Ni nini kinakujia akilini unapofikiria mhamasishaji wa umisheni? Nafasi hii kwa ujumla inaeleweka kupitia mtazamo wa upande mmoja (hasa kama mwajiri wa watumishi wa shirika), badala ya nafasi yenye sura nyingi katika makusudi ya Mungu kwa ulimwengu. Ni kawaida kuelewa kuwa mhamasishaji kwa kipindi kifupi cha huduma, ilhali ni nadra kupata wahamasishaji wanaobaki waaminifu muongo baada ya muongo. Sababu kubwa ni ukosefu wa uelewa kamili wa mhamasishaji. Kuliita Kanisa la ulimwengu kukua katika utambulisho wake wa msingi kama jumuiya ya kimisionari inayozidisha na kuzaa tena kunahitaji umati wa wahamasishaji kutambuliwa, kufunzwa, na kuwezeshwa.
Nafasi Isiyoeleweka
Wahamasishaji wa umisheni ni nafasi isiyoeleweka katika huduma ya Kikristo. Tunamwelewa mchungaji, mchungaji wa umisheni, kiongozi wa kusifu na kuabudu, kiongozi wa huduma ya watoto, kiongozi wa maombi, n.k. Lakini mhamasishaji wa umisheni—ni nani huyo na anafanya nini? Huduma katika kanisa la mahali hapo kwa ujumla inaeleweka, kama walivyo wale wanaohusika moja kwa moja katika uinjilisti wa ulimwengu, lakini mtu anayeziba pengo hili anapuuzwa. Hali hii inaonekana kuanza kubadilika kadiri Roho anavyosisitiza uhamasishaji, akiinua sauti (Isaya 40:3) zinazoitengeneza njia ya Bwana. Hawa wanakua katika ujasiri, ingawa bado hawaeleweki.
Wahamasishaji wa umisheni wako katika kila kanisa la mahali, kila dhehebu, na kila huduma inayofanya kazi pembeni mwa kanisa, mara nyingi bila kujua kwamba wana nafasi hii. Mungu kwa ukuu wake amekwisha kuwaweka ndani ya watu wake. Wao ni wachungaji, walimu, wainjilisti, wakati wengine ni viongozi walei na walei ndani ya jumuiya ya waamini, kila mmoja akisisitiza simulizi la ukombozi la Mungu na jinsi kila mwamini anavyoweza kuhusika. Wengi ni viongozi ndani ya miundo ya madhehebu au mitandao ya makanisa, waliotiwa alama na Bwana kama sauti yake ya kuhamasisha na kuandaa ndani ya miundo hii ya huduma.
Mungu Anainua “Sauti” za Isaya 40
Zaidi ya miaka 2,500 iliyopita, Roho alinena unabii kupitia Isaya unaohusu moja kwa moja mwili wa Kristo leo. Isaya 40:3–5 inatangaza, Sauti ya mtu aliaye nyikani: itengenezeni njia ya Bwana; nyoosheni jangwani njia kuu kwa ajili ya Mungu wetu.
Kila bonde litainuliwa na kila mlima na kilima kitashushwa; mahali palipopotoka patanyooshwa na mahali palipoparuza patalainishwa; utukufu wa Bwana utafunuliwa, na wenye mwili wote wataona pamoja; kwa maana kinywa cha Bwana kimenena. Isaya anafunua mwito wa msingi wa watu wa Mungu—sauti katika kila kizazi zinazowaita watu wa Mungu kwenye utambulisho wao wa msingi: kuitengeneza njia ya Bwana.
Yohana Mbatizaji aliuishi mwito huu, akitangulia kuja kwa Yesu katika karne ya kwanza. Huduma ya Yohana ya mtangulizi iliweka msingi ili kusudi la Yesu liweze kutimizwa. Yohana anatangaza katika Yohana 1:23, Mimi ni ‘sauti ya mtu aliaye nyikani; inyoosheni njia ya Bwana.’ Kwa unyenyekevu, ujasiri, na urahisi, Yohana akawa sauti ya Mungu katika kizazi chake, akiandaa kwa ajili ya kuja kwa kwanza kwa Yesu. Hata hivyo huduma ya Yohana haikuwa kilele cha unabii wa Isaya 40. Mstari wa 5 unafunua, Utukufu wa Bwana utafunuliwa na wenye mwili wote wataona pamoja. Hili halikutokea wakati wa huduma ya Yohana. Sauti ya Yohana ilikuwa utimizo muhimu wa sehemu, lakini si utimizo wa mwisho wa unabii wa Isaya. Sauti yake ilikuwa malimbuko ya mamilioni ya sauti ambazo Mungu anakusudia kuzitumia. Roho Mtakatifu anatafuta sauti zinazofanana leo ili kuitengeneza njia ya Bwana.
Utimizo wa unabii wa Isaya hautakamilika mpaka kizazi hiki cha Isaya 40 kifikie ukomavu, kwa pamoja kikilihamasisha Kanisa la ulimwengu kwa ajili ya utimizo wa Agizo Kuu. Roho Mtakatifu anatafuta sauti katika huduma za mahali, vikundi vidogo, ushirika wa huduma za vyuoni, shule za Biblia, na zaidi. Na sisi, kama Yohana Mbatizaji, tuutambue mwito wetu kama sauti ya mtu aliaye nyikani, inyoosheni njia ya Bwana, tukiitikia kwa imani na ujasiri.
Aina za Wahamasishaji
Uhamasishaji wa umisheni ni jambo kubwa, tata, lenye sura nyingi, lenye aina nyingi za viongozi. Kwa ujumla tumekosa ufahamu wa ni wangapi walio katika kundi la “mhamasishaji wa umisheni.” Ni muhimu kutambua aina mbalimbali za nafasi za wahamasishaji. Si wote walio sawa. Baadhi hujikita katika kazi mahususi wakati aina nyingine za wahamasishaji zinahusika katika maeneo mengine kabisa. Kila mmoja ni muhimu, akifanya kazi kwa kiwango cha juu, ili kuona Kanisa la ulimwengu likiwa yote ambayo Mungu anakusudia katika uhamasishaji.
Katika Waefeso 4:11, Paulo anafunua kazi tano za msingi za uongozi ambazo Yesu aliziweka ili kuandaa huduma za mahali. Kifungu hiki kiko katika muktadha wa kuliwezesha Kanisa la ulimwengu kutimiza mwito wake. Karama hizi mahususi ni nafasi zinazolihudumia Kanisa la ulimwengu. Mstari huu unatupa mwanga kuhusu mpangilio na muundo wa kiutawala wa Kanisa la mwanzo.1 Kulikuwa na aina tatu za kazi za viongozi katika Kanisa la mwanzo: baadhi ambao mamlaka yao yalitambuliwa katika kanisa lote (mitume); baadhi waliosafiri katika huduma nyingi (manabii, wainjilisti, walimu); na wale waliojikita katika huduma moja ya mahali katika eneo moja (wachungaji wa makanisa ya mahali).
Kulingana na Paulo (4:12), kusudi la mwisho la kila moja ya kazi hizo tano za uongozi ni kuyaandaa makanisa na huduma kukua kuwa wanafunzi waliokomaa, ambao wenyewe wanayafanya makundi ya watu kuwa wanafunzi. Kwa hiyo, tunaweza kusema kwamba ofisi hizo tano za uongozi kila moja ina sura ya mhamasishaji wa umisheni. Zinaweza kueleweka kama aina tano tofauti za wahamasishaji. Inawezekana kuliona simulizi kuu la ukombozi la Mungu kupitia mtazamo wa Mungu, Yesu, na Paulo kama wahamasishaji. Tunaweza kwenda hatua moja zaidi na kuelewa vivyo hivyo kuhusu kazi hizi tano za uongozi katika Waefeso 4:11. Uongozi wa huduma (unapojikita ipasavyo katika kile ambacho Biblia na historia ya ukombozi vinajikita) ni kwa kusudi bainifu la kuziandaa jumuiya za waamini za Mungu kuhamasishwa—kuelimishwa, kuvuviwa, na kuamshwa katika Agizo Kuu.
Kanisa la ulimwengu limeangukia desturi hatari ambayo haikukusudiwa kamwe katika Maandiko—viongozi kufanya kazi yote ya huduma wenyewe. Waamini wengi katika huduma za mahali wamechoshwa, hawawezi kutumia karama ambazo Mungu amewapa, kwa sababu wale walio katika huduma ya hadharani mara nyingi wameielewa vibaya kazi yao, wakiingilia eneo la kila mwamini katika makanisa ya mahali.
Kulingana na John Stott, hili linaongoza kwenye mojawapo ya mifano mitatu ya kanisa la mahali. Wa kwanza ni mfano wa kimapokeo wa piramidi ambapo mchungaji yuko kileleni mwa piramidi, wakati washiriki wako ndani ya piramidi katika ngazi za uduni. Mfano huu ni mgeni kwa Agano Jipya. Maandiko yanawaeleza wachungaji katika nafasi ya kuchunga huku kila mshiriki akichangia katika huduma kwa kutumia karama zake. Mfano mwingine ni basi. Mchungaji anaendesha basi huku waumini wakiwa abiria, wakisinzia wanaposafiri kwenda wanakoelekea. Tofauti na mifano yote miwili ni mfano sahihi wa kibiblia wa huduma ya mahali inayoundwa na washiriki ambao kila mmoja ana kazi au nafasi mahususi.2 Tunaona hili katika Waefeso 5:19–21 ambapo kila mshiriki anaelekezwa kuleta zaburi, wimbo, au wimbo wa kiroho katika mkutano.
Hebu tuwatafakari viongozi hawa watano wahamasishaji wa Waefeso 4:11 katika mwili wa Kristo, tukieleza wanachofanya, wanaowahudumia na jinsi wanavyofanya kazi.
Mchungaji-Mhamasishaji
Aina hii ya mhamasishaji ni mchungaji au kiongozi wa huduma anayesimamia kanisa au kikundi cha huduma. Huyu anaweza kuwa kiongozi wa kanisa la mahali, wa ushirika wa huduma ya chuoni au wa kujifunza Biblia. Neno la Kilatini la “mchungaji” lina maana ya mchunga kondoo. Mungu anatafuta kuinua wachungaji wahamasishaji wanaoona kazi yao kuu katika uongozi wa kanisa kuwa kulihamasisha kundi kuwa jumuiya ya kweli ya kimisionari ya Mungu, mahali walipo (tamaduni zinazokaribiana) na ulimwenguni (tamaduni za mbali). Wanahamasisha kwa kutumia jukwaa la kazi yao ya huduma. Hili linapita kuajiri watenda kazi na kufikia mtazamo mpana wa uhamasishaji wa umisheni—kuiongoza huduma yao pamoja katika safari ya kuhamasishwa na kuandaliwa. Kupitia uongozi wao, wanahimiza ukuaji na uelewa wa umisheni katika kikundi chote. Bila wachungaji kufanya kazi kwa makusudi kwa namna hii, itakuwa vigumu kuona wale walio chini ya uongozi wao wakitimiza nafasi zao katika Agizo Kuu kwa ufanisi. Wachungaji-Wahamasishaji wanaojulikana sana wa sasa na wa kihistoria ni pamoja na John Piper, David Platt, Francis Chan, A. T. Pierson (1837–1911), Andrew Murray (1828–1917) na A. J. Gordon (1836–1895).
Mtume-Mhamasishaji
Kiongozi huyu kwa kawaida huteuliwa kusimamia dhehebu, mtandao wa makanisa, shirika la huduma ya vyuoni, au eneo au wilaya ya muundo kama huo wa huduma (akisimamia huduma nyingi za mahali). Wanaweka mbele kusudi kuu la kazi ya muundo wao wa huduma katika harakati ya umisheni. Kwa kuwa neno la Kiyunani mtume linamaanisha “aliyetumwa,” wanajiona kuwa wanahusika kwa nguvu katika kuelimisha, kuvuvia, na kuamsha muundo wao wote wa huduma katika huduma ya tamaduni tofauti (katika tamaduni zinazokaribiana na tamaduni za mbali). Mungu amewaweka ndani ya muktadha wa uongozi ili kuziandaa huduma za mahali zilizo chini ya uongozi wao kustawi kama huduma moja moja za Agizo Kuu. Wakitoa zana za uhamasishaji, kozi, na rasilimali kwa huduma za mahali zilizo chini ya uelekezaji wao, wanafanya kazi ili kuona huduma za mahali zikielimishwa, kuvuviwa, na kuamshwa katika uelewa wa Agizo Kuu. Wanahakikisha kwamba wachungaji na timu za uongozi za huduma za mahali wanafunzwa kuhamasisha na kuandaa huduma zao. Ni nadra leo kumpata mtume-mhamasishaji wa aina hii, lakini Mungu anawaita wengi katika mwelekeo huu. Mifano ya kihistoria ni pamoja na Nicolaus Von Zinzendorf (1700– 1760), Samuel J. Mills (1783–1818), Charles Simeon (1759–1836), William Carey (1761–1834), A. B. Simpson (1843–1919), John R. Mott (1865–1955) huku mifano ya sasa ikijumuisha Reuben Ezemadu (Nigeria), Daniel Bianchi (Argentina), Luis Bush (Argentina) na Rick Warren (Marekani).
Nabii-Mhamasishaji
Huyu ni kiongozi ambaye Mungu humfunulia mwongozo mahususi kuhusu mikakati na ufahamu fulani katika uhamasishaji. Wanazungumza kwa mamlaka kama watu wanaosikia kutoka kwa Mungu kuhusu njia za kusonga mbele. Kazi yao kuu ni kuwaandaa wengine kuelewa ufahamu unaohusiana na mipango, makusudi, na njia za Mungu katika umisheni. Wana ushirika wa kina na moyo wa Yesu, wakizitambua njia zake na kuziwasilisha kwa uwazi kwa makanisa. Wanayasaidia makanisa, ambayo mara nyingi yamekwama katika mtazamo finyu, kubaki yakijikita katika mapenzi ya Mungu: wao ni nani kama huduma za Agizo Kuu. Ni rahisi kwa huduma za mahali kupotoshwa njia, wakipoteza utambulisho wao kama jumuiya ya kimisionari ya Mungu. Mifano ya Manabii-Wahamasishaji ni pamoja na Raymond Lull (1232–1316), Ralph Winter (1924–2009), Donald McGavran (1897–1990), Roland Allen (1868–1947), Loren Cunningham (Marekani), na Thuo Mburu (Kenya).
Mwinjilisti-Mhamasishaji
Wasomi wengi wanamwelewa mwinjilisti kama mtu mwenye karama ya kufanya kazi ya uinjilisti. Hebu tukumbuke wazo la msingi katika kifungu chetu cha Waefeso 4:12—viongozi wakiwaandaa watakatifu kufanya kazi ya huduma. Kwa hiyo, wainjilisti-wahamasishaji huyaandaa makanisa katika uinjilisti na umisheni wa mahali walipo na wa tamaduni tofauti. Wamefunzwa kwa namna mahususi na Mungu kuinjilisha kwa ufanisi na kisha kuyafunza makanisa na wanafunzi katika kuwafikia watu. Wanawaandaa washiriki “kutawanywa” ili kuzidisha makanisa mapya. Mwinjilisti-mhamasishaji ni mtu wa vitendo sana, anayefunua “jinsi” ya kuvuna mavuno miongoni mwa kundi la watu linalolengwa, iwe mahali walipo (utamaduni unaokaribiana) au ulimwenguni (utamaduni wa mbali). Wainjilisti-wahamasishaji wa kihistoria wamejumuisha John Nevius (1829–1893), David Livingstone (1813–1873), Robert P. Wilder (1863–1938) na Jonathon Goforth (1859–1936), wakati katika duru za sasa George Verwer (Uingereza), David Garrison (Marekani), David Watson (Marekani), na David Lim (Ufilipino) wanaangukia katika kundi hili.
Mwalimu-Mhamasishaji
Huyu anaweza kuwa kiongozi wa mahali ndani ya kanisa moja la mahali au anayesafiri kufundisha kundi la makanisa katika eneo fulani la kijiografia. Nafasi yao ni kulifungua Neno la Mungu, wakifunua mapenzi na mpango wa Mungu kutoka katika Maandiko. Wanawapandikiza waamini katika ufuasi, wakitangaza na kutumia ujumbe wote wa Injili ya Ufalme. Walimu-wahamasishaji wanafunua kwa vitendo nafasi nyingi za kila mwamini ndani ya harakati ya umisheni. Walimu-wahamasishaji huyasimika makanisa katika dhamira kuu ya Maandiko—Mungu mhamasishaji akilipatanisha Kanisa lake la ulimwengu na makusudi yake ya ukombozi duniani. Wanaunganisha mambo ili waamini waone maisha yao kuwa sehemu ya moja kwa moja ya hadithi ya Mungu duniani. Hii ni nafasi muhimu sana kwa kuwa walimu wanafunua kusudi la ukombozi la Mungu ndani na kupitia historia ya wokovu, wakilitumia katika muktadha wetu wa Agizo Kuu leo. Mifano ni pamoja na Hudson Taylor (1832–1905), Ajith Fernando (Sri Lanka), Paul Borthwick (Marekani) Max Chismon (New Zealand), Steve Hawthorne (Marekani), na Christopher J. H. Wright (Marekani).
Kwa makala zaidi na vipindi vya podikasti kuhusu mada za msingi zinazohusiana moja kwa moja na uhamasishaji wa umisheni pamoja na zana za uhamasishaji kwa ajili ya wahamasishaji, tafadhali tembelea https://www.globalmmi.net/.
*Dokezo la Mwandishi—Makala hii imetoholewa kutoka kitabu cha mwandishi, Rethinking Global Mobilization: Calling the Church to Her Core Identity. Kitabu hiki kinaweka misingi ya misiolojia ya kibiblia ya uhamasishaji huku kikitoa mfumo wa vitendo wa kuliandaa Kanisa la ulimwengu katika uhamasishaji. Mchapishaji, IGNITE Media, ametoa ruhusa kwa sehemu za kitabu kutumika katika makala hii. Kipate kitabu katika RethinkingMobilization.com au kitafute kwenye Amazon.
Maelezo
- John Stott, The Message of Ephesians (Leicester: IVP, 1989), 166. Rudi kwenye maandishi
- ibid, 167. Rudi kwenye maandishi
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 45:1 (Jan./Feb. 2023), uk. 42-45. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


