NILIPOKUWA NA UMRI WA MIAKA ISHIRINI NA KITU, MIMI (JEFF) nilikuwa mkimbiaji bora wa masafa marefu pamoja na Nike. Mwaka 1982, nilisafiri kutoka Oregon ili kukimbia katika New York City Marathon. Nilikuwa nimejifua kwa miezi kadhaa, nikikimbia maili 100 kwa wiki na kuusukuma mwili wangu hadi mwisho wa uwezo wake. Hata hivyo, siku moja kabla ya mbio hizo ndefu niliugua. Nilizikosa mbio!
Katika 1 Wakorintho 9:24, Paulo alitumia picha ya kukimbia kwa ajili ya mbio halisi za kuwafikia watu waliopotea kwa Injili. “Je, hamjui kwamba katika mashindano ya mbio wakimbiaji wote hukimbia, lakini ni mmoja tu anayepokea zawadi?” (1 Wakorintho 9:24). Mwishoni mwa maisha yake, Paulo alitangaza kwa uhakika, “Nimepigana vita vizuri, nimemaliza mbio, nimeilinda imani.” (2 Timotheo 4:7). Je, sisi, kama wanafunzi wa Yesu, hatutaki kusema jambo hilo hilo? Marafiki, msizikose mbio hizi!
Yesu alifyatua bunduki ya kuanzisha mbio alipotangaza: “Mamlaka yote mbinguni na duniani nimepewa mimi. Basi nendeni mkawafanye wanafunzi mataifa yote, mkiwabatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, mkiwafundisha kushika yote niliyowaamuru ninyi. Na tazama, mimi niko pamoja nanyi siku zote, hata mwisho wa nyakati” (Mathayo 28:18-20).
Kanisa la kwanza liliipokea changamoto ya Yesu na kuruka ndani ya mbio! Kitabu cha Matendo ya Mitume kinafuatilia hadithi ya ajabu ya Injili ikienea kutoka kwa kikundi kidogo cha wanafunzi Wayahudi huko Yerusalemu hadi ilipoenea katika Dola yote ya Kirumi na kuwa kanisa la kimataifa. Hii ni hadithi ya kushangaza ya wanafunzi wanaofanya wanafunzi, makanisa yanayopanda makanisa, na harakati zinazowezeshwa na Roho, zilizojaa maombi na zinazoizingatia Injili.
Tunapoona kile Mungu anachofanya kote ulimwenguni leo inahisiwa kama kitabu cha Matendo ya Mitume. Katika miongo ya hivi karibuni tumeona mavuno ya kimataifa yasiyo na kifani ya wanafunzi wanaofanya wanafunzi na makanisa yanayopanda makanisa kadiri harakati zilivyozaana katika maeneo mbalimbali. Hata hivyo sehemu kubwa ya kanisa la ulimwenguni kote bado haijui kabisa kuhusu kazi hii kuu ambayo Mungu anaifanya katika siku zetu wenyewe.
Mwezi Mei 2017 nilihudhuria mkusanyiko nchini Uingereza wa viongozi 30 wa umisheni wenye uzoefu ambao kwa miongo kadhaa wamehusika na Harakati za Kupanda Makanisa (CPM) kote ulimwenguni. Tulikusanyika ili kuchunguza kazi ya kuanzisha kazi miongoni mwa kila kundi la watu wasiofikiwa kwa harakati ya ufalme ifikapo mwaka 2025. Mpango huu wa 24:14 umepata jina lake kutoka Mathayo 24:14, ambapo Yesu aliufafanua mstari wa kumalizia wa mbio halisi: “Na Injili hii ya ufalme itatangazwa katika ulimwengu wote kuwa ushuhuda kwa mataifa yote, na ndipo mwisho utakapokuja.” Huo ndio mstari wa kumalizia ambao Yesu Kristo alikuwa nao akilini alipotuita kwenye mstari wa kuanzia katika Mathayo 28:18-20.
Mkusanyiko ule wa Uingereza ulimetameta kwa majadiliano yenye nguvu, maombi ya bidii na uhakika wa pamoja kwamba Mungu anafanya jambo fulani duniani leo linalodai umakini wetu. Hata hivyo katikati ya hadithi za harakati za ajabu kote ulimwenguni, watafiti walitufanya tutafakari kwa uzito. Duniani kote ufalme unapoteza nafasi; kusonga mbele kwa Injili hakuendani hata na ukuaji wa idadi ya watu duniani. Ikiwa tutaufikia mstari wa kumalizia wa Mathayo 24:14, ni wazi kwamba tunahitaji kuona kuongezeka kwa wingi kwa harakati za ufalme zinazoenea kwa haraka, zinazofanana na kitabu cha Matendo ya Mitume, kote ulimwenguni.
Wakati wa mkusanyiko huo, swali moja lilianza kuwa kubwa moyoni mwangu: Tunawezaje kulihamasisha kanisa la mahali hapo kwa ajili ya mbio hizi kuu ambazo Mungu ametuitia? Viongozi wengi waanzilishi wa umisheni na mashirika ya umisheni yenye ushawishi wameungana nasi kwa shauku, lakini wito huu si kwa ajili ya wachache waliochaguliwa tu. Tunahitaji wachungaji na makanisa kote ulimwenguni kushikamana nasi bega kwa bega. Kanisa la mahali hapo liko katika kiini cha mpango wa Mungu kwa siku zetu. Umisheni ulianza katika kitabu cha Matendo ya Mitume pamoja na kanisa la mahali hapo, kwanza huko Yerusalemu na kisha huko Antiokia. Kwa hiyo ni jambo la kibiblia kwa kanisa la mahali hapo kuwa katikati kabisa ya mbio, si kuzikosa mbio.
Kanisa la mahali hapo kote ulimwenguni lina rasilimali nyingi mno – rasilimali watu, rasilimali za kifedha, rasilimali za maarifa, rasilimali za teknolojia na hasa rasilimali za maombi. Je, kitia-moyo cha Paulo kuhusu ukarimu (2 Wakorintho 8:12-15) hakitumiki pia katika kuchangia kukamilisha kazi hii kuu iliyopewa kila kanisa na kila mwanafunzi?
Kwa sababu mimi ni mchungaji nchini Marekani, nililifikiria hasa kanisa katika nchi yangu. Tunawezaje kuyatia moyo makanisa na wachungaji kote Marekani, pamoja na katika nchi nyingine, kujiunga na kile Mungu anachokifanya katika harakati hizi za Injili kote ulimwenguni? Kama mtu mmoja katika mkusanyiko alivyouliza, “Tunawezaje kuliamsha jitu linalosinzia, yaani kanisa?”
Makadirio ya tahadhari yanaonyesha zaidi ya makanisa 300,000 ya Kiprotestanti nchini Marekani leo. Hii inamaanisha kwamba kila moja ya makundi ya watu wasiofikiwa 7,000 lingeweza kuwa na makanisa ya Kimarekani mengi kama 43 yanayosaidia kulifikia. Takwimu hizi zinanishangaza sana! Huenda baadhi ya makanisa au makundi ya makanisa yakaanzisha kazi miongoni mwa UPG moja kwa mikakati ya CPM. Huenda baadhi ya yale makanisa makubwa sana 1,667 ya Kimarekani yakasaidia kuanzisha kazi miongoni mwa UPG kadhaa kwa mikakati ya harakati. Ongeza kwa hili makanisa yanayoamini Biblia katika kila nchi nyingine, na tunapaswa kujiuliza kwa nini mbio bado hazijamalizika.
Kanisa la kwanza katika kitabu cha Matendo ya Mitume lilikuwa mwaminifu katika kizazi chao. Je, sisi tutakuwa waaminifu katika kizazi chetu? Je, tutakuwa kama Paulo katika 1 Wakorintho, tukikimbia mbio ili kuwafikia watu kwa ajili ya Yesu Kristo, bila kujali gharama? Je, kila mmoja wetu ataweza kusema mwishoni mwa maisha yake, kama Paulo alivyosema: “Nimemaliza mbio”?
Nilipokuwa kijana, nilipata fursa ya kukimbia katika baadhi ya mbio ndefu kuu za dunia. Lakini fursa hiyo hailinganishwi na fursa kuu ya kukimbia mbio halisi, za kuwafikia watu wa mataifa yote ya dunia kwa Injili ya Yesu Kristo. Tunahitaji kila kanisa na kila mwanafunzi katika mbio hizi. Tunakuhitaji wewe. Usizikose mbio hizi.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 40:1 (Jan./Feb. 2018), uk. 40-41. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


