Mungu anatenda kazi! Anaanzisha Harakati za Kupanda Makanisa (CPM), njia pekee ya huduma ambamo ukuaji wa ufalme unazidi ukuaji wa idadi ya watu, huku pia zikibadilisha jamii kutoka ndani—kwa njia kamilifu zinazogusa maisha yote na zinazojitegemea kifedha. Katika CPM, wanafunzi huzidisha wanafunzi, makanisa huzidisha makanisa, na viongozi huzidisha viongozi. Pia tunajifunza kwamba harakati huzidisha harakati! Utafiti wa viongozi wanaowakilisha CPM zaidi ya 1500 ulionyesha kwamba 80–90% ya harakati zimeanzishwa na harakati nyingine. Harakati hizi zinatiririka kutoka katika makundi ya watu na maeneo yao ya mwanzo kuingia katika makundi mengine ya watu na maeneo mengine, ya karibu na ya mbali. Na harakati hizi ndizo tumaini letu bora chini ya Mungu la kutimiza Agizo Kuu katika maisha yetu.
Mathayo 28:19 inaandika amri ya Yesu ya kuyafanya wanafunzi ethnē zote. Na tunajua kutoka Ufunuo 7:9 kwamba kutakuwa na umati mkubwa kutoka kila kabila na lugha na jamaa na ethnē wakimwabudu Mungu mbele ya kiti chake cha enzi. ZOTE. KILA. Hatujui ni lini jambo hili litatokea, lakini tunajua kwamba huu ndio mpango wa Mungu.
Ninatumia neno la Kigiriki ethnē kwa sababu tafsiri ya kawaida “taifa” mara nyingi huwafanya watu wafikirie nchi za kisiasa badala ya mataifa ya kikabila-kilugha. Lakini kuona kanisa likianzishwa katika nchi ya kisiasa hakutoshi.
Nilizaliwa nchini Indonesia, ambapo wazazi wangu walikuwa wamisionari na walihudumu wakati wa harakati ya ajabu ya Mungu mwaka 1966-68, wakati inakadiriwa kwamba Waislamu milioni mbili wa Kijava waliingia kanisani.1 Miaka mingi baadaye, mimi na mke wangu tulikuwa tukiomba kuhusu wito wetu wa umisheni. Mungu alitaka twende wapi? Tulihisi msukumo kutoka kwa Mungu kuwahudumia wale walio na hitaji kubwa zaidi la Injili.
Kwa sababu ya mamilioni ya Wakristo wa Indonesia, sikuona haja ya juhudi za uanzilishi huko. Fikiria jinsi nilivyoshangaa kutambua kwamba inakadiriwa Waindonesia milioni 121 walikuwa sehemu ya Makundi ya Watu Wasiofikiwa (UPG) 200+! Mwaka 1996, viongozi wa Indonesia walikusanyika kutafakari hitaji la Agizo Kuu ndani ya Indonesia. Hatua kubwa za ushirikiano zilipigwa katika maombi, utafiti na uhamasishaji. Ndani ya miaka mitano tu, idadi ya UPG za Indonesia zilizokuwa zikihudumiwa na watenda kazi wa Injili iliongezeka kutoka 21 tu hadi zaidi ya 100! Juhudi za ajabu na za kujitoa mhanga zilifanywa katika karne zilizotangulia na miaka iliyofuata 1996, lakini miaka 28 iliyopita kulikuwa na Waindonesia milioni 121 wasiofikiwa na leo kuna Waindonesia milioni 192.5 wasiofikiwa.
Mwaka 1996 na baadaye, msukumo wetu ulikuwa sahihi, shauku yetu ilikuwa kubwa, maombi na uhamasishaji mkubwa ulifanyika, na watu wengi walijitoa mhanga kwa kiasi kikubwa. Lakini tulifanya kosa la msingi. Tulidhani kwamba kutuma watenda kazi kwa makundi haya yote kungeleta matokeo ya kuyafikia. Lakini walio wengi sana kati yetu tulitumia mbinu za kimapokeo kujaribu kuyafikia makundi ambayo kwa karne nyingi yalikuwa ama yanaipinga Injili au yametengwa nayo. Tuliona baadhi ya maeneo yenye mafanikio, lakini kwa sehemu kubwa tulishindwa kuleta athari ya kutosha ili kutoa tumaini la kweli la kuyafikia makundi haya.
Kote ulimwenguni, kumekuwa na ongezeko la umakini kwa wasiofikiwa katika miaka 30 iliyopita. Lakini matokeo si bora zaidi. • Bilioni 2.25 (28%) ya watu wa dunia hawana fursa ya kuifikia Injili.2 • Bilioni 3.37 (42.5%) ya watu wa dunia ni washiriki wa Makundi ya Watu Wasiofikiwa 7,415 ya dunia3. • Ni 18.3% tu ya wasio Wakristo wanaomfahamu Mkristo binafsi,4 na kama mwelekeo wa sasa ukiendelea, hilo litaongezeka hadi 20% tu ifikapo 2050! Watasikiaje pasipo mtu kuwaambia? Na tatizo ni tata zaidi kuliko ukweli huu tu.
Tatizo #1: Tunahitaji kuhesabu kwenda juu kabla hatujaweza kuhesabu kurudi nyuma.
Hatari moja miongoni mwa baadhi ya wanaofikiri kuhusu Agizo Kuu ni shauku ya kuhesabu kurudi nyuma. Tunataka kubaini idadi ya makundi yanayohitaji kufikiwa, kisha kuyafuta katika orodha yetu—kwa kuzingatia vigezo fulani vya shughuli badala ya matokeo. Lakini lengo letu ni Injili kwa kila mtu na makanisa yanayozaana ambayo yanajaza na kubadilisha kila jamii ndani ya kundi hilo la watu/ lugha/kabila/ethnē.
Karibu kwa hakika tuna sehemu nyingi zaidi ya UPG 7415 tu za kufikia. Baadhi ya wanamikakati wanakadiria kuhitajika kwa juhudi ya harakati kwa kila sehemu ya watu 100,000. Kuanzisha kazi moja kwa kila sehemu ya watu 100,000 miongoni mwa watu bilioni 3.37 wa Makundi ya Watu Wasiofikiwa kungekuwa angalau sehemu 33,700. Unapoongeza kwenye “makundi ya watu” “maeneo” yao (kama vile wilaya 43,000 za dunia), ongezeko la utata linatisha. Ikiwa kila wilaya ina wastani wa sehemu tatu, hiyo inaweza kuwa maeneo 120,000 yanayohitaji harakati.
Jibu: Harakati zinatiririka kuingia katika makundi mengi ya watu na maeneo yanayowazunguka. Kwa vinasaba vya kila mwanafunzi kuwa mfanya-wanafunzi na ukaribu wa kitamaduni na makundi ya watu wanaowazunguka, wao wanafaa zaidi sana kuwafikia.
Tatizo #2: Baadhi ya makundi ya watu yanayoonekana kuwa “moja” kwa kweli ni makundi mengi (ni wafeli wenye vyumba vingi, si chapati bapa).
Yesu hakutuambia tuwafanye wanafunzi watu wachache mmoja mmoja, bali tuzifanye wanafunzi ethnē nzima. Neno la Kigiriki ethnos (umoja wa ethnē) linafafanuliwa kama “kundi la watu walioungana kwa ukoo, utamaduni, na mapokeo ya pamoja, taifa, jamaa.”5 Ufunuo 5:9 na 7:9 zinakamilisha picha ya ethnē zitakazofikiwa, zikiongeza maneno mengine matatu ya kufafanua: makabila, jamaa, na lugha—makundi mbalimbali yenye utambulisho wa pamoja.
Katika uharaka wetu wa kurahisisha kazi, kwa ajili ya uhamasishaji na mkakati, tumepoteza baadhi ya hekima kutoka kwa waanzilishi wa mwanzo wa dhana ya wasiofikiwa. Kikosi kazi cha Lausanne 1982 kuhusu makundi ya watu kilisema: kwa madhumuni ya uinjilisti ni “kundi kubwa zaidi ambamo Injili inaweza kuenea kama harakati ya kupanda makanisa bila kukutana na vizuizi vya kuelewa au kukubalika.”6
Huu hapa ni mfano mmoja mahususi. Katika miaka ya 1990, timu ya utafiti iliyoongozwa na Marvin Leech iligundua kwamba kundi la watu la Jawa (Wajava), ambalo lilikuwa na mamilioni ya waamini na lilihesabiwa kama kundi moja kubwa la watu “waliofikiwa,” karibu kwa hakika lilikuwa angalau makundi manane tofauti ya watu kwa ufafanuzi wa Lausanne. Matatu kati ya makundi haya yalikuwa na kati ya 7–10% Wakristo wa kiinjili wakati matano kati yake yalikuwa na Wakristo chini ya 1%. Bila shaka, vizuizi vilikuwepo kati ya Jawa Negarigung wenye Wakristo 10% na Jawa Pesisir Lor wenye Wakristo 0.1%. Kuwahesabu kama kundi moja la watu la Jawa kulipuuza sana yale makundi matano yaliyokuwa hayajafikiwa.
Jibu: Tumeona harakati zikianza katika UPG zote tano za Jawa katika miaka 10 iliyopita. Zilianzishwa na vichocheo vya harakati wenye asili ya Kiindonesia na Kijava. Juhudi kubwa zaidi sana zinahitajika ili kuwafikia watu wa Jawa milioni 100+, lakini huu ni mwanzo unaotia moyo sana. Pia jambo lenye umuhimu mkubwa ni kwamba harakati hizi za Jawa na watendaji wengine wa harakati wanawafikia wengine na wameanza kuzidisha wanafunzi na makanisa, wakiwa na harakati katika UPG 30+ na baadhi ya matunda ya kabla ya harakati katika UPG nyingine 40+. Mienendo hii hii inatokea kote ulimwenguni! Utasoma mifano mingine yenye kusisimua katika sehemu iliyobaki ya toleo hili.
Tatizo #3: 2% huenda ni kiwango cha chini mno.
Historia ya neno “wasiofikiwa” inaonyesha kwamba kabla ya 1980, 20% ilionekana kuwa mstari uliokubalika kati ya waliofikiwa na wasiofikiwa. Kisha katika miaka ya 1980, takwimu mbalimbali kama vile 5%, 10%, 20% zilianza kusambaa.
Mwaka 1995, kamati iliyowakilisha Operation World, Adopt-a-People, IMB, SIL, na AD2000 ilifanya uamuzi wa kuchagua vigezo “vya kiholela kwa kiasi fulani” vya chini ya 2% Wakristo wa kiinjili na 5% Wanaokiri Ukristo.7
Dave Datema anasema “hakuweza kupata utafiti au uchunguzi mwingine wowote wa kuunga mkono uchaguzi wa 2% ya Wakristo wa kiinjili kama kigezo” wala hakuweza kupata “utafiti wa kuhalalisha” matumizi ya 5%.”8
Inavutia kwamba Patrick Johnstone anaandika mwaka 2011 kwamba wanasosholojia wengi huchukua 20% kama kiwango ambacho sehemu ya jamii huanza kuathiri mtazamo wa ulimwengu wa jamii pana zaidi.9
Mwaka 2011, utafiti kutoka Rensselaer Polytechnic Institute uligundua kwamba “hatua ya mabadiliko makubwa” (tipping point) kwa kuenea kwa haraka kwa mawazo ilikuwa 10%. “Mara idadi hiyo inapopita asilimia 10, wazo huenea kama moto.”10 Huenda tunapaswa kufungua upya mazungumzo kuhusu asilimia na kuzingatia ushahidi wa sasa katika kufanya uamuzi huu.
Jibu: Harakati si nzuri tu katika kuanza; zina nguvu sana katika kudumisha juhudi. Baadhi ya harakati zinaona vizazi 15, 20, hata 30. Mara harakati inapofikia vizazi vinne katika mikondo mingi, kuna uwezekano mkubwa sana kwamba itaendelea kuzaana na kufikia kwa ufanisi sehemu na sehemu ndogo za kundi au makundi yao ya watu.
Tatizo #4: Msisitizo uliopitiliza juu ya makundi ya kikabila-kilugha
Nimekuwa mtetezi mwenye shauku wa kulenga UPG. Lakini tunapaswa kukiri kwamba wengi wetu tumelenga karibu kabisa makundi ya kikabila-kilugha, bila kuzingatia kwa kiasi kikubwa makundi ya kikabila, ya lugha, ya kitamaduni, ya kiukoo na makundi mengine mengi.
Fikiria ukweli kwamba makundi ya watu hayajatengwa katika nchi moja ya asili iliyo safi na yenye watu wa aina moja. Yanazidi kuchanganyika na makundi mengine. Ndiyo sababu Muungano wa 24:14 una maono ya harakati katika kila kundi la watu wasiofikiwa na kila mahali pasipofikiwa.
Mfano ulio dhahiri zaidi ni majiji. Kuna “majiji makubwa mno 593 ambayo wengi wa wakazi wake si Wakristo”.11 Justin Long anasema kwamba utata wa ajabu wa majiji “unamaanisha kwamba kujumuisha ‘majiji’ kama sehemu za kuorodheshwa, kulengwa, kuelezwa, kutafitiwa, kuandikwa, kufuatiliwa, kupimwa, na kuanzishiwa kazi kimkakati yaelekea ni muhimu sawasawa na ‘makundi ya watu wasiofikiwa.’”12
Jibu: Harakati zinazidi kulenga kuyafikia majiji na sehemu za kijiografia, pamoja na sehemu za kikabila-kilugha. Makala kadhaa katika toleo hili zinatoa mifano ya hili.
Tatizo #5: Kushindwa kwa Kanisa13
• Kanisa lina takriban mara 3,000 ya rasilimali za kifedha na mara 9,000 ya nguvu kazi inayohitajika ili kukamilisha Agizo Kuu. • Wakristo wa kiinjili wangeweza kutoa fedha zote zinazohitajika kupanda kanisa katika kila moja ya makundi ya watu wasiofikiwa 7,400, kwa 0.03% tu ya mapato yao. • Kila mwaka, tunatumia dola bilioni $52 kwa umisheni wa aina yoyote. Wakati huo huo dola bilioni $59 hupotea kwa wizi unaofanywa na washiriki wa makanisa. Jibu: Mungu anafanya jambo jipya! Harakati hizi ni mafanikio mapya kabisa kutoka kwa Mungu, yenye mifumo ya miaka 2,000. Kanisa la ulimwenguni kote lina fursa ya kujiunga na tendo hili jipya la Mungu. Mungu anaanzisha mito jangwani, kwa kuwa harakati zenye matunda zaidi zinakua katika mengi ya makundi ya watu na maeneo ambayo (hapo awali) yalikuwa magumu zaidi na yaliyofikiwa kwa kiasi kidogo zaidi duniani. Sehemu iliyobaki ya toleo hili inaonyesha njia kuu ambayo Mungu anaonekana kuitumia kuwafikia wasiofikiwa.
Katika makala iliyo katika toleo hili: “How Long to Reach the Goal?,” Justin Long anaandika kwamba tangu 1995, harakati zimekua kwa “wastani wa kiwango cha ukuaji cha kila mwaka cha 23%, au idadi ya waamini ikiongezeka mara mbili kwa wastani kila miaka 3.5.” Hilo ni tofauti kabisa na wastani wa kiwango cha ukuaji cha 1.18% cha Ukristo duniani katika miaka 20 iliyopita, au hata ukuaji wa 1.8% wa Wakristo wa kiinjili na 1.89% wa Wakristo wa Kipentekoste.
Ukuaji huu wa 23% kimsingi ni wa ndani, kadiri harakati zinavyowafikia watu wao wenyewe. Na hata hivyo, wanapotafuta kuwafikia watu wa makundi yao wenyewe ambao hawajafikiwa kwa hali ya kukata tamaa, wanafunzi hawa wa harakati mara nyingi husukumwa na Roho kuvuka mipaka yao ili kuwafikia makundi mengine ya watu na maeneo mengine yaliyo karibu.
Kwa sasa tunajua kuhusu: • CPM 1,967 • harakati changa 1600+, zenye matunda ya kizazi cha 2 na cha 3 • maeneo mengine 2000+ ambapo kazi ya harakati imeanzishwa. Jambo la kuzingatia ni kwamba CPM za mwanzo 200+ zimeanzisha takriban CPM na CPM changa 3,300! Tunaweza kuanza kuona jinsi kuanzisha kazi ya harakati 33,700 au hata 120,000 kunavyoweza kuwezekana.
Mungu Muumba wetu anapenda utofauti. Kwa hiyo ingawa tunaweza kutambua kanuni zinazofanana, kila hadithi ya harakati inayoanzisha harakati nyingine ni ya kipekee. Jifunze kutoka katika mifano ifuatayo ya Injili ya Mungu inayotiririka, kadiri harakati zinavyoanzisha harakati.
Unaposoma, mwulize Mungu jinsi unavyoweza kujihusisha. Kisha soma makala ya kuhitimisha, “What Must be Done?” kwa baadhi ya mawazo mahususi ya kuchochea fikra zako.
Stan Parks, Ph.D. anahudumu katika Muungano wa 24:14 (2414now.net) pamoja na Beyond (beyond.org). Yeye ni mkufunzi na kocha kwa Harakati mbalimbali za Kupanda Makanisa duniani kote, na yeye na mke wake Kay wameishi na kuhudumu miongoni mwa wasiofikiwa tangu 1994. Tazama tangazo kwenye jalada la nyuma kuhusu 24:14—A Testimony to All Peoples, kilichohaririwa na Stan Parks na Dave Coles. Matoleo ya kielektroniki yanapatikana bure katika lugha kuu 11 katika 2414now.net/resources. Nakala za karatasi na Kindle zinapatikana Amazon.
Maelezo
- Willis, Avery T. 1977 Indonesian Revival: Why Two Million Came to Christ. Pasadena: William Carey Library Publishing. Rudi kwenye maandishi
- www.gordonconwell.edu/center-for-global-christianity/wp-content/uploads/sites/13/2022/01/Status-of-Global-Christianity-2022.pdf Rudi kwenye maandishi
- Kwa ufafanuzi wa Joshua Project wa makundi ambamo Wakristo wa kiinjili ni <= 2%; Wanaokiri Ukristo ni <= 5% Rudi kwenye maandishi
- www.gordonconwell.edu/center-for-global-christianity/wp-content/uploads/sites/13/2022/01/Status-of-Global-Christianity-2022.pdf Rudi kwenye maandishi
- Danker, Frederick William. 2000 A Greek-English Lexicon of the New Testament and Other Early Christian Literature, toleo la tatu, kwa msingi wa Walter Bauer na matoleo ya awali ya Kiingereza ya W.F. Arndt, F.W. Gingrich, na F.W. Danker. Chicago na London: University of Chicago Press, 276. Rudi kwenye maandishi
- www.missionfrontiers.org/issue/article/unreached-peoples Rudi kwenye maandishi
- Datema, Dave. 2016 “Defining Unreached: A Short History”. International Journal of Frontier Missiology 33:2, 55-60. www.ijfm.org/PDFs_IJFM/33_2_PDFs/IJFM_33_2-Datema.pdf. Rudi kwenye maandishi
- Ibid., 60-61. Rudi kwenye maandishi
- Johnstone, Patrick. 2011 The Future of the Global Church (Colorado Springs, CO: Global Mapping International), 224. Rudi kwenye maandishi
- Xie, J., et. al. 2011 “Minority Rules: Scientists Discover Tipping Point for the Spread of Ideas,” news.rpi.edu/ luwakkey/2902. Makala ya asili inapatikana katika: www.cs.rpi.edu/~szymansk/papers/pre.11.pdf. Rudi kwenye maandishi
- Long, Justin. 2021 “Urbanization and Measuring the Remaining Task.” Mission Frontiers, Sept/Oct, 30-31. Rudi kwenye maandishi
- Ibid. Rudi kwenye maandishi
- Takwimu zifuatazo zimetoka www.thetravelingteam.org/stats. Rudi kwenye maandishi
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 45:1 (Jan./Feb. 2023), uk. 8-11. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


