima tuweze kukimbia kwa taarifa ya ghafla (mst. 16). Kuendelea huku kwa Ufalme kutatushtukiza. Kwa hiyo, lazima tuwe tayari kwa fursa za ghafla na kubadilisha maisha, vipaumbele, na mipango yetu haraka. Hali ya sasa ya dharura ya wakimbizi ni mojawapo ya fursa kama hizo. Waislamu wengi zaidi wamemjia Kristo katika karne hii kuliko katika karne zote zilizotangulia za Uislamu. Wale walioitikia hali ya dharura ya wakimbizi wameona Waislamu wengi wakimjia Kristo. Lakini wengi wetu tulilazimika kusimamisha kazi yetu ya kawaida ili kuitikia fursa hii iliyozaliwa na msukosuko. Kutakuwa na fursa nyingine wakati ujao, na lazima tuwe tayari kuitikia haraka kazi ya Mungu. Kwa kweli, inaonekana kwamba majanga haya huenda pia yakaleta fursa isiyo na kifani ya kuanzishwa kwa Harakati za Ufalme, lakini tu ikiwa watu wa Mungu wako tayari kuhama na wepesi wa kubadilika.
Yesu anatuambia kwamba tutalazimika kukimbia lakini tunaweza kumwomba rehema katikati ya magumu yetu (mst. 20). Tunapaswa kuwa watu wa maombi ya kudumu. Haya si maombi ya aina inayochukua dakika chache. Wala haya hayatakuwa maombi ya aina ambayo tunamsihi Mungu atende. Hawa watakuwa wana na binti za Mfalme wakipigana vita kwa ushupavu pamoja na Baba yao wa Mbinguni (linganisha Waefeso 6) dhidi ya maadui wasioonekana lakini ambao matendo yao yanahisiwa. Haya ni maombi ya aina iliyo ngumu na pia iliyojaa furaha.
Yesu anatuambia tukeshe (mst. 42). Hii inamaanisha kufahamu mikakati ambayo Mungu anaitekeleza. Tunaonywa kuwa macho kuhusu manabii wa uongo. Tunawezaje kuwatofautisha manabii wa uongo na manabii wa kweli? Kwa kuujua moyo wa Mfalme. Yeye huuteka moyo wetu, roho yetu, akili yetu, na nguvu zetu. Na, anapofanya hivyo, tunakuwa na nguvu ya kuwa jasiri, kuwa hodari, kuishi kwa namna tofauti, kuwapenda wasiopendeka, kuwapenda adui zetu, na kustahimili taabu. Upendo huu wa 1 Wakorintho 13 kwa mujibu wa Leon Morris ni, “…si ukubali wa subira na wa kujisalimisha, bali ni ustahimilivu hai na chanya. Ni ustahimilivu wa askari ambaye, katikati ya mapigano makali, havunjiki moyo.”
Yesu anatuambia tuwe watumishi wema wanaoaminika (mst. 45), tuwape chakula wale wanaokihitaji. Kifungu hiki hakionekani kuhusu chakula kihalisi, bali ni mfano. Tofauti na njaa za kawaida, ambapo tunaitikia kwa msaada wa chakula kwa wenye uhitaji zaidi, mara nyingi tunawatuma watenda kazi wanaopaswa kupunguza njaa ya kiroho kwenda mahali ambapo kuna rasilimali za kiroho kupita kiasi. Mfano huu hutusaidia kuelewa kwa nini tunayapa kipaumbele makundi ya watu yaliyosahaulika duniani. Lazima tuwe waaminifu na wakali kwa nafsi zetu ili kuona kama watenda kazi wetu wa Agizo Kuu kweli wanafanya kazi mahali ambapo uhitaji wa kiroho ni mkubwa zaidi.
Yesu anatuambia tusiambatane na vitu vya kidunia. Anaonyesha kwamba hatupaswi kurudi nyuma kuchukua vitu vyetu (mst. 17-18). Kuishi kwa namna hii ni tofauti na jinsi majirani zetu wanavyoishi. Hatuishi kwa ajili ya tamaa zetu za kimwili za burudani, utajiri, na urembo (linganisha Warumi 8:5). Badala yake, tunaishi kwa ajili ya uzuri wa Mfalme. Hii inamaanisha kutumia muda mchache zaidi kwa ajili ya starehe zetu wenyewe, na badala yake kufanya kazi kwa bidii zaidi kwa ajili ya ustawi wa wengine, kutoa muda na fedha zetu, na kuishi kwa ajili ya utukufu usioonekana.
Kuishi kwa ajili ya uzuri wa Mfalme kutahitaji kujitoa sadaka—kujitoa sadaka kupita kiasi, kujitoa sadaka kunakouma. Hata hivyo, pamoja na kujitoa sadaka huko, Malaki 1:11 inasema kwamba katika kila mahali ambapo jina lake ni kuu katika mataifa, kuna uvumba wenye harufu nzuri wa sadaka zetu safi. Hakuna sadaka iliyo kubwa mno ikiwa inalifanya Jina lake kuwa kuu zaidi katika mataifa.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 40:1 (Jan./Feb. 2018), uk. 42-43. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


