SAFARI YA VIJAY YA KUTEMBEA KWA MAOMBI ILIMPELEKA hadi mji mmoja ambapo hakujulikana. Alienda huko kwa sababu watu wa huko walikuwa sehemu ya kundi ambalo halijafikiwa, ambalo alitamani sana kuliona likifikiwa. Lakini alipokuwa akitembea huku na huko, hakupata kitu ila kutazamwa kwa uadui. “Wewe ni nani?” mwanamume mmoja katika duka aliposimama kunywa chai yake ya asubuhi alimhoji. “Kwa nini umekuja hapa?”
Akiwa mtu wa nje na mgeni, Vijay alikabiliwa na hali nyeti. Kile ambacho angefanya baadaye kingeweza kuamua kama mlango wa kuingia katika jamii hii ungefunguka au ungefungwa. Mwitikio uliofunzwa vizuri na unaoongozwa na Roho ungeweza kusababisha habari kuenea haraka kwamba mgeni huyu “ni mtu mzuri.”
Vinasaba huanza na hatua za kwanza.
Iwe anatambua au la, hatua za kwanza za kichocheo katika jamii mpya zina umuhimu wa kina zaidi. Zinaweka mfumo wa afya kwa ajili ya kanisa la baadaye analotumaini kulianzisha. Vinasaba vyenyewe vya makanisa ya baadaye huanza na kile anachofanya mfanya-wanafunzi katika siku zake za kwanza. Hatua hizo za mwanzo huacha alama katika kila kanisa katika harakati kwa miaka mingi ijayo. Je, wanafunzi wa baadaye watajulikana kwa kuakisi huruma ya Yesu? Je, wataleta mabadiliko? Je, watazaana? Je, harakati itakuwa endelevu?
Vichocheo vya Harakati za Kufanya Wanafunzi (DMM) hukabiliwa na hali ya Vijay kila wakati. Katika Asia ya kusini, ni nadra kupokelewa kwa urafiki na kwa uwazi katika jamii mpya. Wafanya-wanafunzi wana nafasi moja tu ya kutoa taswira nzuri ya kwanza. Lakini ni ipi njia bora zaidi ya kufanya hivyo — kupitia mradi wa kijamii wa gharama kubwa, au kupitia wingi wa wafuasi wa Yesu wenye macho ya kuona kile Yesu anachokiona na kujitoa kuitikia kama Yeye alivyofanya?
Binafsi, kwa hiari na yenye kufaa kwa eneo husika
Mbinu za kawaida za kuingia katika jamii mpya mara nyingi huhusisha programu zilizopangwa tayari. Mara nyingi hutegemea rasilimali za nje na mifumo inayohitaji kuwalipa na kuwadumisha watenda kazi na shughuli. Mbinu hizi mara nyingi kwa kweli huzaa kanisa. Lakini zinaonekana kuwa zisizo za kibinafsi na makanisa mapya huishia kuwa na kasoro kubwa katika vinasaba vyao. Vipengele muhimu vya kufanya wanafunzi lazima vifundishwe au “vipandikizwe” baadaye kanisa likiwa limeimarika vizuri.
Wafanya-wanafunzi waliofunzwa vizuri wanaofuata mifumo ya kibiblia, wanaweza vizuri zaidi kuonyesha huruma kwa njia zenye maana na zinazofaa kipekee kwa kila jamii. Wanajifunza kufanya mambo yasiyohitaji programu za gharama kubwa. Wanafunzi hawa wanampenda Mungu kwa kina, na wanazifahamu kikamilifu njia Zake na kuzitii. Wanaanza kwa kutafuta mwongozo Wake kupitia maombi kwa ajili ya kila jamii mpya.
Vichocheo vinapoingiza vinasaba vinavyoakisi mtindo huu wa maisha, vikundi vipya vya Usomaji wa Biblia kwa Kugundua (UBK) huanza na kuongoza kwenye kuzaliwa kwa makanisa mapya. Wanajulikana kwa mtindo wao wa maisha wa upendo, huruma, nguvu na kweli unaofuata mfano wa Yesu. Wanafunzi wapya wanaona kwamba wana rasilimali za kuanzisha vikundi vipya, na hilo linaongoza kwenye kuzaana hadi vizazi vya 3 na 4.
Hadithi tatu zinaonyesha tofauti ambayo hili huleta katika eneo ambalo halijafikiwa.
“Si lazima mteseke hivi.”
“Alipouona umati, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamesumbuliwa na hawakuwa na msaada, kama kondoo wasio na mchungaji.” Mathayo 9:36
Stephen alikuwa akipita katika kijiji kimoja, akiomba alipokuwa akienda. Katika mazungumzo na wakazi, aligundua kwamba walikuwa wakiangamizwa na mlipuko wa homa ya nguruwe. Alianza kuuliza ni watu wangapi walioathirika na ni wangapi waliokuwa wamekufa.
Ilivunja moyo kusikia kuhusu vifo hivyo, kwa sababu alijua kwamba haikuwa lazima wateseke hivi. Chanjo ya bure ilipatikana kutoka serikalini, lakini hawakujua chochote kuhusu chanjo hiyo wala jinsi ya kuipata.
Kwa hiyo, alikutana na viongozi na kuwajulisha kuhusu chanjo hiyo. Aliwasaidia kuandika kwa uangalifu idadi ya watu wanaoishi kijijini ili idadi sahihi ya chanjo iweze kuidhinishwa. Viongozi walituma ujumbe pamoja naye kwa mamlaka husika na wakapata idhini ya chanjo.
“Kwa nini umetufanyia hivi?” watu walianza kumwuliza Stephen. Familia moja ilimkaribisha mara moja nyumbani kwao. Alianzisha kikundi cha Usomaji wa Biblia kwa Kugundua pamoja nao. Muda mfupi baadaye, kikundi hicho cha Kugundua kilikuwa kanisa jipya. Familia hiyo ilianzisha UBK nyingine mahali pengine ambayo nayo ilikua na kuwa kanisa. Mmoja wa wanafunzi wapya kutoka kanisa hilo haraka alianzisha kikundi kingine yeye mwenyewe. Ndani ya muda mfupi, hili lilikua hadi vizazi vitatu vya makanisa.
Huruma kama mtindo wa maisha ni sifa muhimu ya wanafunzi wa Yesu. Watu wa kawaida huonyesha huruma kama sehemu ya maisha yao ya kila siku. Stephen hakuonekana kama mwakilishi wa shirika. Alionyesha tu kujali kwa dhati. Alijua rasilimali iliyoweza kusaidia, naye akawaunganisha nayo.
Ninawezaje kusaidia?
“Msichukue mfuko wa fedha, wala mkoba, wala viatu….” Luka 10:4
Kulingana na maagizo ya Yesu, Samuel hakuchukua fedha za ziada alipoanza kutembelea kijiji chenye takriban nyumba 150. Kama kawaida, hakuna mtu aliyetaka kuzungumza naye, lakini aliomba apate njia ya kuungana na watu hawa.
Aliona watoto wakikimbia huku na huko, bila kutunzwa wala kuadibishwa. Aligundua kwamba hawa walikuwa watoto wa wazazi wanaofanya kazi ambao hawakuwa na muda wala ujuzi wa kuwasaidia katika kazi zao za shule. Shule ya umma waliyosoma haikutoa msaada wa kuwafundisha jinsi ya kujisomea na kujiandaa kwa mitihani. Kwa hiyo, waliachwa bila uangalizi kwa sehemu kubwa ya mchana.
Kupitia maombi Samuel alisukumwa kuwafundisha masomo ya ziada yeye mwenyewe. Kulikuwa na mti mkubwa katikati ya kijiji ambapo alijitolea kukutana na watoto hawa na kuwafundisha. Alianza na watano na muda si mrefu wakaongezeka hadi kumi na tano. Baada ya muda wa masomo, alishiriki hadithi za Biblia, akiwafundisha kuwa wema na kuwatii wazazi wao.
Wazazi walianza kuona mabadiliko kwa watoto wao. Wanandoa mmoja waliona alichokuwa akifanya wakamkaribisha nyumbani kwao, na hatimaye wakamweleza matatizo katika ndoa yao. Muda si mrefu Samuel alikuwa akishiriki hadithi za Biblia na familia nzima. Aliwauliza walijifunza nini kutoka katika hadithi hizo na wangefanya nini kuhusu hilo. Kikundi hiki kilianza kukua. Kisha binti aliyekuwa darasa la tisa alianzisha kikundi kingine pamoja na marafiki zake watano. Kisha mama na baba walianzisha kikundi kingine katika jamii walimofanya kazi.
Kwenda katika jamii bila rasilimali zozote za kushiriki ni kinyume na mantiki ya kawaida. Ni kawaida zaidi kuleta kitu kutoka nje. Mbinu hii ya kawaida inalenga kuisaidia jamii kwa kitu ambacho haiwezi kujifanyia yenyewe. Hata hivyo, nia njema mara nyingi hutafsiriwa kama “kununua” haki ya kusikilizwa, dhana ya kawaida katika sehemu kubwa ya Asia. Hakuna kitu kinachoharibu zaidi mwanzo wa harakati kuliko kuendeleza mbinu inayoongoza kwenye kutoelewana huku.
Aliamua kutokuwa mzigo
“Mnakumbuka, ndugu, kazi yetu na taabu yetu: Tulifanya kazi usiku na mchana, ili tusimlemee yeyote kati yenu tulipokuwa tukiwahubiri Injili ya Mungu.” – 1 Wathesalonike 2:9
Dileep alipata njia nyingine ya kuitumikia jamii. Alipata kazi ya kuuza magazeti. Kwa njia hii, hakuwa mzigo kwa jamii na alikuwa na njia ya kuwafahamu watu.
Katika nyumba moja kwenye njia yake ya kusambaza magazeti, mwanamume mmoja aitwaye Ravi alikuwa akitoka kulipia gazeti lake. Siku moja, hakuwa Ravi, bali mke wake, aliyetoka nyumbani. “Mume wako yuko wapi?” Dileep aliuliza. Alieleza, “Hajisikii vizuri kwa wiki mbili. Tulimpeleka hata hospitalini kwa matibabu, lakini hapati nafuu.” Dileep aliuliza, “Je, naweza kuingia na kuzungumza naye?”
Kwa hiyo, Dileep alimtembelea Ravi, akisikiliza matatizo yake yote na kushiriki hadithi ya jinsi Mungu alivyoumba ulimwengu na anavyowajali wanadamu. “Usijali,” alisema, “Nitamwomba Mungu ili akuponye ugonjwa wako.” Asubuhi iliyofuata, Ravi alijisikia vizuri zaidi. Hili lilileta ziara za mara kwa mara za Dileep na hadithi zaidi kutoka katika Biblia. Kisha ziara hizo zikawa kikundi cha kugundua cha watu saba. Muda mfupi sana baadaye, mmoja wa wale saba alianzisha kikundi kingine cha watu watano.
Ubunifu wa Dileep ulimletea mapato binafsi na pia njia endelevu ya kuungana na watu. Mara uhusiano ulipojengwa, alichohitaji kufanya ni kuendelea na kile alichokuwa akifanya. Uendelevu hauwezi kuwa jambo la kufikiriwa baadaye. Programu inaweza kuishiwa rasilimali, lakini maisha ya kujitoa dhabihu ni ushuhuda endelevu wa neema ya Mungu.
Binafsi, yenye kufaa na endelevu
Wafanya-wanafunzi watatu waligundua kwamba kujitoa binafsi kuona mahitaji na kuwapenda jirani zao kwa njia yenye maana katika kuitikia kulizaa matunda ya kudumu.
Katika kisa kimoja, mfanya-wanafunzi aliona tatizo na kuisaidia jamii kunufaika na rasilimali ya serikali. Katika kingine, alitumia rasilimali binafsi – muda na juhudi zake mwenyewe kuwafundisha watoto masomo ya ziada. Na katika cha tatu, alipata kazi ya kujikimu na kuwepo kwa watu bila kuwa mzigo.
Wote watatu walifunzwa na kulelewa ili kutekeleza kwa vitendo kanuni kutoka katika Maandiko, wakizigeuza kuwa hatua za vitendo zinazoleta athari ya kimkakati. Katika ulimwengu tata tunaoishi, njia ya kusonga mbele inahitaji wingi wa wanafunzi wanaoishi na kufanya kazi kwa macho yaliyo wazi kabisa na kwa imani thabiti kwamba Mungu atawatumia kuleta tofauti. Matokeo yake ni kuzaliwa kwa mikusanyiko mipya yenye vinasaba hivi hivi vilivyopandwa ndani yake tangu mwanzo kabisa. Kuna tofauti ya kushangaza katika sifa muhimu za harakati zinazoanza kwa njia hii.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 39:6 (Nov./Des. 2017), uk. 16-19. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


