MsimamiziNinavyoelewa, Vyombo vya Habari kwa Harakati maana yake ni kutumia mitandao mbalimbali ya kijamii au vyombo vingine vya habari kuwapata watafutaji, Watu wa Amani, na kuwaingiza katika mkondo wa kuwa wanafunzi wanaozaana na wafanya-wanafunzi. Vyombo vya Habari kwa Harakati vimefanikiwaje katika eneo lako? Vimefanyaje kazi?
GPNingependa kuanza na hadithi za mafanikio, lakini ukweli ni kwamba baadhi ya mambo hayafanyi kazi kabisa. Nilikuwa nikifanya kazi na huduma kubwa iliyotumia intaneti kuyafikia mataifa. Tulianzisha kampeni ya kuwafikia watu katika sehemu maalum ya eneo la Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini (MENA). Nakumbuka siku moja niliona majibu kutoka kwa machapisho ya Facebook na video kadhaa kwenye YouTube. Nilipoona majina na maoni yao yote kwa Kiarabu, nilizidiwa na wingi wa majibu. Unapofanya kazi na watu mmoja mmoja, umezoea kukutana kama kikundi kidogo. Lakini katika hali hii, niliona mamia, kisha yakawa maelfu. Jambo hilo lilinikosesha usingizi usiku kwa sababu nilijua hatukuwa na miunganisho mizuri uwandani wakati huo—mtu wa kwenda kukutana ana kwa ana na aliyejibu. Kusema, “Uliwasiliana nasi na kuuliza kuhusu Yesu. Tunaweza kukutana kunywa kahawa pamoja na kulizungumzia?”
Huo ulikuwa wakati wa mgogoro maishani mwangu kwa sababu nilihisi tulikuwa mawakili wabaya. Hatukuwa tukimheshimu Mungu, tangu mwanzo hadi mwisho. Kupitia urafiki wangu nilijua kwamba mambo ya ajabu yalikuwa yakitendeka uwandani katika kuzidisha wanafunzi. Wakati huo wa mgogoro ulinisukuma kusema, “Mungu, wewe unafanya nini? Tunaiunganishaje kazi hii yote nzuri inayofanyika mtandaoni na kupitia vyombo vya habari kama redio za AM/FM, televisheni ya satelaiti na redio ya intaneti? Tunawezaje kuunganisha vyombo vya habari vinavyoongozwa na Injili na wanafunzi wanaozaana walio uwandani?”
Kile ninachoona kikitendeka ambacho KINAFANIKIWA ni zile juhudi za ushirikiano za mtandaoni na nje ya mtandao ambapo wafuasi wa Kristo wa mahali hapo huongoza na wafuasi wa Kristo kutoka nje hutoa msaada kadiri unavyohitajika. Kwa mfano, waamini wenye asili ya Kiislamu wanapotengeneza maudhui ya mtandaoni, wakitumia lugha yao na msamiati wao—yanalenga sawasawa. Kisha wanapofanya kazi na wengine ambao huenda wana utaalamu wa matangazo ya Google na kampeni za Facebook, juhudi zao zinakuwa za ushirikiano. Na wanapounganishwa na waamini walio uwandani, ufuatiliaji wa haraka unawezekana. Mtafutaji anapowasiliana na mtu mtandaoni, tunaweza kuwa na uhakika kwamba ndani ya muda mfupi atatembelewa ana kwa ana na mfuasi wa Kristo ndani ya saa chache au siku moja au mbili. Napenda inapofanya kazi hivyo! Ni ushirikiano. Ni watu kutoka mataifa mengi wakifanya kazi pamoja mtandaoni na nje ya mtandao ili kuzidisha wanafunzi.
ChrisNilihudumu Bosnia kwa muongo mmoja kisha nikaanza kutekeleza mkakati wa Vyombo vya Habari kwa Harakati. Katika siku 20 za kwanza, tuliona mwitikio wa kiroho mwingi kuliko tuliokuwa nao katika miaka 10 iliyotangulia ikijumlishwa. Watu walikuwepo huko nje, unapoweka tangazo nchi nzima. Tulikuwa tukipokea ujumbe mwingi zaidi kutoka kwa watu ambao kwa kweli walikuwa wakiota ndoto za Yesu, wakitaka Biblia, na wakitaka kuzungumza. Tulipokuwa tukiunda mfumo huo, tuligundua kwamba ulikuwa unaweza kuzaa tena kwa kiasi kikubwa. Hatimaye tulitoa ukocha na mafunzo kwa timu katika nchi mbili jirani.
Katika moja ya nchi hizo, walianza kuweka matangazo katika majiji matatu ambako walikuwa na timu. Ndani ya miezi tisa ya kwanza, walianza kuweka matangazo katika majiji 16. Waliweza kuwafundisha viongozi walei wa makanisa na wachungaji wapatao 50 kanuni za DMM, kisha kuwafundisha mkakati wa vyombo vya habari na jinsi ya kuwafuatilia wanaowasiliana nao. Katika miezi hiyo tisa ya kwanza, waliona watu wapatao 50 wakimwamini Yesu, na wengine wapatao 250 wakianza aina fulani ya uhusiano wa ufuasi (katika mwaka uliotangulia, walikuwa na watu wanne tu katika uhusiano wa ufuasi.). Hili liliongeza kipengele cha kichocheo: ikiwa neno ni kweli na mavuno yako tayari, hili linatuwezesha kuvuna kwa kasi zaidi, ingawa kasi si lengo. Linapanua tu uwezo.
Jambo lingine lililoletwa ni kile kipengele cha ushirikiano ulichokitaja, GP. Ilikuwa njia laini ya kuzungumza na watu wa makanisa ya kimapokeo kuhusu DMM. Tulikuwa tumejaribu kuwa na mazungumzo hayo, tukijaribu kutekeleza DMM nchini Bosnia na katika eneo la Balkan kwa takriban muongo mmoja. Lakini tulikutana na vikwazo fulani katika kuzungumza na viongozi wa makanisa ya kimapokeo, yaelekea kwa sababu tulikuja kwa nguvu kupita kiasi na kusema mambo yasiyofaa. Lakini jambo hili la vyombo vya habari lilikuwa njia laini ya kufikiria kufanya ufuasi kwa njia tofauti. Na matokeo yalitia moyo sana—kutoka kugusa majiji matatu hadi majiji 16 katika mojawapo ya nchi hizo.
JonNadhani wakati mwingine tunaacha ukubwa wa miguu yetu uamue kile tutakachofanya na ukuaji utakaotokea. Kama msemo unavyosema, tunatengeneza kiatu na hapo ndipo mguu unalazimika kutoshea. Nina kumbukumbu katika shajara yangu ambapo (takriban miaka miwili iliyopita) niliandika maneno haya matatu: kugeuza kuwa bidhaa, ushindani na mkanganyiko. Ninachoona ni kwamba sisi [baadhi ya watu] tunaamini jambo hili ni risasi ya kichawi: unaweka matangazo machache ya Facebook na kudhani utapata harakati. Mimi nina maoni kwamba si suala la vyombo vya habari. Si suala la masoko. Si suala la teknolojia. Ni Roho Mtakatifu akifanya kazi katika maisha ya watu. Mambo hayo yote yanaweza kuwa na sehemu yake, lakini baadhi ya timu zinafanya mambo yote sahihi na hazioni harakati. Nadhani Mungu bado anapendezwa na hilo, na pia nadhani wanahitaji kuwa na kile ninachokiita “ustahimilivu” (grit) ili kuendelea. Inakubidi uendelee kutafuta hadi upate kile kitakachofanya kazi mahali hapo.
Hata hivyo usalama, teknolojia na uwezo wa kuanza kutoka mwanzo kabisa vinazidi kuwa vigumu. Hata hivyo bado inafanya kazi katika maeneo fulani. Mojawapo ya mambo ninayoyathamini ni uwezo wa kuona kinachoendelea duniani kote. Katika maeneo mengine inaonekana kufanya kazi kwa kasi zaidi na kwa ukubwa zaidi kuliko maeneo mengine. Inavutia kwamba maeneo mengi yaliyobaki ambayo hayajafikiwa ni miongoni mwa yale ya polepole zaidi.
Hivi karibuni, tulianza kazi pamoja na watu nchini Bangladesh, tukifanya kazi na watafsiri wa Biblia tangu mwanzo. Maandiko yalitafsiriwa katika lugha hiyo, programu (app) ikatengenezwa, ikitumia maudhui kutoka filamu ya Yesu, filamu ya LUMO (https://lumoproject.com—inapatikana katika Lugha zaidi ya 1,050), na nyinginezo. Tunaona ujumbe mwingi ukiingia. Kisha tunatumia teknolojia kama Echo Global kulinda utambulisho wa wahudumu wanaojibu walioko huko, ambao kisha wanakutana na watu na kuona mambo yakitendeka. Inagharimu senti 0.0004 kwa kila mtu ili kuwafanya watazame karibu sekunde 45 za kipande cha video kutoka filamu ya Yesu. Kwa kweli, kulikuwa na tatizo la kiteknolojia kwa sababu ya tovuti waliyokuwa wakiitumia ambapo ulilazimika kubofya “kubali” ili vidakuzi (cookies) vifanye kazi, hivyo video haikuwa ikifanya kazi. Watu walikuwa wakituma ujumbe, wakisema, “Subiri kidogo! Tunataka kuiona video hii!” Kuna njaa kubwa sana pale ambapo watu hawajawahi kufikiwa na neno la Mungu katika lugha ya mioyo yao.
Usiku mmoja, tulikuwa tukiingia katika baa moja jijini London kula chakula cha jioni, na mtafsiri wa Biblia akaniambia, “Nimekuwa nikiomba kwa miaka 60 ili jambo hili litokee, [na sasa linatokea] kwa sababu mna mashirika mengi na watu wakifanya kazi pamoja ili kuona jambo hili likitendeka.” Wanajua kwamba si bidhaa ambayo unachomeka tu na kuanza kutumia. Si mashindano. Ni kukamilishana, na haileti mkanganyiko bali inaleta mafanikio makubwa na ufahamu mpya.
Kwa sasa tunaendesha kampeni katika nchi moja ya Afrika Kaskazini, ambapo kwa wastani watu 30,000 wanaingia kwenye tovuti kila siku mbili na kubofya ili kuona maudhui zaidi. Hilo huchujwa kupitia kurasa kadhaa tofauti kabla hata hawajaanza kutuma ujumbe. Ubora wa ujumbe huo kutoka kwa watafutaji unazidi kuwa juu. Kama ningechagua jambo moja, lisingekuwa Facebook na lisingekuwa Tik-Tok au aina fulani ya video. Lingekuwa Maandiko tu: Neno la Mungu. Nadhani hapo ndipo Roho anafanya kazi kwa njia zenye nguvu. Katika baadhi ya maeneo haya magumu ambapo timu zimekuwa zikiweka matangazo kwa muda mrefu na bado hazijaona mafanikio makubwa, bado wanaona watu wakifikiwa na ujumbe na wanakutana na watu. Ni kwamba tu bado hakujatokea mambo ya aina ya harakati kamili. Kuna ushindani mwingi, gharama na changamoto za kiufundi ni kubwa, lakini kwa sasa ningependekeza njia hii kwa mtu yeyote. Inashangaza unapoangalia hata watu 1,000 ambao wametazama kipande cha kitu fulani au wamepata neno la Mungu mikononi mwao kwa dola $20 ukilinganisha na njia nyingine yoyote. Nilikuwa mpanda makanisa nchini Taiwan kwa miaka mingi pamoja na timu yangu. Kwa $20, hakukuwa na kitu chochote ambacho ningeweza kufanya kimwili kupata ukubwa, kasi na upana ambao tunaweza kuupata sasa hivi, kwa kutumia teknolojia na vyombo vya habari.
MsimamiziNinawasikia nyote mkisema kwamba imekuwa changamoto kutoka kwenye mwitikio wa vyombo vya habari tu hadi harakati kamili. Lakini iwe tunaona harakati kamili au la, tunaona kiwango cha maji kikipanda. Tunaona watu wengi wakifikiwa na Maandiko, na hilo linaathiri jamii nzima iwe tunafikia harakati kamili mara moja au la. JLA, naomba nikuulize: “Katika siku hizi, unaona ni matumizi gani bora ya mkakati huu wa Vyombo vya Habari kwa Harakati? Ni maeneo gani ambapo watenda kazi yaelekea wataona faida nzuri ya uwekezaji wao wa muda na huenda pia wa fedha?”
JLANinafikiria majukwaa. Duniani kote, majukwaa maarufu zaidi ni Facebook na Instagram, hata katika nchi tunayoilenga huko Afrika Kaskazini. Idadi ya kutisha ya watu hutumia saa nyingi sana kwenye jukwaa hilo. Kwa maoni yangu, hayo ndiyo yenye zana kuu zinazoweza kuwezesha kuunda ujumbe na kuufikisha ujumbe kwa mtu sahihi. Majukwaa mengine yanawezekana, lakini hayajaendelezwa sana.
MsimamiziKuna mtu mwingine anayetaka kutoa maoni?
GPNdiyo, tunataka kuwafikia watu wengi zaidi kwa haraka zaidi lakini pia kwa ufanisi zaidi, ili kwa kweli tuwe tunafanya wanafunzi na kuwazidisha ili kuona harakati. Mahali ambapo tumeona mafanikio makubwa zaidi ni katika kutumia Instagram na Facebook na kidogo kwenye YouTube, lakini si kwa kiasi hicho. Jon alikuwa sahihi kabisa aliposema baadhi ya mambo yanafanya kazi na mengine hayafanyi.
Sisi kama mwili wa Kristo, tumekuwa wazembe mno kwa kudhani kwamba ujumbe tunaouweka kwenye Instagram au Facebook kwa kweli unawafikia walengwa waliokusudiwa. Ikiwa hatutumii lahaja au lugha sahihi, hatutumii msamiati sahihi au, inapokuwa ni ya kuona, rangi, picha na michoro sahihi—mambo hayo yote yanazungumza—na yatawafikia walengwa wetu au kuwakosa kabisa.
Tunaposisitiza Maandiko na kuufanya ujumbe uwe wa mahali husika, hapo ndipo tunaungana na Mungu. Anaongeza njaa ya kiroho kote duniani. Kwa sisi tuliofanya kazi miongoni mwa Waislamu kwa miongo kadhaa, inafurahisha sana kuona kinachotokea sasa. Miaka thelathini iliyopita, tulifurahi sana tulipoona Mwislamu mmoja au wawili kwa mwaka wakiota ndoto kuhusu Yesu na kutaka kumfuata.
Lakini kinachotokea sasa ni mamia kila wiki na maelfu kila mwaka. Kwa kweli tunaona mamilioni ya Waislamu waliokombolewa wanaomfuata Yesu sasa. Kwa hiyo, Jon, nashukuru kwa kusema kwamba si suala la vyombo vya habari. Si suala la mbinu. Ni suala la kuungana na Mungu. Ikiwa tumejipanga pamoja na Mungu, atatuonyesha njia bora za kutumia vyombo vya habari na teknolojia ili kuzidisha wanafunzi.
MsimamiziJon, ni mtu au huduma ya aina gani ambayo ingekujia na kusema, “Nahitaji msaada wako. Ninapenda kuanza na Vyombo vya Habari kwa Harakati”? Ni matatizo gani ambayo mtu huyo anajaribu kuyatatua, na ungeweza kusema, “Ndiyo, naweza kukusaidia”?
JonNaomba niongeze maoni yangu kidogo kuhusu ile mada nyingine, kisha nitajibu hili. Kuna vyombo vya habari vya kusukuma (push) na vyombo vya habari vya kuvuta (pull). Facebook na Instagram, na majukwaa kama hayo ni vyombo vya habari vya kusukuma. Tunaweka maudhui ambayo tunatumaini yanagusa watu na yangewachochea kubofya, kujifunza zaidi na kutazama zaidi. Injini za utafutaji, kama Google au YouTube, ni mkakati wa kuvuta, ambapo watu tayari wanaonyesha nia yao kupitia kile wanachokitafuta. Mambo kama, “Ninapataje Biblia?” au “Yesu ni nani?” Lengo hapo ni kuwavuta kutoka kwenye ukurasa wa matokeo ya injini ya utafutaji hadi mahali ambapo wanaweza kuufahamu ujumbe na “kuutafakari,” kujifunza zaidi na kujenga hali ya kuaminiana. Kisha tunatumaini watawasiliana nasi na kutuma maoni.
Ikiwa timu ndiyo inaanza tu, ningependekeza kufanya kazi kwa njia ya asili (organically). Jifunze jambo moja tu na ulimudu hilo kwanza, hata kama ni kitu kama programu ya Biblia ya YouVersion, ambapo unaweka Maandiko katika lugha za mahali hapo juu ya picha nzuri ya mahali hapo. Fanya mambo kama hayo kabla hujaanza kurusha matangazo kila mahali au kujaribu kufanya chochote kingine. Jifunze na uone ni maneno gani watu wanayachagua katika utafutaji wa Google, na uweke kitu pale. Unaweza kuwa wa moja kwa moja kabisa, na yaelekea utaona kwamba hakuna ushindani mwingi wala gharama kubwa katika maeneo ya aina hiyo. Watu wanaotujia sisi katika Kavanah Media kwa kawaida ni mashirika au timu ambazo tayari zimechanganyikiwa. Ama wamezidiwa na mambo haya au wamekuwa wakiyafanya na kugundua, “Hii haionekani kufanya kazi.” Tunazama ndani na kusema, “Hizi ni baadhi ya sababu za kiufundi, au hizi ni baadhi ya sababu za kimasoko, au sehemu nyingine zake.” Huenda marekebisho madogo tu yangesaidia. Wakati mwingine hakuna kosa lolote. Wamefanya kila kitu vizuri. Wanahitaji tu mtu wa kusema, “Mnafanya vizuri. Endeleeni tu!”
Lakini kwa sasa kuna kiwango kikubwa cha uchovu uliokithiri. Mashirika matatu tofauti ya umisheni yamenijia faraghani na kusema, “Watu wetu wamechanganyikiwa na wamechoka kabisa.” Nadhani sehemu ya hilo inatokana na matarajio yasiyo halisi. Inachukua miezi sita hadi mwaka mmoja kabla huenda ukaona mafanikio ya aina yoyote, kutegemea nchi unayofanyia kazi. Katika Kavanah Media, tunaona watu wanaoingia ndani yake kisha kusema, “Sikwenda uwandani ili kujifunza Facebook. Nilikwenda uwandani kwa sababu nilitaka kuzungumza na watu kuhusu Yesu.” Mojawapo ya mambo ninayoyathamini kuhusu hilo ni kubaki “katika njia yako ya kuogelea.” Wewe unafanya nini vizuri? Fanya hilo vizuri na waache wengine waliobobea katika mambo mengine wayafanye mambo hayo. Kisha fikiria: tunawezaje kufanya kazi pamoja? Kama mtu angenijia na kusema, “Niko katika nchi X na ninataka kufanya mkakati huu wa vyombo vya habari,” huenda ningemuuliza, “Ni nani mwingine tayari anayeufanya huko? Ungeweza kushirikiana na nani? Ni watu gani wa mahali hapo tayari wanahusika katika juhudi hizo?”
Tunataka kuongeza ufanisi wa juhudi badala ya kila mtu kujaribu kujifunza kila kitu na kutumia fedha nyingi mno kutengeneza video ambayo itadumu kwa dakika 15 tu. Hebu tutafute jinsi ya kuwa Mwili wa Kristo pamoja. Ikiwa mtu anahitaji msaada wa kiufundi, naweza kusaidia katika hilo. Lakini ikiwa wanahitaji kujifunza DMM, nitawapeleka kwa mtu mwenye utaalamu wa kufundisha DMM. Nimepitia mafunzo hayo, lakini waache wataalamu hao wafanye kile wanachokifanya vizuri sana. Ikiwa unataka kujifunza Adobe Premiere basi nitakutambulisha kwa baadhi ya watu bora wa vyombo vya habari walioko huko. Vyovyote itakavyokuwa, nadhani kuna thamani kubwa katika kuwatambulisha watu kwa wenzao, na kwa mambo ambayo tayari yanafanya kazi. Tunataka kuwasaidia watu wasibuni gurudumu upya.
Msimamizi24:14 ni muungano wa harakati, wenye harakati zaidi ya 1400 duniani kote kama sehemu ya muungano wetu. Ninavutiwa na mtazamo wao. Inaonekana kwamba Vyombo vya Habari kwa Harakati vinalenga sana kuanzisha kitu. Lakini je, kuna matumizi kwa harakati zilizopo? Je, yeyote kati yenu ana ushirikiano na harakati zilizopo?
JonNinafanya kazi na makundi mawili tofauti; moja linaendelea kutumia vyombo vya habari kufanya hivyo. Ukiangalia mahali ambapo watu wanaopita katika mfumo wao wanatoka, sehemu yao inatoka kupitia matangazo ya satelaiti, sehemu kupitia mitandao ya kijamii, sehemu kupitia tu watu wanaoshuhudia imani yao ndani ya teksi na mahali pengine popote. Unaona vipande hivi vyote vikija pamoja katika mfumo jumuishi unaowezesha ule ufuatiliaji muhimu, kama GP alivyosema. Watu wanafuatiliwa haraka na hakuna anayepotea njiani.
Kuna jingine ambalo ni harakati kamili, na kilichonishangaza sana kuhusu hilo ni kwamba wanajaribu kuongeza vyombo vya habari tena ndani ya harakati, kwa sababu wameshaweka mfumo. Wanasema, “Sasa tunaweza kuhudumia hata zaidi katika sehemu ya juu ya “funeli” yetu. Ni funeli inayoshuka hadi mahali ambapo inaanza kuenea. Hiyo ndiyo sehemu ya harakati. Kuwa na vipande hivyo vyote mahali pake kunaweza kufanya hivyo. Una huduma moja ambayo “imezaliwa kwa asili tu,” harakati ya uwandani tu ambayo sasa inaongeza vyombo vya habari ndani yake, na una nyingine ambayo kwa njia nyingi ilizaliwa kutokana na vyombo vya habari, lakini sehemu kubwa yake sasa haihusiani kabisa na vyombo vya habari. Ni watu tu walio uwandani, wakiona mambo yakitendeka. Ninathamini utofauti wa kazi ya Roho kote ulimwenguni katika hilo.
GPMimi pia. Si kitu kimoja kinachowafaa wote na hatuna risasi ya fedha. Huyu ni Roho wa Mungu akifanya kazi kote duniani. Kama Jon alivyosema, kuna kundi lenye harakati iliyoimarika ambalo tayari limeruka hadi katika lugha nyingine na nchi nyingine. Ni harakati kubwa mno ya harakati.
Wametumia vipengele mbalimbali vya vyombo vya habari, lakini walifikia hatua ya mgogoro ambapo walisema, “Lo! Tuna maelfu ya waamini wapya katika makundi mbalimbali ya watu na mafunzo tunayoyafanya hapa na viongozi hawa tunahitaji kuyaweka katika lugha nyingine.” Hilo ni hitaji la kipekee na la dharura. Tunaona timu nyingine zikiwa katika mwanzo kabisa wa kuanzisha kazi ya harakati. Wanataka kuona harakati, na wamekuwa wakitaabika kwa uaminifu lakini bado hawaoni mwitikio. Baadhi wanahisi wamezidiwa na hawahisi kwamba wanawafuatilia watu kwa ufanisi.
Tuna timu zilizo uwandani sasa zikisema, “Tunahitaji wataalamu wa vyombo vya habari kama sehemu ya timu yetu. Ile harakati ya harakati tuliyoitaja tayari imeruka hadi nchi nyingine. Wanasema, “Tunahitaji ujuzi huu laini. Tunahitaji wataalamu wa vyombo vya habari na wataalamu wa mawasiliano watakaotoa muda kujenga mahusiano ya kuaminiana na kufanya kazi bega kwa bega na viongozi wa harakati.”
Nataka kuwatia moyo kwamba Mungu anafanya jambo fulani. Hili si mtu mmoja tu au kundi moja tu. Huu ni mwili wa Kristo ukiitikia mambo mawili: 1) mgogoro wetu wenyewe wa imani na hali za kukata tamaa, katikati ya 2) muunganiko wa kimataifa unaoongozwa na Roho wa wafuasi wa Kristo wanaofanya kazi katika vyombo vya habari, upandaji wa makanisa na kufanya wanafunzi, ambao wanataka kufanya kazi pamoja.
Mgogoro mzito ulionikosesha usingizi usiku ulikuwa kwamba tulikuwa tukitumia muda, juhudi, na fedha kuwafikia waliopotea mtandaoni, lakini kwa kweli hatukuwa tukizidisha wanafunzi uwandani, na kwamba Mungu angetuhukumu kwa hilo. Lakini Mungu katika rehema na huruma yake anatupa fursa ya kusema, “Tunaweza kufanya hili vizuri zaidi. Tunaweza kufanya hili kwa njia tofauti, kwa njia yenye ufanisi zaidi.”
Najua mmesikia usemi huu, “Ukiendelea kufanya jambo lile lile, utaendelea kupata matokeo yale yale.” Tunahitaji kutafakari:
- tunafanya nini kinachofanya kazi ambacho tunahitaji kuendelea kukifanya?
- tunafanya nini kisichofanya kazi ambacho tunahitaji kukibadilisha?
- tunafanya nini ambacho bado hakijazaa matunda, lakini tunahitaji kuvumilia? Mungu atuonyeshe hatua inayofuata!
MsimamiziAsanteni wanajopo. Tunatazamia kuona jinsi Mungu atakavyolitumia hili.
Viungo vingine vya ziada:
mediatomovements.org • kingdom.training • Christian Media Marketing Podcast • https://open.spotify.com show/4jpCpjr3Sjxvf5hHt7Mf6B • Media4Movements • Visual Story Network • Disciple Tools, Mobile • Ministry Forum • Indigitous Resources • Jesus Film • Project app, Indigitube • Scripture Earth • Max7 Animated Bible Stories • Kolo World app (Android na iOS) • Free Bible Images
Jumuiya za Mafunzo:
- Campfire Creatives - Jumuiya ya mtandaoni kwa watengenezaji wa maudhui ya vyombo vya habari yenye uzoefu mpana wa mafunzo ya Vyombo vya Habari na Sanaa kwa ajili ya Umisheni
- Zume—safari ya ufuasi inayopatikana katika lugha 40+, inafundisha vikundi vidogo jinsi ya kulitii Agizo Kuu na kuzidisha wanafunzi
- Mission Media Coach
Programu (Apps):
- https://thedmmplatform.com
- https://waha.app
- http://SPapp.website
Ilichapishwa kwa mara ya kwanza katika Mission Frontiers 44:5 (Sep./Okt. 2022), uk. 40-44. Frontier Ventures. Imeshirikishwa kwa ruhusa.


