Nilikuwa nikiongoza mkutano wa viongozi wa makanisa wazawa wapatao 30 kutoka makabila mbalimbali. Niliwauliza wote, “Ni changamoto gani kubwa zaidi mnayokabiliana nayo?” Kiongozi mmoja kutoka kabila la Wahmong alisimama na kusema kwamba tatizo lao kubwa zaidi lilikuwa kwamba mishahara ilikuwa imekatwa na huduma ya kanisa ilikuwa ikiathirika. Alieleza kwamba ofisi ya kitaifa ya dhehebu ilikuwa ikituma kila mwezi ruzuku ya mishahara (iliyopokelewa kutoka vyanzo vya wafadhili wa kigeni) kwa ajili ya viongozi wa kanisa lake la mahali.
“Asante, mwalimu,” nilijibu. “Niruhusu niulize maswali machache, ili nielewe jinsi huduma ya kanisa la mahali inavyoathirika. Ninajua kwamba katika kabila lenu mnawafunza kila mwaka viongozi wa vikundi vidogo vya Theological Education by Extension (TEE). Ruzuku zilipokuwa zikija, mlikuwa mkiwafunza viongozi wangapi wa vikundi vidogo vya TEE kila mwaka?”
Alisema, “Viongozi wapya wawili au watatu kila mwaka.”
Niliendelea, “Katika mwaka mmoja tangu ruzuku ikatwe, mmewafunza viongozi wangapi wa vikundi vidogo vya TEE.”
“Tumewafunza viongozi wawili au watatu.”
“Hebu nione kama nimeelewa sawasawa. Mmewafunza idadi ile ile ya viongozi, mkiwa na ruzuku au bila ruzuku.”
“Ndiyo,” alikubali.
Swali langu la pili, “Katika wiki ya kawaida wakati ruzuku zilipokuwa zikitolewa, sadaka ya kanisa ya kila wiki ilikuwa kiasi gani?”
Alitaja kiasi fulani. Kisha nikauliza, “Tangu ruzuku ikatwe, sadaka ya kawaida ya kila wiki imekuwa kiasi gani?” Alisema sadaka ilikuwa imeongezeka zaidi ya mara mbili!
“Hilo linawezekanaje?” niliuliza.
Alijibu, “Sababu iko wazi kabisa: kwa sababu kila mtu alitambua kwamba kanisa hili liliwategemea washiriki wa mahali hapo ili lifanye kazi.” Walionyesha kwamba kanisa ni lao kwa kutoa.
“Mwalimu, tafadhali nivumilie kwa swali moja la mwisho. Mlikuwa mkibatiza watu wangapi kila mwaka mlipokuwa mkipokea ruzuku?”
Alijibu, “Kwa kawaida ubatizo mmoja mpya kwa mwaka.”
“Ni watu wangapi wanaobatizwa kwa mwaka, tangu mkate ruzuku?” Alieleza kwamba watu wapatao 10 walibatizwa katika mwaka huo. “Lo, hilo ni jambo la ajabu! Ni nini kinachoeleza ongezeko hili kubwa?”
“Lo, hilo ni rahisi sana kueleza. Hapo awali, tulipopokea mshahara, dhehebu kuu lilitueleza ni vijiji gani tulipaswa kufanya uinjilisti, na tena katika eneo letu la karibu tu. Mishahara ilipoacha kutolewa, tuliweza kwenda popote Roho wa Mungu alipotuongoza. Tuliweza kwenda kuwatembelea ndugu zetu na marafiki zetu tuliounganika nao katika wilaya nyingine, na walikuwa wazi zaidi sana kwetu na kwa ujumbe wa Kristo.”
“Basi hebu nirudie kwa ufupi ili nione kama nimeelewa sawasawa. Tangu mshahara ukatwe, mmeweza kuwafunza idadi ile ile ya viongozi wa vikundi vidogo kila mwaka, mmeongeza sadaka za kanisa lenu mara mbili na mna ufanisi mara 10 zaidi katika uinjilisti. Je, unaweza kunieleza jinsi huduma ya kanisa imeathirika kwa kutopokea mishahara?”
Mazungumzo haya ya ghafla yanaonyesha baadhi ya njia ambazo matumizi ya fedha za nje yanaweza kudhoofisha ukuaji wa Ufalme na kuzuia ufanyaji wa wanafunzi wa kweli kwa vizazi na kuzaana kwa makanisa. Ingawa yalimwaibisha kiongozi huyo, yaliwagusa kwa kina wengi wa waliokuwepo.
Ufadhili kutoka nje kwa viongozi wa kanisa la mahali ili watekeleze shughuli za kawaida za kanisa la mahali ulidhoofisha uhusiano kati ya washiriki wa mahali hapo na uongozi wao wa mahali. Ufadhili kutoka nje ulipunguza utoaji wa mahali hapo kwa sababu watu hawakuona haja ya kutoa wakati fedha zilizopatikana kwa urahisi zaidi zingeweza kupatikana.1 Hisia ya wenyeji kwamba maisha ya huduma ya kanisa ni yao ilipungua kwa sababu ya uwepo wa wafadhili wa nje. Kile ambacho hakikutajwa katika mkutano huo ni ukweli wa ziada kwamba msaada wa kichungaji ulikuja na masharti na matarajio juu ya dhehebu na kanisa la mahali.
Nimeona mienendo hii na mingine mibaya inayosababishwa na mishahara kutoka nje katika ngazi ya kanisa la mahali katika makumi ya makanisa kote katika nchi hiyo. Hakuna anayejifanya kwamba fedha hazina nafasi katika huduma na katika kuanzisha makanisa mengi. Hata hivyo, chanzo cha fedha na jinsi fedha zinavyotumika kutakuwa na athari kubwa kwa kile kinachotokea. Kuleta fedha za nje kwa makanisa ya mahali ili makanisa hayo yatekeleze kazi zao za msingi kama kanisa karibu kila mara kutadhoofisha harakati.
Vichocheo vingine vya harakati kote ulimwenguni wamefikia hitimisho linalofanana, kuhusu baadhi ya njia nzuri na baadhi ya njia mbaya za kutumia fedha za nje katika kuchochea harakati. David Hunt, kwa kuzingatia utafiti wake na uhusiano wake wa karibu na harakati barani Afrika, anaeleza kwamba ufadhili wa nje unaweza kwa urahisi kuingiza ugeni katika huduma. Hilo, kwa upande wake, linaweza kudhoofisha harakati na hisia ya wenyeji kwamba kazi ni yao.
Ikiwa kanisa linapokea msaada, iwe katika mfumo wa msaada kwa mpanda makanisa au mchungaji wa mahali hapo, … basi mfumo wa kanisa unabeba kipengele cha kigeni. Ufadhili wa kigeni wa majengo ya makanisa umemaanisha kwamba jamii ilipokea kitu ambacho haingeweza kukizalisha yenyewe peke yake. Ili kanisa lirudie jambo hili katika jamii inayofuata, lazima lisubiri msaada zaidi kutoka nje.2
Mfano wa pili unatoka katika utafiti wa shahada ya uzamivu wa Wayne Allen kuhusu athari ya kutoa ruzuku kwa watendakazi wazawa wa kanisa nchini Indonesia. Alihitimisha kwamba “ukuaji wa kanisa la kitaifa ulituama au kusimama pale umisheni ulipoanza kutoa ruzuku kwa watendakazi wazawa wa kanisa.”3 Hili ni onyo zito kwa wote walio makini kuhusu kuzaana kwa makanisa.
Baadhi ya matumizi ya fedha za nje karibu kila mara hudhoofisha uwezekano wa harakati. Haya yanapaswa kuepukwa:
- Mishahara au ruzuku za mishahara kwa wachungaji au viongozi wa kanisa ili watekeleze kazi za msingi za kanisa la mahali (Matendo ya Mitume 2:36-42). Kazi hizo za msingi ni pamoja na, lakini si tu, uinjilisti, ufuasi na ibada za kawaida.
- Kufadhili majengo ya makanisa ya mahali, ikiwa ni pamoja na kujenga upanuzi wa nyumba za viongozi wa makanisa ya nyumbani ili kuongeza ukubwa wa chumba cha mikutano.
- Kukodisha majengo ili makanisa ya mahali yakutanie humo.
- Kuwapeleka viongozi wa kanisa kwa miaka kadhaa katika chuo cha Biblia au seminari ya bweni katika eneo jingine au nchi nyingine. Wengi wa wanaofanya hivyo wanafunzwa hadi kupoteza manufaa yao katika kazi ya uanzilishi vijijini walikotoka, na idadi kubwa yao hawarudi kamwe katika eneo lao ambalo halijafikiwa ili kuanzisha kazi mpya, bali hutafuta nafasi za kazi za kanisa zenye mshahara, ambazo mafunzo yao ya seminari yaliwaandaa kwazo.
- Shughuli ambazo kanisa la mahali tayari limezifadhili lenyewe, lakini mfadhili anataka kuona zikifanyika kwa haraka zaidi au kwa upana zaidi. Tumeona kwamba ni afya zaidi sana kuziacha huduma zikue kwa kasi ambayo viongozi wa mahali hapo wanaweza kuimudu. Ufadhili uliotolewa ili kuharakisha shughuli umeleta mafanikio ya muda mfupi, lakini kwa bahati mbaya, unajenga mtindo wa kufikiri kwamba mambo yanaweza kutokea tu pale mfadhili wa nje anapoyasukuma.
- Shughuli hizi tano za ufadhili wakati mwingine zimeleta msukumo wa muda mfupi, lakini katika kila kisa tunachokijua, zimeweka mifumo isiyoweza kuzaa tena, zimedhoofisha hisia ya umiliki na uwajibikaji wa makanisa ya mahali, na zimeunda mifumo isiyoweza kudumu katika kuzaana kwa wanafunzi na makanisa. Kwa maneno mengine, vinasaba vya juhudi hizi za ufadhili vinapingana na kuzaana halisi kwa wanafunzi na makanisa.
Baadhi ya matumizi ya fedha za nje yamezisaidia harakati kwa uthabiti kuanza au kupanuka.
Kwa kuzingatia mahojiano na viongozi wa harakati na uzoefu binafsi, haya ni baadhi ya matumizi ya fedha za nje ambayo yamethibitika kusaidia kuchochea harakati:
- Mafunzo katika mitazamo ya msingi na mazoea ya kuzidisha wanafunzi na makanisa. Unapofadhili mafunzo ya kuzidisha, daima dai mchango wa mahali hapo. Kwa mfano, kanisa la mahali linaloandaa mafunzo linaweza kutoa malazi na chakula, na washiriki wanaweza kuchangia chakula au fedha. Viongozi wa harakati wanapaswa kufunzwa mahali walipo na wakiwa kazini. Mafunzo ya muda mfupi ya nje ya chuo, ambayo huwaweka watendaji wa harakati katika muktadha wao na wakishiriki kikamilifu katika huduma, nayo yamethibitika kusaidia.
- Fedha za usafiri na baadhi ya gharama ndogo ndogo ili kusaidia vikundi vya jumuiya ya watendaji vya eneo au vya kikanda kukutana mara kwa mara kwa ajili ya mafunzo, utatuzi wa matatizo na kutiana moyo. Kubadilishana mawazo katika nyakati hizi za kunolewa kumekuwa daima msukumo wa kuona harakati zikianza na kupanuka.
- Vifaa vya gharama nafuu kama vile spika ndogo zinazotumika pamoja na kadi za SD, Biblia za sauti, na Maandiko yaliyochapishwa au sehemu za Maandiko.
- Mikakati rahisi ya kuingia inayoweza kuzaa tena ili kujenga mahusiano katika maeneo au jamii ambazo hazijafikiwa ambapo hakuna uhusiano wa awali. Harakati huenea hasa kupitia njia za mahusiano lakini pia zitahitaji kugundua mikakati ya kuingia katika maeneo ambapo hakuna uhusiano wa awali. Kuunganika na jamii katika mazingira ya uanzilishi ili kushiriki Injili kunaweza kuhitaji ufadhili fulani. Tahadhari inahitajika ili kutounda mbinu za kuingia zenye gharama kubwa au tata ambazo haziwezi kurudiwa na wengine. Mikakati ya kuingia inayoweza kuzaa tena ni ile ambayo waamini wa kawaida wa mahali hapo na makanisa rahisi wanaweza kuiiga na kuitumia katika maeneo mengi.
- Fedha za misaada ya maafa kwa ajili ya shughuli zilizobainishwa na kwa kipindi maalum cha muda. Baada ya maafa kama vile njaa, tsunami, tetemeko la ardhi, vita, au mlipuko wa ugonjwa, mahitaji na fursa nyingi hujitokeza ambazo zinaweza kuzaa matunda mengi katika kuwapata Watu wa Amani na kuanzisha vikundi vipya na makanisa rahisi. Harakati nyingi zinaripoti kwamba juhudi za kishujaa za washiriki wao wakati wa janga la COVID-19, ambazo zilifadhiliwa kwa kiasi kikubwa na fedha za mahali hapo na kiasi fulani cha ufadhili wa nje, zimeleta kuzaa matunda kukubwa zaidi kuliko miaka iliyotangulia.
- Mazingira ya uanzilishi yanaweza kuleta hitaji la kuweka watendakazi ili kuchochea harakati. Mbinu moja iliyozaa matunda imekuwa ufadhili wa mara moja wa kuwatuma viongozi wa harakati waliokomaa pamoja na familia zao ili waanzishe biashara changa. Biashara hizi si tu zinaitegemeza familia bali pia zimezalisha faida ya kusaidia kuanzisha biashara nyingine changa za uanzilishi zinazofanana.
- Miradi inayosaidia kuchochea harakati, lakini kwa wazi iko nje ya kiwango cha ujuzi na/au fedha za kanisa rahisi la mahali au mtandao wa makanisa. Baadhi ya mifano ingekuwa tafsiri ya Biblia, kutengeneza vyombo vya habari kama vile filamu ya Yesu, au kuunda maudhui ya mtandaoni kwa ajili ya harakati. Bado juhudi inahitajika ili kukuza hatua binafsi na hisia ya umiliki kwa makanisa yoyote ya mahali yatakayonufaika na mradi kama huo.
- Ruzuku za kifedha na fedha za usafiri kwa wazidishaji wa makanisa, wakufunzi wa kuzidisha na vichocheo vya kikanda waliothibitika. Majukumu haya matatu yanaelezwa katika “ngazi tano za uongozi” ambazo mara nyingi huonekana katika kuchochea harakati. Tazama maandiko ya Steve Addison4 na Nathan Shank5 ambayo yameyakuza mawazo haya. Tumeona kwamba ufadhili wa nje unasaidia katika ngazi hizi tatu. Hata hivyo, kuleta ufadhili kwa watu wa mahali ili wafanye uinjilisti na kukusanya kanisa katika eneo lao (wapanzi wa mbegu na wapanda makanisa) kumekuwa na madhara kila mara, kama kisa cha mwanzo wa makala hii kinavyoonyesha.
- Kutokana na mafunzo yaliyopatikana nchini Bangladesh, Richard Reach6 anaeleza kwamba ni muhimu sana kuanzisha kamati ya mahali hapo kwa ajili ya uwajibikaji wa kifedha pale ufadhili wa kigeni wa nje unapotumika. Kiunganishi au mfadhili wa nje anahitaji kujenga na kudumisha mahusiano ya karibu ya kibinafsi na wale wanaopokea fedha, na kusisitiza uwajibikaji. Uwajibikaji unahitaji kurekebishwa ili uendane na muktadha wa utamaduni wa mahali hapo badala ya kusafirisha tu viwango vikali vya Kimagharibi vya fedha, mahusiano yanayohusika yasije yakaharibika.
Harakati hustawi pale wanafunzi wa mahali hapo, kwa nguvu za Roho Mtakatifu, wanapoipeleka Injili kwa hiari yao wenyewe kwa familia, marafiki, majirani na wafanyakazi wenzao. Ili Ufalme upanuke kupitia hatua za hiari, kichocheo cha nje kinahitaji kuacha nafasi kwa wenyeji wa ndani kufuatilia utume wa Mungu. Kuzaana kwa hiari kwa wanafunzi hutokea vizuri zaidi kupitia uwezo na rasilimali za kifedha za kanisa la mahali na waamini. Kwa sababu hiyo, tunahitaji kuepuka kwa dhati matumizi ya fedha za nje ambayo hudhoofisha uwezekano wa harakati, na kuweka mipaka ya ufadhili kwa matumizi ambayo yameonyesha uwezekano wa kusaidia harakati kuanza au kupanuka.
Kwa usomaji zaidi:
Corbett, Steve, and Brian Fikkert. When Helping Hurts: How to Alleviate Poverty without Hurting the Poor and Yourself. Chicago, IL: Moody Publishers, 2012.
Reach, Richard. Movements that Move: Seven Root Principles Driving Movements. St Charles, IL: Church Smart Resources, 2016.
Lupton, Robert D. Toxic Charity: How Churches and Charities Hurt Those They Help, And How to Reverse It. San Francisco, CA: HarperOne, 2012.
Saint, Steve. The Great Omission: Fulfilling Christ’s Commission Completely. Edmonds, WA: YWAM Publishing, 2001. Tazama sura ya 7: “Money Matters More than You Know.”
Schwartz, Glenn. When Charity Destroys Dignity: Overcoming Unhealthy Dependency in the Christian Movement. Bloomington, IN: Author House, 2007.
Maelezo
- Stout, Ken (2008). Tasnifu ya MA: Fostering Sustainability & Minimizing Dependency in Mission Finances. 1-2. Rudi kwenye maandishi
- Hunt, David F. (2009). Tasnifu ya uzamivu: A Revolution in Church Multiplication in East Africa: Transformational Leaders Develop a Self-Sustainable Model of Rapid Church Multiplication. 114 Rudi kwenye maandishi
- Allen, Wayne. “When the Mission Pays the Pastor.” Mission Frontiers, Januari-Februari1999. Rudi kwenye maandishi
- Addison, Steve. Pioneering Movements: Leadership that Multiplies Disciples and Churches. Downers Grove, IL: Inter Varsity Press, 2015. Rudi kwenye maandishi
- Shank, Nathan. “5 Levels of Movement Leadership” Mission Frontiers, Machi-Aprili 2016. 25-27 Rudi kwenye maandishi
- Mahojiano binafsi, Januari 2016 Rudi kwenye maandishi
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 44:1 (Jan./Feb. 2022), uk. 34-37. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


