HIVI SASA HIVI, KUNA waamini ulimwenguni kote walio ukingoni mwa kuchukua hatua inayofuata kwa ajili ya Bwana. Machoni pa baadhi ya watu, hatua hiyo inaweza kuonekana ndogo, kama kumshirikisha mfanyakazi mwenzako Injili, au inaweza kuwa kubwa kama kuuza nyumba na kuhamia nchi mpya kwa ajili ya Yesu. Vyovyote vile, ukubwa wa hatua si jambo la muhimu; bali ni kwamba Bwana amenena na sasa tunapata fursa ya kumfuata pale anapotuita. Ingawa wakati mwingine kile anachokinena kinaweza kuonekana kigumu, kwa sisi sote tunaomkiri Yesu, tumeitwa kumtii. Kauli yake katika Agizo Kuu bado inasimama: “Wafundisheni kuyatii yote niliyowaamuru.”
Katika ulimwengu, na hata katika utamaduni wa Kikristo ambamo kwa kusikitisha utii unahisiwa kama neno chafu, sisi ni watu wa Mungu tunaopaswa kufuata popote anapoita. “Yesu ni Bwana” ni kauli ya ujasiri tunayoikiri. Na hatupaswi tu kuutii wito wake, bali pia kuwafundisha wengine kufanya vivyo hivyo. Laiti akili zetu zingeweza kuona kweli kwamba kumtii Mungu si jambo la kazi ngumu ya kuchosha, bali ni fursa ya kuheshimiwa. Lakini kama wengi wetu tunavyoweza kushuhudia, kwa ujumla utii si rahisi. Nina uhakika haikuwa rahisi kwa Ibrahimu kutoka kuelekea nchi asiyoijua. Wala haikuwa rahisi kwa Musa kumwendea Farao na kusema, “Wape watu wangu ruhusa waende.” Je, ilikuwa rahisi kwa Nuhu kujenga safina wakati hapakuwa na mvua? Je, ilikuwa rahisi kwa Yohana Mbatizaji kupungua, ili Yesu aweze kuzidi? Je, ilikuwa rahisi kwa wanafunzi kupokea vipigo, mateso na, kwa walio wengi wao, kifo kwa ajili ya imani? Je, ilikuwa rahisi kwa Sauli kuacha dini ya Kiyahudi na kuwa Paulo na kufanya kazi bila kuchoka kwa ajili ya Ufalme? Na hata Yesu mwenyewe—je, ilikuwa rahisi kwake kuyatoa maisha yake msalabani? Hata hivyo hata yeye alisema, “Si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.” Katika utamaduni wa Kikristo ambao umeketi kwa hofu bila kufanya kitu ukisubiri “milango iliyo wazi,” tuna Maandiko yaliyojaa watu waliotembea kwa imani, wakijitahidi kuelekea yaliyo mbele, hata pale mlango haukuonekana kuwa wazi sana. Kwa hiyo Bwana anaponena, utaitikiaje? Kuchukua hatua katika nyakati hizi ndicho tunachokiita Utii wa Haraka. Wa Dhati Kabisa. Wenye Gharama. Walio wengi wa watu wanaotumiwa kwa nguvu na Bwana hujifunza kuenenda katika aina hii ya utii wa dhati kabisa na wa haraka kwa ufasaha. Niwe wazi: Hii haimaanishi kwamba ni rahisi; inamaanisha tu kwamba wamejifunza kwamba Yeye ni Bwana. Mungu hupenda kuchukua vyombo dhaifu kama hivi vilivyokuwa waaminifu katika mambo madogo na kuvikabidhi zaidi. Kwa kufanya hivyo, imani hujengwa, lakini bila utii, siwezi kufikiria jinsi imani inavyoweza kukua.
Ili kulithibitisha jambo hili, rafiki yangu mmoja aitwaye Curtis anasimulia hadithi ya kuwafundisha viongozi wa mojawapo ya mitandao mitano mikubwa zaidi ya makanisa ya chini kwa chini nchini China. Mada ya wakati huo pamoja ilikuwa Bwana akiwakusanya watu kutoka makabila na mataifa yote mbalimbali kuingia katika Ufalme wake. Katika mkusanyiko huo, Curtis aliweka ramani ya dunia ukutani na akaanza kueleza baadhi ya yaliyokuwa yakitokea katika Ukristo katika nchi mbalimbali. Kundi hili kimsingi lilikuwa limetengwa na Ukristo wa ulimwengu kwa miaka 40 iliyotangulia, kwa hiyo walikuwa wakiandika maelezo kwa uangalifu mkubwa. Mafunzo hayo yalipokuwa yakikaribia mwisho, Bwana aliweka moyoni mwa Curtis kwamba mmoja wa watu waliokuwa chumbani aliitwa kwa umisheni wa nje. Hili lilikuwa jambo lisilo la kawaida kwa mwamini wa Kichina wakati huo. Ilikuwa kawaida zaidi kwa watu kusafiri ndani ya China kumshiriki Yesu, lakini si mara nyingi nje ya China. Curtis aliwashirikisha waamini waliokusanyika kile Bwana alichomwambia, na waliposikia hili, kundi liliamua kuomba kwa dakika 10 na kumtafuta Mungu ili kuona ni nani. Baada ya kuomba, swali liliulizwa kama Bwana alikuwa ameliweka jambo hilo moyoni mwa mtu yeyote. Hakuna aliyeitikia. Kwa hiyo waliomba tena kwa dakika kumi. Tena, hakuna aliyeitikia. Kwa hiyo mara nyingine, walimtafuta Bwana, lakini tena, hakuna aliyeitikia. Hili lilitokea mara saba, lakini baada ya mara ya saba, mwanamke mmoja alianza kulia na kusema, “Ni mimi. Hata kabla hujauliza swali mara ya kwanza, ramani ilipowekwa ukutani na Burma ikazungumziwa, Bwana aliniambia nimeitwa Burma. Lakini simjui mtu yeyote huko, wala lugha, wala jinsi ningeweza kujikimu. Lakini Bwana amenena nami nitatii.” Baada ya hapo, waamini waliokuwa chumbani humo walitumia muda kumweka wakfu mwanamke huyo ili atumwe. Walipomaliza, ilikuwa alfajiri ya siku iliyofuata na Curtis alichukua muda kulala, lakini aliamka saa tatu baadaye. Aliangalia huku na huko na alipoona kwamba binti yule hakuwepo, alimwuliza mwanamume mmoja alikokwenda. Akiwa amechanganyikiwa kiasi na swali hilo, mwanamume huyo alimwangalia Curtis na kusema, “Ameondoka.” Curtis aliuliza kama ilikuwa zamu yake kuleta chakula kwa ajili ya kundi, lakini mwanamume huyo, akiwa bado amechanganyikiwa kiasi na swali hilo, alisema, “Bwana alimwita Burma. Ameondoka. Ulipokuwa umelala, Bwana alimwinua mwanamke mwingine kwenda pamoja naye. Baada ya hapo, tulimwaga mifuko yetu na kulikuwa na fedha za kutosha tu kwa tiketi mbili za basi za kwenda tu hadi mpakani mwa Burma na China. Walipanda basi la kwanza saa 10 alfajiri (4:00 a.m.) na sisi ndiyo tunarudi sasa hivi kutoka kuwapeleka kituoni.”
Kwa hiyo sasa, hapo hapo ulipo, fikiria ramani ya Marekani iko mbele yako—au bora zaidi—toa ramani uiangalie. Sasa angalia jimbo lako… kaunti yako…hadi kufikia ngazi ya eneo dogo la sensa. Je, tutakuwa sehemu ya kile ambacho Mungu anafanya katika kizazi hiki? Je, tutaungana mikono pamoja katika kuona Injili ya Ufalme ikienea kama chachu katika kila kaunti na kila eneo dogo la sensa katika taifa letu na nje yake?
Utii wa Haraka. Wa Dhati Kabisa. Wenye Gharama. Ikiwa hatuendi pale Mungu anapotuita na pale tunapomhitaji Mungu, tunawezaje kutarajia kuona harakati za ukubwa wa Mungu? Kwa hiyo Mungu anapokuita, utakwenda? Iwe kubwa au ndogo, utatii? Hata pale inapokuwa ngumu, fikra yetu na iwe kwamba ni heshima na fursa kufuata hata njia ikiwa nyembamba kiasi gani.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 39:3 (Mei/Juni 2017), uk. 17-19. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


