Kukaa mbali kijamii na kujitenga kunakohusiana na COVID-19 kulileta changamoto kubwa kwa Harakati za Kufanya Wanafunzi (DMM) kote ulimwenguni kwa sababu harakati hustawi kwa mwingiliano wa kibinafsi unaoendelea na wa karibu sana. Lakini Bwana alitutia moyo kwamba kila hali ya dharura ina fursa ya ufalme iliyofichika ndani yake. Kwa muda mrefu tumeamini kwamba kuwasaidia watu wanaoumia ni sehemu ya kuwa wanafunzi na pia ya kufanya wanafunzi. Kutumia kanuni hii kwa njia mpya kulionyesha kwamba ufalme bado unaweza kustawi katikati ya habari mbaya mno.
Katika Afrika Mashariki, tulikabiliwa na dhoruba kamili iliyokuwa zaidi ya COVID-19 tu. Kabla ya COVID tulikuwa na ukame mkali katika sehemu nyingi za Kaskazini mwa Kenya na maeneo mengine ya Afrika Mashariki. Kisha mwezi Oktoba 2019, tulikumbwa na mvua kubwa na mafuriko makali ndani ya muda wa wiki moja. Kati ya ukame na mafuriko, kila kitu kiliathirika kwa sababu sehemu kubwa ya makundi ya watu ni wafugaji wahamaji. Wanyama wowote waliobaki baada ya ukame waliuawa na mafuriko.
Kisha mwezi Desemba, tulianza kuona nzige kwa mara ya kwanza maishani mwetu. Nzige walikuja na kuharibu mimea iliyobaki, chakula cha wanyama na hata mashamba.
Kuelekea mwisho wa Februari 2020, COVID-19 ilitufikia, na katikati kabisa ya shughuli za harakati ukaja mfululizo huu wa changamoto. Kufikia mwanzoni mwa Machi hali ilikuwa ya kuvunja moyo sana kwa viongozi wetu wengi. Serikali ya Kenya ilikuwa ikifunga nchi. Wakati huo nilikuwa nimesafiri hadi sehemu ya kaskazini ya nchi na nikakwama huko kwa sababu ya amri ya kufunga nchi (lockdown) kuanzia Machi hadi Agosti.
Mojawapo ya changamoto ilikuwa kwamba hatukuweza kusafiri kwenda sehemu nyingine za nchi; hatukuweza hata kuingiliana na watu. Tukaanza kufikiri, “Tutaitikiaje hali hii? Tunahitaji njia mpya za kufanya huduma, ili tuweze kuwafikia watu.” Tulikuja na njia tatu za kuitikia.
Mwitikio wetu wa kwanza ulikuwa maombi. Katikati ya Machi tuliwaita washiriki wote wa timu yetu kuomba: timu yetu ya msingi na viongozi wetu wa nchi, wakiwakilisha nchi zote tunazofanyia kazi. Sote tulianza kuomba kwa wakati mmoja, tukitumia WhatsApp kusambaza maombi. Tuliomba kwamba Mungu aidumishe harakati, kwa sababu tuligundua kwamba viongozi na familia walikuwa ghafla wakipoteza vyanzo vyao vyote vya mapato. Maombi yalikuwa muhimu sana kwetu ili kudumisha kasi. Sote tulianza kuomba, hasa siku za Jumanne na Alhamisi, na tukatangaza kufunga siku za Jumatano. Ilikuwa siku nzima ya kufunga kila wiki, jambo ambalo bado linaendelea hadi leo.
Pili, tulisema, “Tutaingiliana na timu yetu kwa njia zinazowatia moyo, kwa sababu kila mtu anapitia hali hii.” Tulianza kutuma jumbe fupi na tukawapangia viongozi nchi na kanda zao na tukaanza kuwatia moyo kwa Maandiko na kuwauliza, “Hamjambo? Mnapitiaje hali hii? Mnafanya nini ili kusaidia?” Tulijua kwamba kama viongozi wetu hawangetiwa moyo, hilo lingeathiri kasi ya harakati. Kwa hiyo, tulitenga siku za Ijumaa kwa ajili ya kuwapigia simu viongozi wetu ili kuwatia moyo. Waliowapigia simu walikuwa watu ambao viongozi hao hawakuwatarajia. Wangepokea simu kutoka kwa mtu ambaye hakuwahi kuwapigia simu hapo awali. Sababu ya kupiga simu ilikuwa kusema tu, “Tuko pamoja nawe katika hali hii na tunataka kukutia moyo.” Hilo kwa kweli lilitusaidia kubaki pamoja.
Kisha mwezi Aprili tulianza kuwa na mikutano ya Zoom siku za Jumanne na Alhamisi pamoja na timu yetu yote. Katika mikutano hiyo tulijadili hali ilivyo, jambo lililosaidia kudumisha mtiririko wa mawasiliano. Tulipoanza kutumia Zoom, tulianza kukaribiana zaidi kwa kuonana na kusikilizana.
Tatu, tulisema, “Lazima kuwe na njia za kivitendo za kuwafikia watu wakati wa hali hii ya dharura. Tunawezaje kudumisha kile kilichoanzishwa?” (Tuko katika hatua ya kudumisha harakati. Tulitoka katika kuanzisha na kuzidisha hadi kudumisha.) Sehemu ya kuwadumisha viongozi, vikundi na makanisa ilikuwa kusaidia kuhusu mapato ya wapanda makanisa waanzilishi kwa kuwa mapato yao yalikuwa yametoweka. Tuliuliza, “Tunawezaje kuwasaidia kupata chakula? Familia nyingi zimeishiwa na chakula; hawawezi kupata chakula kwa sababu Nairobi imefungwa, na bidhaa zetu zote zinazokwenda sehemu mbalimbali hutoka huko.” Hili lilileta jambo jipya. Tulianza kuona ukarimu wa wanafunzi; walianza kushirikiana vitu vidogo walivyokuwa navyo kwa upendo wa kivitendo. Katika hatua hii haikuwa suala la kiasi gani ungeweza kushiriki, ilikuwa tu kushiriki kile kidogo ulichokuwa nacho.
Majirani walianza kuwapa majirani zao. Tulianza kuona vikundi vikizaana kwa sababu ya wema wa kivitendo ambao wanafunzi wao walikuwa wakiuonyesha. Tulianza kupokea hadithi za ajabu za watu waliokuwa na chakula cha kutosha tu kwa familia zao wenyewe, labda kwa wiki moja, lakini walianza kushiriki na familia ambazo hazikuwa na chochote. Na kwa sehemu kubwa, wale waliowashirikisha walikuwa majirani zao Waislamu. Upendo huu, ulioonyeshwa wakati ambapo kila mtu alikuwa akipitia changamoto zile zile ngumu, uliwasaidia watu kufunguka ili kusikia Injili.
Mwezi Mei na Juni, tulianza kuomba msaada. Msaada uliingia kidogo kidogo na kufikia Desemba tuliweza kulisha familia zaidi ya 13,500 (familia katika muktadha wetu ina wastani wa watu wanane). Kupitia hili, kila moja ya familia hizo ilikuwa ikizidisha makanisa.
Tulifanya uchambuzi na kuandaa ripoti mwezi Desemba, tulipofika mwisho wa mwaka. Tuligundua kwamba kupitia watu kushiriki kwa makusudi—si Injili tu, bali pia kushiriki upendo—tuliona kuzaana kwa vikundi na makanisa. Makanisa yoyote yaliyokuwa yakitegemea kukutana katika jengo la kanisa hayakuweza kukutana humo. Kwa hiyo, watu walianza kukutana majumbani, na mikutano ya majumbani ikaanza kuzaana. Katika eneo hilo, nyumba ni ndogo sana; hazingeweza kuwatosha watu wengi. Kwa hiyo, mikusanyiko ya majumbani ikaanza kujigawa katika nyumba nyingi. Matokeo yake, majirani zaidi, watu zaidi, na Makundi ya Watu Wasiofikiwa (UPG) zaidi walifikiwa.
Niliangalia kilichotokea katika miaka 15 iliyopita ya harakati yetu katika Afrika Mashariki, na 2020 ulikuwa kilele. Tuliona makanisa 1,300 yakipandwa katika mwaka huo mmoja tu. Hili lilikuwa la ajabu kwa sababu mapema mwaka huo, tulikuwa tumepunguza malengo yetu kwa 30%; tulisema tutamwamini Mungu kwa makanisa mapya 600 hadi 800. Lakini Mungu alitupeleka mbali zaidi ya hapo, kama yeye pekee awezavyo kufanya. Sikuweza kuamini, timu zote zilipowasilisha data zao za mwaka. Ilinibidi nione michoro ya takwimu na kuangalia mimi mwenyewe kundi la watu baada ya kundi la watu.
Mungu alifanya hili kupitia kile tunachokiita pembetatu ya kufanya wanafunzi: kumpenda Mungu, kumpenda jirani yako na kufanya wanafunzi. Upendo wa kivitendo uliweza kufungua mioyo ya watu ili waitikie Injili kwa njia chanya. Kazi ilianzishwa miongoni mwa makundi mapya ya watu, maeneo mapya yalifunguka na tunaendelea na hilo. Nimetoka tu katika kukutana na waratibu 40 ambao wameanza kulichakata hili ili kubaini jinsi ya kujenga juu ya kasi hii kwa mwaka huu na miaka ijayo.
Nafasi ya Kujifunza Teknolojia Mpya
Kabla ya COVID-19, wengi wetu katika muktadha wetu (nikiwemo mimi) hatukujua kutumia teknolojia ya habari (TEHAMA). Kila kutajwa kwa kutumia Zoom kwa ajili ya mkutano kulikutana na upinzani mwingi kuhusu kasi ya intaneti. Nilikuwa nimejaribu mikutano miwili mitatu ya Zoom, ilibidi mtu anipigie simu na kunipa maelekezo ya jinsi ya kufanya. Hata kujua jinsi ya kuwasha kipaza sauti katika zoom kulikuwa kugumu sana. Wakati wa mkutano wa kwanza tuliofanya ungeweza kusikia kila aina ya sauti chinichini. Kulikuwa na kelele nyingi, lakini angalau tuliweza kuona nyuso za kila mmoja na hilo lilisisimua. Tulianza kujifunza majukwaa kama Zoom, WhatsApp na mengineyo. Kwa sababu ya COVID tuliushinda upinzani huo, licha ya changamoto.
Nilikwama kwa miezi kadhaa kaskazini mwa Kenya ambako intaneti ilikuwa mbaya mno. Nakumbuka siku ya kwanza ya mafunzo ya msingi ya DMM. Tulikuwa na watu wapatao 130 wakijiunga kutoka kote ulimwenguni, na ghafla intaneti yangu ikaacha kufanya kazi. Sikuweza kupata mtandao wowote kabisa. Kwa hiyo, niliingia garini mwangu na kuanza kuzunguka, nikitafuta mtandao kwenye simu yangu. Hatimaye, katika kiwanja kidogo cha ndege, nilipata mtandao pekee uliopatikana katika mji mzima. Watu walinikodolea macho, wakifikiri: “Huyu mtu kichaa anafanya nini na kompyuta katika uwanja wazi?” Ilikuwa aibu lakini nilikuwa tayari kuifanya. Kufikia wakati mtandao uliponiwezesha kuunganika tena, watu walikuwa tayari katika majadiliano, lakini walifurahi kwamba niliweza kurudi. Nilijisikia vibaya sana, kwa sababu hii ilikuwa siku ya kwanza ya mafunzo, lakini tulifanya kile tulichoweza ili kujifunza na kuwa wabunifu na kutafuta njia mpya za kuunganika.
Tulianza kurekodi mafundisho na kuyatuma kwa timu zetu. Tuliweza kufanya Usomaji wa Biblia kwa Kugundua (UBK) pamoja na viongozi wetu wote wa nchi au waratibu wetu wote kwenye jukwaa moja. Tulipoanza kutumia Zoom, kwa kweli tuliendelea kukua. Tulianza wiki tisa za mafunzo ya msingi ya DMM pamoja na watu 115 kutoka kote ulimwenguni. Tulikuwa na watu kutoka India, Sri Lanka, Indonesia, Amerika Kusini na kila mahali. Watu ambao hatukuwahi kukutana nao waliendelea kwa wiki zote tisa na tuliendesha makundi ya mafunzo, ambayo baadhi yake bado yanaendelea.
Tulikuwa na mashirika mengi ya umisheni na timu za kimataifa zilizoleta walio wengi kati ya wamisionari wao kwa ajili ya kozi za mafunzo za ngazi ya kwanza, mafunzo ya ngazi ya pili na madarasa ya uongozi. Hilo liliendelea kupanuka mbali zaidi ya Afrika Mashariki. Mungu aliitumia COVID-19 kutuunganisha na wengine na kuwa baraka kubwa zaidi kwa mwili wa Kristo ulimwenguni kote kupitia mafunzo yetu.
Tunaendesha Kambi ya Kimataifa ya Vichocheo vya DMM kila mwaka. Mwezi Oktoba, tulisema, “Kwa nini tusijaribu kufanya hili kwa njia ya mtandao?” Hatukujua ingekuwaje, lakini tulikuwa na watu kutoka nchi 27 waliojiunga nasi kwa siku tatu za kambi ya vichocheo. Hizo ni baadhi ya njia za ajabu ambazo Mungu alitumia teknolojia kupanua mipaka ya huduma yetu.
Natarajia matumizi haya makubwa zaidi ya teknolojia yataendelea. Hatuangalii nyuma. Bado tunapendelea kukutana ana kwa ana kwa ajili ya ukocha na mahusiano ya mahali hapo. Lakini njia ya kusonga mbele ni kutumia teknolojia mpya ili kuwafikia watu ambao hatungeweza kuwafikia kwa njia za kimapokeo. Kwa mfano, wiki iliyopita nilianza kutoa ulezi kwa kikundi cha vichocheo vya DMM siku ya Alhamisi kwa saa moja. Si mimi ninayefundisha, ninawezesha tu. Ningewezaje kutofanya hivyo, sasa kwa kuwa Mungu ametoa chombo hiki? Zamani niliweza kukutana na watu walio Kenya tu au katika eneo letu. Sasa ninazungumza na timu katika India Kaskazini na kutoa ukocha kwa timu katika Jiji la Panama—maeneo ambayo sijawahi kufika. Tumejifunza kupitia haya yote kwamba tunahitaji kuwa wabunifu na kutumia kila fursa (ikiwemo majukwaa na teknolojia mpya) kwa ajili ya kupanua ufalme wa Mungu.
Masomo Mawili Tuliyojifunza, Ambayo Tunaweza Kuyabeba Kuelekea Siku Zijazo
Tumejifunza kwanza kwamba nyakati mbaya zinaweza kuleta matokeo mazuri, kwa hiyo hatupaswi kuvunjika moyo kwa sababu ya nyakati mbaya. Mungu ana njia ya kuleta matokeo yake mwenyewe katika nyakati mbaya. Tunamtazama Mungu kwa ajili ya matokeo kwa sababu matokeo yanamtegemea Mungu, si hali zilivyo. Ndiyo sababu hatuziruhusu hali kuondoa kile ambacho Mungu ametupa.
Pili, viongozi wanahitaji kuwa wabunifu katika kukabiliana na changamoto na matatizo. Lakini mwitikio huo unapaswa kutokana na maombi na kumtegemea Mungu kwa sababu Roho Mtakatifu atatuongoza.
Katika kitabu cha Matendo ya Mitume, tunaona kwamba kila mara mitume au kanisa walipokabiliwa na changamoto, mateso au matatizo daima waliomba. Wakati mwingine tunataka kutatua tatizo tunalojua liko juu ya uwezo wetu. Kama viongozi, tunaomba ili kupata mwelekeo kutoka kwa Mungu kwa ajili ya jambo linalofuata au kwa ajili ya njia inayofuata ya kutatua tatizo. Hata katika hali mbaya kabisa, Roho Mtakatifu anaweza kuonyesha njia ya kibunifu ya kusonga mbele.
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 44:3 (Mei/Juni 2022), uk. 40-43. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


